1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Yemen ajiuzulu

23 Januari 2015

Bunge la Yemen litakutana kwa dharura siku ya Jumapili kutokana na kujiuzulu kwa Rais Abdrabuh Mansour Hadi wa nchi hiyo, kufuatia mzozo wa kisiasa kati ya serikali ya Wasuni na wapiganaji wa Kishia wa Huthi.

https://p.dw.com/p/1EPRn
Rais Abdrabuh Mansour Hadi wa Yemen
Rais Abdrabuh Mansour Hadi wa YemenPicha: picture-alliance/AP/J. DeCrow

Rais Hadi ambaye ni mshirika mkuu wa Marekani katika kupambana na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, ameandika barua ya kujiuzulu hapo jana, akisema hawezi kuendelea kubakia madarakani wakati nchi hiyo ikidumbukia katika hali ya ghasia. Hadi ameufikia uamuzi huo baada ya mji mkuu wa Yemen, Sanaa, kuwa chini ya wapiganaji wa Huthi.

Amesema anaamini ameshindwa kufikia malengo yake ya kikazi na kwamba viongozi wa kisiasa wa Yemen wameshindwa kuiongoza nchi hiyo katika hali ya utulivu, baada ya kutofanikiwa kuumaliza mzozo uliopo.

Waziri Mkuu wa Yemen, Khalid Bahah pia amejiuzulu, akisema hataki kuwa sehemu ya kuanguka kwa nchi hiyo. Hata hivyo, bunge la Yemen limeukataa uamuzi wa Rais Hadi kujiuzulu.

Wapiganaji wa Huthi
Wapiganaji wa HuthiPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

Tangazo hilo la kushtusha limetolewa wakati ambapo wanamgambo wa Huthi wamechukua udhibiti kamili wa mji mkuu wa Sanaa, baada ya mwezi Septemba mwaka uliopita, kuyatwaa maeneo mengi ya mji huo. Wapiganaji hao jana waliendelea kumshikilia msaidizi mwandamizi wa rais, ambaye walimteka nyara siku ya Jumamosi.

Marekani yawaondoa wafanyakazi wa ubalozi wake Sanaa

Wakati huo huo, Marekani imewaondoa baadhi ya wafanyakazi wake wa ubalozi kutoka kwenye mji wa Sanaa, kutokana na kuongezeka kwa mzozo wa kisiasa, hali inayoipa Marekani wasiwasi wa juhudi zake za kupambana na ugaidi nchini Yemen.

Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jen Psaki amesema ubalozi wa Marekani utaendelea kubakia wazi na kuendesha shughuli zake kama kawaida.

Jen Psaki, msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani
Jen Psaki, msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya MarekaniPicha: SAUL LOEB/AFP/Getty Images

''Bila shaka usalama na ulinzi kwa wafanyakazi wetu ni jambo muhimu. Tumejiandaa kurekebisha mambo na kuwaondoa wafanyakazi wetu iwapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo, lakini hakuna mabadiliko yoyote yale kuhusu uwepo wetu katika suala la usalama, alisema Psaki.''

Amefafanua kuwa Marekani itaendelea kuunga mkono makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani wakati wa kipindi cha mpito. Amesema Marekani ilikuwa na matumaini kwamba mazungumzo kati ya makundi yanayohasimiana nchini Yemen yataendelea, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuumaliza mzozo uliopo.

Yemen ni ngome muhimu ya tawi la kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Uarabuni-AQAP, linaloonekana kuwa hatari, ambalo hivi karibuni lilikiri kuhusika na shambulizi la kigaidi katika jarida la vikaragosi la Ufaransa la Charlie Hebdo na kuwaua watu 12. Yemen imeiruhusu Marekani kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Al-Qaeda nchini humo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri:Yusuf Saumu