1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Marekani azuru Afghanistan

Angela Mdungu
22 Machi 2021

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, amesema utawala wa Rais Joe Biden unataka kuona vita ikikomeshwa kwa namna yenye kuwajibika katika vita ya muda mrefu nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/3qx1P
Lloyd Austin in Afghanistan
Picha: Presidential Palace/AP/picture alliance

Katika ziara hiyo, Waziri Austin amesema vurugu zinapaswa kupungua ili diplomasia yenye manufaa ipate nafasi. Akizungumzia juu ya muda wa vikosi vya Marekani kuondoka Afghanistan, Austin amesema, "Kuhusu tarehe ya mwisho ama tarehe maalumu iliyowekwa ya kuwaondoa wanajeshi hili liko mikononi mwa bosi wangu. Huo ni uamuzi utakaofanywa na rais hapo baadaye kwa kutegemea namna anavyotaka kulishughulikia ili kusonga mbele, na sitaki kujaribu kuingilia kufanya kazi ya bosi wangu."

Kwenye ziara hiyo katika mji mkuu wa Afganistan, Kabul waziri huyo wa ulinzi wa Marekani alikutana na makamanda wa jeshi na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali akiwemo Rais Ashraf Ghani.

Wiki iliyopita, Rais wa Marekani Joe Biden, alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha ABC cha nchini mwake alisema itakuwa ngumu kwa Marekani kuviondoa vikosi vyake nchini Afghanistan kwa wakati uliopangwa yaani, tarehe mosi mwezi Mei.

Hata hivyo, Biden aliongeza kuwa ikiwa muda huo ambao uliwekwa kama sehemu ya makubaliano kati ya rais aliyemaliza muda wake Donald Trump na kundi la Taliban utaongezwa basi huenda zoezi hilo likachukua muda mrefu zaidi.

Lloyd Austin in Afghanistan
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyid Austin (kushoto) na Rais wa Afghanistan Ashraf GhaniPicha: Presidential Palace/AP/picture alliance

Ijumaa iliyopita, Taliban iliionya Marekani kuwa ikiwa haitozingatia tarehe iliyokubaliwa itapaswa kukabiliana na matokeo ya kufanya hivyo. Mmoja wa wajumbe wa timu ya mazungumzo wa upande wa Taliban Suhail Shaheen, aliwaambia waandishi habari kuwa, ikiwa vikosi hivyo vya Marekani vitakaa muda zaidi ya tarehe mosi mwezi Mei, jambo hilo litakuwa ni ukiukaji wa makubaliano na si kutoka upande wao.

Licha ya mazungumzo ya amani machafuko yaendelea Afghanistan

Wakati huo huo, machafuko yanaendelea kushuhudiwa nchini Afganistan licha ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya nchi hiyo inayotambuliwa kimataifa na kundi la Taliban, ambalo limekuwa likikataa kuweka chini silaha.

Msemaji wa kundi hilo hapo jana alisema kuwa, mpango wa pamoja wa kupunguza vurugu hizo ukiwashirikisha maafisa wa Marekani umekuwa kwa muda mrefu sasa bila kuwa na meaelezo ya kutosha ya mpango huo.

Kauli iliyotolewa na ikulu ya Afghanistan baada ya mkutano wa Rais Ghani na waziri ulinzi wa Marekani inasema, pande zote zimelaani machafuko yanayoendelea Afghanistan.