1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoIvory Coast

Nigeria na Ivory Coast zatinga fainali za AFCON

Lilian Mtono
8 Februari 2024

Mabingwa mara tatu wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Nigeria wamefanikiwa kuingia kwenye fainali za AFCON baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/4c9T1
Picha ya pamoja na Sebastien Haller na Victor Osimhen
Wachezaji vinara wa timu ya Ivory Coast Sebastian Haller(kushoto) na Victor Osimhen wa Nigeria. Timu hizi ndizo zitakazopambana kwenye fainali za AFCONPicha: Kim Price/CSM via ZUMA Press Wire/picture alliance/Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Ivory Coast, wenyeji wa michuano hiyo ilifanikiwa kutinga fainali baada ya kuiondoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Nigeria ilipata ushindi huo baada ya mlinda lango Stanley Nwabali, kuokoa mikwaju miwili ya penati. Timu hizo zilimaliza mchezo kwa sare ya 1-1 jana Jumatano.

Nigeria ilishindwa mara tano kati ya mara sita katika hatua ya nusu fainali za michuano hiyo huko nyuma na sasa itakabiliana na wenyeji Ivory Coast katika fainali hizo zitakazochezwa siku ya Jumapili.

William Troost-Ekong aliipatia Nigeria bao la kuongoza, kabla ya Afrika Kusini kujipatia bao la kusawazisha katika dakika za mwisho, lililofungwa na Teboho Mokoena.

Soma pia:Nigeria yalenga kubeba taji la AFCON

Hata hivyo, mkosi ulikiangukia kikosi hicho baada ya mlinzi wake Grant Kekana kupigwa kadi nyekundu katika muda wa ziada, na kuipa nafasi Nigeria kuwaongezea kishindo na hatimaye kupoteza mechi hiyo kwenye mikwaju ya penati baada ya Nwabali kuokoa mashuti ya Mokoena na Evidence Makgopa.

AFCON I Nigeria dhidi ya Afrika Kusini
Mlinda lango wa Afrika Kusini akijaribu kuokoa shuti la penati lililopigwa na William Troost-Ekong, aliyeifungia Nigeria goli la kwanza katika nusu fainali za AFCONPicha: Themba Hadebe/AP/picture alliance

Kocha wa Nigeria Jose Peseiro aliwaambia waandishi wa habari "Ulikuwa ni ushindi mzuri dhidi ya kikosi bora kabisa na kilichojipanga vizuri zaidi kwenye michuano hiyo. Tulistahili kushinda, lakini Afrik a Kusini walistahili kushinda pia."

"Tulikuwa wazuri kwenye penati, kwa hiyo wachezaji wangu walistahili. Timu ilipambana vilivyo."

Na kwa upande mwingine, Sebastien Haller ameibuka shujaa katika mechi kati ya wenyeji Ivory Coast na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kuipatia timu yake bao pekee la ushindi na kuingia kwenye fainali za AFCON.

Ivory Coast yawashangaza wengi

Mshambuliaji huyo wa Borussia Dortmund ya Ujerumani ambaye kwa mara ya kwanza alianza kwenye mchezo huo, kutokana na kuwa majeruhi hapo kabla, alifunga bao hilo baada ya pasi safi kutoka kwa Max-Alain Gradel katika dakika ya 65. mechi hiyo ilichezwa kwenye uwanja wa Ebimpe Olympic.

Ushindi huo hatimaye uliwapunguzia kishindo wakati wakijiandaa kukutana na Nigeria kwenye fainali zitakazopigwa kwenye uwanja huohuo siku ya Jumapili.

Mabingwa hao wa mara mbili wa AFCON wanakuwa wenyeji wa kwanza wa michuano hiyo kuingia fainali tangu Misri ilipoingia fainali za mwaka 2006, na hatua hii imewashangaza wengi kwa kuwa timu hiyo ilikuwa hatarini kutolewa katika hatua za makundi.

Mpinzani wake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ilifanikiwa kunyakua ubingwa wa AFCON mnamo mwaka 1974, wakati huo ikijulikana kama Zaire.

Kocha wa Ivory Coast Emerse Fae, aliyechukua nafasi ya Jean-Louis Gasset aliyetimuliwa kufuatia matokeo ya hovyo katika hatua za makundi ameutaja ushindi huo kama "miujiza."

Soma pia:Cote d'Ivoire, Cape Verde zaingia robo fainali AFCON