1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Mashambulizi ya Iran hayatapoteza lengo letu Gaza

15 Aprili 2024

Israel imefanya mashambulizi ya usiku kucha katika Ukanda wa Gaza, huku jeshi lake likisema halitopoteza mwelekeo katika vita vyake Gaza kutokana na shambulio la Iran ambalo halijawahi kushuhudiwa.

https://p.dw.com/p/4elzj
Khan Yunis, Ukanda wa Gaza | mji ulioharibiwa kwa mashambulizi ya Israel.
Eneo la Ukanda wa Gaza la Khan Yunis lililoharibiwa vibaya na mashambulizi ya vikosi vya Israel, yaliochochewa na shambulio la Hamas la Oktoba, 7Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Jeshi la Israel limesema halitapoteza hata dakika moja katika oparesheni yake yenye lengo la kuwaokoa mateka wanaoshikiliwa na kundi la Hamas. 

Wakati wapatanishi wakiendelea  kutafuta suluhu ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yaliochochewa na shambulio la Hamas la Oktoba 7, hofu imeongezeka kwa Israel kupeleka wanajeshi zaidi katika mji wa kusini mwa Gaza, Rafah ambako wakaazi zaidi ya milioni 2.4 wa eneo hilo wamekimbilia ili kujilinda na mapigano yanayoendelea.

Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagar amesema kwamba licha ya mashambulio ya Iran, hawajapoteza lengo lao katika vita vyake ndani ya Ukanda wa Gaza katika kuwaokoa mateka takriban 130, ikiwemo 34 wanaohofiwa kuuwawa, ambao Israel inasema wamesalia katika mikono ya kundi la Hamas.

Soma pia:Baraza la Haki la UN lataka Israel kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita huko Gaza

Hagari ameongeza kwamba jeshi  litaongeza vikosi zaidi vya akiba kwa ajili ya ufanisi wa shughuli zake za kijeshi katika eneo la Rafah, ikiwa ni wiki moja tu tangu kuondoa idadi kubwa ya wanajeshi wakwe wa ardhini katika eneo hilo.

''Hamas hivi karibuni wamekaata pendekezo la kuachiliwa kwa mateka lililotolewa kwao na wapatanishi." Alisema katika taarifa yake.

Aliongeza kwamba Hamas na Iran wanataka kuweka Mashariki ya kati katika hali tete ya kiusalama hatua ambayo Israel haiko tayari hilo litokee.

"Tutaendelea kulinda taifa la Israel pamoja na washirika wetu, tutaendelea kujenga mustakabali ulio salama na dhabiti zaidi kwa Mashariki ya Kati nzima." Alisema, msemaji huyo wa IDF.

Makubaliano kuhusu kuachiliwa kwa mateka

Hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yalioafikiwa kati ya Israel na Hamas huku msimamo wa pande zote mbili ikiwa haujabadilika.

Hamas ilikataa mapendekezo yote ya maafikiano yaliotolewa na Israel, ikisisitiza kukomeshwa kabisa kwa mapigano na Israel kuondoa kikamilifu wanajeshi wake katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Katika hatua nyingine vyombo vya habari vinavyoendeshwa na Hamas vimesema kwamba ndege za Israel zimefanya mashambulizi kadhaa usiku wa kuamkia leo katika maeneo ya katikati mwa Gaza na kuwajeruhi watu kadhaa.

Taarifa hizo zilieleza kuwa jeshi la Israel pia lilifanya mashambulizi makali ya makombora katika eneo la kusini mashariki mwa Gaza, kadhalika wametekeleza mashambulizi ya anga kwenye ghala la kibiashara karibu na lango la kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Soma pia:Mapambano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas yapamba moto

Israel imeendesha mashambulizi hayo huku kukiwa na tetesi za kufunguliwa upya kwa kituo cha ukaguzi katika barabara ya pwani kwenye eneo hilo lililozingirwa.