1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres asema Gaza yageuka uwanja wa makaburi kwa watoto

Josephat Charo
7 Novemba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameieleza hali katika Ukanda wa Gaza kuwa janga la kibinadamu. Hali ni ya wasiwasi mjini Jerusalem, Ukingo wa Magharibi na kwenye mpaka baina ya Israel na Lebanon.

https://p.dw.com/p/4YTvj
UN Secretary General Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akitoa hotuba kuhusu hali ya Gaza mjini New York 06.11.2023Picha: Mark J. Sullivan/Zumapress/picture alliance

Idadi ya Wapalestina waliouliwa Gaza tangu kuanza kwa vita mnamo Oktoba 7 kati ya Israel na kundi la Hamas, linalotambuliwa kama la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya, imepanda hadi kufikia 10,022, kwa mujibu wa wizara ya afya inayodhibitiwa na kundi hilo. Wizara hiyo inasema maalfu ya wanawake na vijana ni miongoni mwa wale waliuouliwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya kutokea angani na ya ardhini ya Israel.

Guterres amelilaani kundi la Hamas kwa vitendo vyake vya kigaidi na kurudia wito wake kutaka zaidi ya mateka 200 ambao wamekuwa wakishikiliwa na wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza kwa mwezi mmoja sasa, waachiwe huru mara moja. Pia amesema usitishwaji mapigano kuruhusu utoaji wa misaada ya kibinadamu sharti utekelezwe na Israel na watawala wa Hamas huko Gaza ili kufikisha mwisho jinamizi la vita.

Akizungumza na waandishi habari mjini New York, Guterres amesema operesheni ya ardhini ya jeshi la Israel na mashambulizi ya mabomu yanayoendelea yanawaathiri raia, hospitali, kambi za wakimbizi, misikiti, makanisa na vifaa vya umoja wa Mataifa yakiwemo makazi. Guterres amesema wakati huo huo Hamas na wanamgambo wengine wanawatumia raia kama ngao ya binadamu kujilinda na wanaendelea kuvurumisha maroketi kiholela kuelekea Israel.

Kwa huzuni Guterres amesema malori kiasi 400 ya mahitaji ya misaada yamefanikiwa kuingia Ukanda wa Gaza katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Kabla vita kuanza malori kiasi 500 yalikuwa yakiingia Gaza kila siku.Guterres ameongeza kusema mafuta yanayohitajika kwa dharura na ambayo ni muhimu kuendeshea shughuli katika hospitali, hayakuweza kusafirishwa kufika Gaza, akiitaja Gaza kama kaburi kwa watoto.

Marekani yakiri maalfu wamekufa Gaza

Marekani imekiri kumetokea vifo vya maalfu ya raia katika Ukanda wa Gaza, ingawa haikutoa takwimu halisi. Ni baada ya rais Joe BIden wa Marekani kuhoji awali juu ya uhalali wa takwimu zinazochapishwa na wizara ya afya ya Gaza. Kufuatia kauli za Biden, maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema takwimu za wizara ya afya ya Gaza zimedhihirisha kwa ujumla ni za kuaminika katika mizozo iliyopita.

Palästina Israelische Streitkräfte werfen Leuchtraketen über Gaza-Stadt ab
Hali ilivyokuwa mjini Gaza usiku wa Novemba 6, 2023Picha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, Brigedia Jeneali, Pat Ryder, amesema kuhusiana na idadi ya raia waliouliwa Gaza, tunafahamu takwimu zimefikia maelfu. Aliwaambia waandishi habari alipoulizwa kuhusu tangazo la wizara ya afya ya Gaza kwamba idadi ya vifo imefikia 10,000.

Ryder pia amesema hii ndio sababu kwa nini kimekuwa kipengee cha kusisitizwa na Israel na mataifa mengine katika eneo hilo kuhusu jinsi ilivyo muhimu kuruhusu msaada wa kibinadamu na misaada mingine kuepelekwa Gaza.

Wakati haya yakiarifiwa, kundi la Hamas limevurumisha maroketi kuelekea Israel kutokea Lebanon. Tawi la kijeshi la Hamas, Al-Qassam birgades, limesema hapo jana katika taarifa yake kwamba limefyetua maroketi 16. Mji wa Nahariyya na Haifa kuisni imeshambuliwa huku Hamas ikisema katika mtandao wa Telegram kwamba mashambulizi hayo yalifanywa kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wao katika Ukanda wa Gaza.

Likijibu kauli hiyo, jeshi la Israel limedai maroketi 30 yalifyetuliwa kuelekea kaskazini mwa Israel na kusababisha ving'ora vya tahadhari ya mashambulizi ya angani kulia katika vijiji kadhaa. Kundi la Hamas lina wapiganaji kadhaa kusini mwa Lebanon na limewahi kudai kufanya mashambulizi nchini Israel kutokea huko.

(dpa,reuters)