1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Umoja wa Ulaya zashindwa kuwafikiana

Mohammed Abdulrahman
27 Machi 2018

Baada ya mazungumzo na Rais wa Uturuki mjini Varna, Bulgaria, Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema umoja huo una wasiwasi juu ya utawala wa sheria nchini Uturuki, na wameshindwa kuwafikiana katika masuala mazito.

https://p.dw.com/p/2v3OA
Bulgarien EU- Türkei Gipfel: Präsident Donald Tusk, Tayyip Erdogan und Jean-Claude Juncker
Picha: Reuters/S. Nenov

Mkutano huo, kati ya Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk, Rais wa Halmashauri Kuu ya umoja huo Jean Claude Juncker na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ulishindwa kuwasogeza pamoja katika masuala mazito.

Akiulizwa na waandishi habari iwapo yamefikiwa maridhiano au maamuzi yoyote katika mkutano wao, Tusk alisema alimuelezea Rais Recep Tayyep Erdogan wasiwasi wake kuhusu  kuheshimiwa kwa utawala wa kisheria nchini Uturuki na kutaja kwamba ilikuwa ni orodha ndefu. Tusk akongeza kwamba ikiwa angeulizwa iwapo kuna maridhiano au ufumbuzi uliofikiwa katika baadhi ya masuala, rais huyo wa Umoja wa Ulaya  angesema hapana.

Tusk alisema amekosoa vikali kukamatwa kwa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya nchini Uturuki pamoja na kuzuiliwa na Uturuki kwa visima vya gesi nje ya mwambao wa Cyprus, huku  akielezea pia hofu aliyonayo kuhusu hatua ya kijeshi ya Uturuki nchini Syria. 

"Tunaelewa haja ya Uturuki kushughulikia kwa ufanisi usalama wake baada ya jaribio la mapinduzi na mashambulizi ya kigaidi iliyoyapata, lakini tuna wasiwasi kwamba baadhi ya mbinu zinazotumika zinadhoofisha misingi ya uhuru na utawala wa sheria Uturuki," amesema Tusk.

Bulgarien Warna EU Türkei Gipfel Erdogan, Boyko Borisow, Donald Tusk und Jean-Claude Juncker
Kutoka kushoto: Rais wa Uturuki Reccep Erdogan, Waziri Mkuu wa Bulgaria Boyko Borisow, Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk, Rais wa halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ean-Claude Juncker .Picha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Erdogan ana matumaini

Lakini pamoja na  maelezo hayo ya Tusk, Erdogan alielekea kuwa na matumaini kwamba uhusiano kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya bado unaweza kurudi tena kuwa bora na ana matumaini kuwa kipindi cha matatizo sasa kimewekwa kando. Umoja wa Ulaya, umeendelea kuikosoa Uturuki baada ya karibu watu 160,000 kukamatwa wakiwemo waandishi habari, kufuatia jaribio  la mapinduzi lililoshindwa. Aidha, Erdogan ameukosoa umoja huo akisema ulishindwa kuonyesha mshikamano na serikali yake, baada ya kulikandamiza jaribio hilo la mapinduzi.

"Uturuki inaheshimu haki za msingi za binadamu na ni nchi inayoheshimu haki za binadamu, hii ni dhahiri katika matukio ya tarhe 15 Julai wakati wa jaribio la mapinduzi. Operesheni zetu dhidi ya ugaidi zitaendelea siku zote ikiwa kitisho hiki kinaendelea kuwepo na tutafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha usalama," amesema Erdogan, akizungumzia suala la haki za binaadamu.

Rais wa Uturuki akazungumzia suala la nchi yake kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya tokea 1963 akisisitiza kwamba bado Urutuki inapigania uwanachama huo na kuutaka Umoja wa Ulaya uanze tena mazungumzo ambayo yamekwama tokea mwishoni mwa mwaka 2016.

Amesema litakuwa ni kosa kwa upande wa Umoja wa Ulaya ambao unataka mchango wake katika masuala ya kimataifa utanuke zaidi, huku ukiiweka kando  Uturuki. Erdogan alitoa wito wa mageuzi ya haraka katika suala la umoja wa  orodha na akagusia juu ya mapendekezo ya serikali yake mwezi Februari, kuhusu jinsi Uturuki itakavyoweza kupiga hatua ya maendeleo katika suala la uhuru wa utoaji visa.

Kwa upande wake Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker alisema pasina shaka yoyote, umoja huo utaheshimu ahadi ulizotoa, ukitenga euro bilioni 3 kuwasaidia wakimbizi wa Syria walioko Uturuki. Mnamo Machi 2016, Umoja wa Ulaya na Uturuki zilikubaliana kuzuwia wimbi la wahamiaji, katika kile kilichoelezwa kuwa mkataba wa aina yake huku Uturuki ikitarajia kwamba itapatiwa ridhaa katika suala la visa kuingia Ulaya. Kwa sasa pande hizo mbili zingali bado mbali na maafikiano katika masuala kadhaa.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahmanm, dpa, afp

Mhariri: Mohammed Khelef