1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel: Karibu watu 50,000 waondoka kaskazini mwa Gaza

Lilian Mtono
9 Novemba 2023

Jeshi la Israel, karibu raia 50,000 wamekimbia kaskazini mwa Gaza na kuelekea kusini mwa eneo hilo la Palestina jana Jumatano, katikati ya mzozo unaozidi kutokota kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Hamas.

https://p.dw.com/p/4YagH
Vifaru vya jeshi la Israel kama vinavyoonekana wakati jeshi hilo likiendeleza operesheni ya ardhini katika eneo la Ukanda wa Gaza dhidi ya kundi la Hamas
Vifaru vya jeshi la Israel kama vinavyoonekana wakati jeshi hilo likiendeleza operesheni ya ardhini katika eneo la Ukanda wa Gaza dhidi ya kundi la HamasPicha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amenukuliwa akisema wameshuhudia wakazi hao wa Gaza wakiondoka na kuongeza kuwa wanaondoka kwa sababu wanajua kwamba tayari Hamas imepoteza udhibiti katika eneo la kaskazini na kwamba eneo la kusini liko salama zaidi.

Ameongeza kuwa hawatasitisha mapigano dhidi ya wanamgambo wa Hamas, lakini amesema Israel inaruhusu usitishwaji wa mapigano katika nyakati fulani ili kuruhusu misaada ya kiutu kuwafikia raia waliokimbilia kusini mwa Gaza.

Jeshi la Israel laharibu mahandaki 130 ya Hamas

Jeshi la Israel, IDF awali lilisema liliharibu mahandaki 130 ya wanamgambo wa Hamas tangu mzozo huo ulipoibuka mwezi mmoja uliopita. Kulingana na jeshi hilo, wanamgambo wa Hamas wana mtandao mkubwa wa mahandaki ya chini ya ardhi katika eneo la Ukanda wa Gaza.

IDF ilichapisha video zilizoonyesha vifaa vikichimba maeneo ya kuingia kwenye mahandaki na kuondoa vifuniko vilivyotengenezwa kwa saruji na kukuta vifaa vya kusambazia maji, hali iliyodhihirisha kwamba wanamgambo hao walikuwa wamejiandaa kukaa kwenye mahandaki hayo kwa muda mrefu. Baadhi ya mahandaki pia yalikuwa na umeme.

Soma Pia:Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G7 wakutana nchini Japan 

Mahandaki hayo yalikuwa na urefu wa mita mbili na upana wa mita moja, lakini baadhi yalikuwa na ukubwa wa kupitisha magari na yalichimbwa kwenda chini zaidi, na kuwa na uwezo wa kuhimili mashambulizi ya Israel.

Wakazi wa Palestina wakiwa wamebeba mali zao wakati wakiyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya Hamas.
Wakazi wa Palestina wakiwa wamebeba mali zao wakati wakiyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya Hamas.Picha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Italia kupeleka meli yenye hospitali karibu na pwani ya Gaza

Nje ya uwanja wa mapambano, Italia imesema imepeleka meli yenye hospitali karibu na eneo la maji la Gaza ili kusaidia kuwatibu wahanga wa mzozo huo, hii ikiwa ni kulingana na waziri wa ulinzi Guido Crosseto.

Soma pia: Jeshi la Israel lashambulia maeneo 450 Gaza

Meli hiyo imeondoka jana kutoka bandari ya Civitaveccia, magharibi mwa Italia ikiwa na watumishi 170, ambao ni pamoja na watu waliofunzwa kutoa huduma za dharura, amesema waziri huyo.

Meli hiyo itasimama Cyprus kabla ya kuelekea kwenye eneo lililo karibu zaidi na Ukanda wa Gaza, na majeruhi watapelekwa kwenye meli hiyo na kutibiwa kisha watarudishwa Gaza. Kulingana na Crosetto hii ni operesheni ya kwanza ya aina hii ya kiutu katika eneo hilo na anaamini mataifa mengine yatafuata nyayo zao.

soma pia: Guterres: Gaza yageuka uwanja wa makaburi kwa watoto

Katika hatua nyingine, Uholanzi imesema itapeleka meli ya kijeshi katika eneo la Cyprus kusaidia utoaji wa misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza. Meli hiyo pia inaweza kusaidia kuwaokoa watu, amesema waziri wa ulinzi wa Uholanzi Kajsa Ollongren.

Mzozo wa Mashariki ya kati unazidi kuwaathiri pakubwa wapalestina ambao kwa sasa wana uhitaji mkubwa wa maji, chakula, madawa na makaazi mapya, baada ya Israel kuendelea kuushambulia ukanda wa Gaza kwa makombora, kujibu mashambulizi yaliyofanywa Kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba na kundi la wanamgambo la Hamas na kusababisha vifo vya watu 1,400.

Sikiliza zaidi: 

Vita vya Israel na Hamas vyatimia mwezi mmoja