1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndia

Urusi yashtumu nchi za Magharibi kuiwekea India shinikizo

8 Septemba 2023

Viongozi wa G20 wanaendelea kuwasili New Delhi kwa mkutano wa kilele unaoanza kesho Jumamosi kujadili sera za usalama wa chakula, matatizo ya madeni na jinsi ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/4W7xS
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akiwahili New Delhi kuelekea mkutano wa G20
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akiwahili New Delhi kuelekea mkutano wa G20Picha: Amit Dave/REUTERS

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov tayari amewasili India kuongoza ujumbe wa Moscow kwa niaba ya Rais Vladimir Putin.

Putin hatohudhuria mkutano huo wala kuhutubia kwa njia ya video katikati ya msuguano kati ya Moscow na baadhi ya nchi wanachama wa G20 juu ya vita vya Ukraine.

Rais wa China Xi Jinping pia hatohudhuria mkutano huo na badala yake atawakilishwa na Waziri Mkuu Li Qiang.

Soma pia: Viongozi wa G20 waliogawika waelekea India kwa mkutano wa kilele 

Kabla ya kuwasili kwa Lavrov mjini New Delhi, taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilieleza kuwa, mzozo wa Ukraine ulichochewa na Marekani na bado nchi hiyo inaendelea kuongeza mafuta kwenye moto na hivyo kuhatarisha usalama wa Ulaya.

Sunak: Kutokuwepo kwa Putin ni ishara ya kutengwa

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, aliyewasili New Delhi mapema leo mchana, amesema kuwa kutokuwepo kwa Putin kwenye mkutano huo kunaonyesha ni kwa jinsi gani kiongozi huyo wa Urusi anavyojichimbia shimo la kutengwa kidiplomasia.

Gazeti la Uingereza la The Financial Times limeripoti kuwa Sunak anatarajiwa kumuhimiza Waziri Mkuu wa India Narendra Modi "kuikosoa" Urusi juu ya uvamizi wake nchini Ukraine na kutumia ushawishi wake kusaidia kumaliza vita hivyo.

Urusi hata hivyo imeshutumu vikali kundi la nchi saba tajiri na zenye nguvu kiviwanda duniani G7 kwa kuiwekea India shinikizo. Kwa zaidi ya miezi 18, India imejaribu kuonyesha msimamo wa kutoegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine, ikionekana kufanya hivyo ili kutoikwaza Urusi ambayo ni moja kati ya washirika wake wa tangu zamani.

Lavrov amesisitiza kuwa, mkutano huo ni wa kujadili masuala ya kiuchumi na utulivu wa mfumo wa fedha duniani na wala sio kuhusu usalama wa kimataifa.

Moscow imeisifu India kwa kukataa miito ya mataifa ya Magharibi kuikaribisha Ukraine kama ilivyofanya mwenyeji Indonesia mwaka uliopita katika mkutano wa G20 uliofanyika Bali. Urusi imedai kulikuwepo na jaribio la G7 la kupanua ajenda ya mkutano huo na kujumuisha pia usalama wa kimataifa.

India yataka azimio la G20 kujumuisha maoni ya Urusi na China

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel
Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles MichelPicha: Sajjad Hussain/AFP/Getty Images

India kwa upande wake imesema leo kuwa nchi za G20 tayari zinakaribia kufikia azimio la pamoja na kuashiria kuwa wapatanishi wamepiga hatua katika kusuluhisha tofauti miongoni mwa nchi wanachama juu ya vita vya nchini Ukraine.

India inataka azimio la mwisho la pamoja la G20, kujumuisha pia maoni ya Urusi na China.

Soma pia: Mkutano wa G20 kumalizika India bila tamko la pamoja

Hata hivyo Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ameeleza kuwa, itakuwa vigumu mno kutabiri iwapo viongozi hao wa G20 wanaweza kufikia makubaliano juu ya azimio la pamoja na kutoa wito kwa hatua kali zaidi kuchukuliwa dhidi ya Urusi.

"Nadhani tunahitaji kuihimiza China kuchukua nafasi ya uwajibikaji katika ngazi ya kimataifa, kutetea Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kutetea uhuru wa Ukraine"

Wachambuzi wamesema kuwa migawanyiko juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine inatishia kukwamisha maendeleo juu ya masuala muhimu kama vile usalama wa chakula, afueni ya madeni na ushirikiano wa kimataifa wa kupambana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.

Rais wa Marekani Joe Biden, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres miongoni mwa viongozi wengine, wanahudhuria mkutano huo.