1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Marekani yapiga zaidi ya vituo 85 vya wanamgambo Syria, Iraq

Iddi Ssessanga
3 Februari 2024

Jeshi la Marekani limesema jana kuwa limeshambulia vituo zaidi ya 85 nchini Syria na Iraq, kujibu shambulio baya lililofanywa na wanamgambo wanaoiunga mkono Iran, na kuuwa wanajeshi watatu wa Marekani nchini Jordan.

https://p.dw.com/p/4bzm0
Kituo cha kijeshi cha Marekani cha Tower 22
MArekani imefanya mashambulizi hayo kujibu mauaji dhidi ya askari wake katika kambi hii iliyopo Jordan.Picha: Planet Labs PBC/AP/dpa/picture alliance

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu nchini Syria, lenye makao yake nchini Uingereza, limesema katika taarifa kwamba ndege za kivita za Marekani zimefanya duru kadhaa za mashambulizi dhidi ya maeneo kwenye urefu wa kilomita 130 kuanzia mji wa Deir e-Zour hadi mpaka wa Syria na Iraq.

Soma pia: Biden aamua kujibu shambulizi lililotokea Jordan

Shirika hilo limesema wanamgambo wasiopungua 18 wanaoiunga mkono Iran wameuawa. Kamandi ya kanda ya jeshi la Marekani, CENTCOM, imethibitisha mashambulizi hayo kupitia mtandao wa X, na kusema maeneo yalioshambuliwa ni pamoja na vituo vya kamandi na udhibiti wa operesheni, intelijensia, hifadhi za maroketi, makombora na droni miongoni mwa vingine.

Ikulu ya White House imesema Marekani hatitaki vita na Iran licha ya mashambulizi hayo.