1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yalaani mashambulizi ya Marekani

Zainab Aziz
24 Januari 2024

Iraq imeilaumu Marekani kwa kuchangia kuongezeka ghasia katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya Marekani kufanya mashambulizi ya anga kuyalenga makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq siku ya Jumatano.

https://p.dw.com/p/4bdiW
Irak | Al Asad
Kituo cha jeshi cha Al Asad nchini Iraq.Picha: Ayman Henny/AFP/Getty Images

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, alisema vikosi vya nchi yake vilifanya mashambulizi ambayo ni ya lazima dhidi ya vituo vitatu vinavyotumiwa na wanamgambo wa Kitaeb Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran na makundi mengine yenye uhusiano na Iran yaliyo nchini Iraq.

Lakini msemaji wa Waziri Mkuu wa Iraq alisema kitendo hicho hakikubaliki, kinakiuka hadhi ya mipaka na uhuru wa taifa hilo na kinadhoofisha ushirikiano wa miaka mingi, na wakati huo huo "kinachangia kuongezeka kwa migogoro" kwenye kanda nzima ya Mashariki ya Kati.