1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa majeshi Kenya afariki katika ajali ya ndege

Sylvia Mwehozi
18 Aprili 2024

Mkuu wa Majeshi wa Kenya Francis Ogolla ni miongoni mwa watu waliofariki katika ajali ya ndege ya kijeshi iliyoanguka katika mpaka wa Kaben-Cheptule

https://p.dw.com/p/4ewXu
Mkuu wa majeshi wa Kenya Francis Ogolla wakati wa uhai wake
Mkuu wa vikosi vya ulinzi wa Kenya Jenerali Francis Omondi Ogolla wakati wa uhai wakePicha: LUIS TATO/AFP/Getty Images

Rais wa Kenya  William Ruto ametangaza kuwa Mkuu wa majeshi wa Kenya Jenerali Francis Omondi Ogolla ni miongoni mwa watu 10 waliofariki katika ajali ya helikopita.

"Leo saa nane mchana, taifa letu lilipata ajali mbaya ya angani... Nina huzuni kubwa kutangaza kifo cha Jenerali Francis Omondi Ogolla," Ruto amewaeleza waandishi wa habari, akiongeza kuwa maafisa wengine tisa pia waliuawa huku wawili wakinusurika.

 Amesema Jeshi la wanaanga la Kenya limetuma timu ya uchunguzi wa anga ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, iliyotokea katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, takriban kilomita 400 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Nairobi.

Ndege ya KDF
Ndege ya jeshi la Kenya KDFPicha: Reuters/B. Ratner

Kabla ya tangazo hilo, Ruto aliitisha mkutano wa dharura wa baraza la usalama la nchi hiyo, baada ya helikopta inayoripotiwa kuwa ilikuwa imewabeba maafisa wakuu wa kijeshi kuanguka.

Mkuu wa vikosi vya ulinzi Jenerali Francis Omondi Ogolla alikuwa miongoni mwa waliokuwemo kwenye helikopta hiyo iliyoanguka katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, takriban kilomita 400 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Nairobi. Ripoti hizo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya.

Jenerali Ogolla alikuwa kwenye shughuli za kikazi wakati ajali hiyo ilipotokea.

Rais Ruto ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti. Viongozi mbalimbali akiwemo rais mstaafu Uhuru Kenyatta wametuma salamu za rambirambi kwa familia na kusema taifa limepata pigo. 

Taarifa za awali.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisema kwenye taarifa yake kwamba "Rais William Ruto ameitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Kitaifa katika Ikulu ya Nairobi jioni ya leo kufuatia ajali ya helikopta ya Jeshi la Kenya alasiri ya leo katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet."

Taarifa za awali zilizotolewa na chanzo kimoja cha polisi kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina askari watano wamefariki papo hapo na wengine watatu wamenusurika wakati ndege hiyo ilipoanguka, limeripoti shirika la habari la Reuters.

Ndege ya kijeshi ya Kenya
Helkopita ya jeshi la Kenya KDFPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura kupitia mtandao wakijamii wa X, amesema kwamba taarifa rasmi kuhusu ajali hiyo itatolewa hivi karibuni.

Ogolla, 61, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Ruto Aprili mwaka jana. Ruto aliwaambia waandishi wa habari mwezi Mei mwaka jana kwamba alimteua Ogolla licha ya yeye kuwa miongoni mwa waliojaribu kubatilisha ushindi wake mdogo wa uchaguzi dhidi ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga mwaka wa 2022.Kenya kuviondoa vikosi vya jeshi Somalia

 "Nilipotazama wasifu wake, alikuwa mtu bora zaidi kuwa jenerali," alisema Ruto, akiongeza kuwa uamuzi wake ulikwenda kinyume na matakwa ya watu wengi. 

Ogolla alijiunga na KDF mnamo Aprili 1984, akipanda ngazi hadi kuwa kamanda wa Jeshi la wanaanga la Kenya mnamo 2018, wadhifa alioshikilia kwa miaka mitatu.