1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab yashambulia kambi ya Manda Bay, Kenya

Iddi Ssessanga
5 Januari 2020

Kundi la Al-Shabaab limefanya mashambulizi mapema Jumapili, dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Kenya, inayotumiwa na wanajeshi wa Marekani na Kenya. Lakini Kenya imesema imefanikiwa kuzuwia mashambulizi hayo bila madhara.

https://p.dw.com/p/3VjCn
Somalien Al-Shabaab-Kämpfer
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. A. Warsameh

Kundi hilo la itikadi kali limeielezea kambi hiyo, karibu na mpaka wa Somalia, kama "moja ya vituo kadhaa vinavyotumiwa katika vita vya msalaba vya Marekani dhidi ya Uislamu katika kanda hiyo."

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Luteni Kanali Paul Njuguma alisema wapiganaji walivamia tu uwanja wa ndege wa Manda na siyo kambi ya jeshi ya Simba kama ilivyodai Al-Shabaab. Uwanja huo wa kiraia pia unatumika kama lango la kuingilia kambini hapo.

"Hiyo ilikuwa propaganda," alisema Njuguna, akipinga madai ya Al-Shabaab. Katika ujumbe wa Twitter, KDDF ilisema: "Alfajiri ya leo majira ya saa 11:30, kulikuwepo na jaribio la kuvuruga usalama katika uwanja wa ndege wa Manda. Jaribio hilo lilizuwiwa kwa ufanisi."

"Mpaka sasa miili minne ya magaidi imegunduliwa. Uwanja wa ndege uko salama," uliendelea kusema ujumbe huo wa Twitter. Hakujaripotiwa maafa yoyote kwa wanajeshi wa Marekani au Kenya.

Jeshi la Kenya lilisema moshi unaoonekana kwenye mkanda kutoka eneo la tukio unatoka kwenye gari la mafuta lililoathiriwa katika uvamizi huo, na kwamba moto huo umedhibitiwa "na taratibu za kawaida za kiusalama zinaendelea."

Kenia | Camp Simba
Kambi ya Simba iliyoko Manda Bay, kaunti ya Lamu nchini Kenya ambayo Al-Shabaab ilidai kuishambulia.Picha: picture-alliance/AP Photo/Staff Sgt. L. West

Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika pia ilitoa ujumbe wa Twitter, ikikiri kwamba ilikuwa inafuatilia hali hiyo, lakini haikutoa maelezo zaidi. Marekani imefanya mashambulizi kadhaa yanayoilenga Al-Shabaab nchini Somalia.

Marekani inavisaidia vikosi vya Somalia pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Afrika katika mapambano dhidi ya Al-Shabaab, ambalo lina mafungamano na mtaadao wa Al-Qaeda.

Al-Shabaab yadai kuhusika

Al-Shabaab ilichapisha picha za wapiganaji wake waliofunika nyuso wakiwa karibu na ndege iliyokuwa inawaka moto, ingawa picha hizo hazikuweza kuthibitishwa na wachambuzi huru.

"Ndege saba na gari tatu za kijeshi ziliharibiwa katika shambulio," ilisema Al-Shabaab katika taarifa yake iliyohusisha picha zinazoonyesha ndege ikiwaka moto huku wapiganaji wake wakiwa wamesimama kando na ndege hiyo.

Kundi hilo la wapiganaji limedai kuhusika na shambulio hilo katika kaunti ya Lamu kwenye pwani ya Bahari ya Hindi nchini Kenya, eneo ambalo limekuwa kituo cha utalii kwa muda mrefu, lakini lililoko katika hatari ya vurugu za wanamgambo kutokana na ukaribu wake na Somalia.

Kenya ilituma wanajeshi nchini Somalia mwaka 2011 kufuatia mkururu wa mashambulizi ya kuvuka mpaka na matukio ya utekaji nyara.

Wanajeshi hao baadae waliingizwa katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika, ambacho kwa sasa kinao jumla ya wanajeshi 21,000, kinachosaidia serikali dhaifu inayoungwa mkono na mataifa ya magahribi dhidi ya Al-Shabaab.

Kenia Drei Tote bei Überfall auf Bus
Al-Shabaab imekuwa ikilenga pia shabaha za kiraia, kama basi hili lililoshambuliwa katika eneo la Nyongoro, kaunti ya Lamu, Januari 2, 2020.Picha: picture-alliance/AP Photo

Mwendelezo wa mashambulizi

Shambulio hilo la karibuni limefanyika wiki moja tu baada ya bomu la Al-Shaab lililotegwa ndani ya lori kuuwa watu wasiopungua 79 katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na Marekani kuuwa wapiganaji saba wa Al-Shabaab katika mashambuliji ya kujibu.

Mwaka uliyopita Al-Shabaab ilishambulia kambi ya jeshi la Marekani ndani ya Somalia. Kundi hilo pia limeendesha mashambulizi kadhaa dhidi ya wanajeshi wa Kenya huko nyuma likiiadhibu nchi hiyo kwa hatua yake ya kupeleka majeshi Somalia kupambana nalo.

Al-Shabaab pia imeshambulia shabaha za kiraia nchini Kenya, yakiwemo mabasi, shule na maduka makubwa. Shambulio la mapema Jumapili limekuja siku chache baada ya shambulio la ndege ya Marekani kumuuwa kamanda wa juu wa jeshi la Iran na Iran kuapa kulipiza kisasi.

Lakini kundi la Al-Shabaab linafuata madhehebu ya Kisunni na hakuna ishara yoyote ya uhusiano na Iran inayofuata madhehebu ya kishia au mawakala wake.

Vyanzo: dpae