1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais Liberia: George Weah akiri kushindwa

18 Novemba 2023

Kiongozi wa Liberia na mwanasoka nyota wa zamani George Weah amekiri kushindwa na mpinzani wake Joseph Boakai katika awamu ya pili ya uchaguzi mkuu wa Urais baada ya kinyang'anyiro kikali.

https://p.dw.com/p/4Z8CU
| George Manneh Weah, Rais wa Liberia
Rais wa Liberia George WeahPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Weah amesema ni wakati wa kuweka mbele maslahi ya Liberia badala ya maslahi binafsi. Matokeo ya awali yaliyokaribia kukamilika yalionesha kuwa Boakai aliyewahi kuwa makamu wa rais,  anaongoza kwa karibu asilimia 51 ya kura katika taifa hilo lililoanzishwa na waliokuwa watumwa huko Amerika baada ya kuachiwa huru.

Ijumaa jioni, Weah aliyekuwa akitafuta kutetea kiti chake alitoa hotuba katika redio ya taifa akisema kuwa, "Matokeo yaliyotangazwa usiku, ingawa si ya mwisho, yanaonesha kuwa Boakai anaongoza kwa kiasi ambacho hatuwezi kumfikia na kumshinda". Aliongeza kuwa chama chake cha CDC "kimeshindwa uchaguzi lakini Liberia imeshinda".

Soma zaidi: Raia wa Liberia kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais

Kulingana na tume ya uchaguzi ya nchini humo, wakati asilimia 99.5 ya vituo vya kupiga kura vikiripoti hesabu za kura baada ya uchaguzi huo wa Jumanne, Boakai alishajipatia asilimia 50.89 ya kura. Kiongozi huyo alikuwa akiongoza kwa kura 28,000 dhidi ya Weah.

Wawili hao walikamilisha awamu ya kwanza ya uchaguzi mwezi kwa tofauti ndogo ya kura Boakai alikiongoza kwa kura 7,126 pekee. Joseph Boakai mwenye miaka 78 alishindwa na Weah kwa tofauti kubwa ya kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa mwaka 2017.

Awali, kuchaguliwa kwa Weah wakati alipoingia madarakani kuliibua matumaini mapya ya mabadiliko katika taifa hilo lakini wakosoaji wameituhumu serikali yake kwa ubadhirifu na wamemtuhumu Weah mwenyewe kwa kushindwa kuitimiza ahadi yake ya kuboresha maisha ya watu masikini.

Marekani yatuma salamu zapongezi kwa Boakai

Kufuatia uchaguzi huo, Marekani imetuma salamu za pongezi Joseph Boakai na kwa Weah kwa kukubali kwake matokeo kwa amani. Msemaji wa Wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani Matthew Miller katika taarifa yake ametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kufuata mfano wa Weah na kukubali matokeo.

Liberia | Aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Liberia  Joseph Boakai
Joseph Boakai Picha: Carielle Doe/REUTERS

Kwa upande wake George Weah alisema kuwa amezungumza na Boakai na kumpongeza kwa ushindi huo. Hata hivyo anaendelea kuwa rais hadi atakapokabidhi rasmi madaraka mwezi Januari na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya mustakabali mzuri wa Liberia.

Uchaguzi wa mwaka huu wa Liberia ni wa kwanza kufanyika tangu Umoja wa Mataifa ulipouondoa ujumbe wake wa kulinda amani mwaka 2018 ambao ulipelekwa baada ya watu zaidi ya 250,000 kuuwawa katika awamu mbili za vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya miaka ya 1989 na 2003.

Waangalizi wa kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya wameipongeza Liberia kwa kufanya uchaguzi wa amani. Nayo jumuiya ya umuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imesema uchaguzi huo ulikuwa wa amani kwa kiasi kikubwa lakini uliainisha matukio kadhaa yaliyosababisha watu kujeruhiwa na kulazwa katika mikoa minne.