1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yarejesha ndege za Boeing 737 MAX

Lilian Mtono
1 Februari 2022

Shirika la ndege la Ethiopia leo limeanza kuzitumia tena ndege zake aina ya Boeing chapa 737 MAX kiasi miaka mitatu tangu watu 157 walipokufa katika ajali mbaya iliyohusisha aina hiyo ya ndege.

https://p.dw.com/p/46Nix
Äthiopien Seattle Boeing Field King County International Airport | Ethiopian Airlines Being 737 Max
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Fiedler

Kupitia taarifa iliyotolewa leo, shirika hilo la ndege limesema uamuzi wa kuanza kutumia tena ndege chapa737 MAX umechukuliwa baada ya ukaguzi wa kina uliofanywa na wasimamizi wa usafiri wa anga nchini Marekani, Umoja wa Ulaya, China na Ethiopia kwenyewe.

Katika safari ya kwanza ndege ya shirika hilo iliruka kwenye anga ya Ethiopia kwa muda saa nne ikiwa imewabeba wawakilishi wa shirika, wale kutoka kampuni ya Boeing na balozi wa Marekani nchini Ethiopia.

Soma Zaidi:Rubani wa ndege ya Ethiopia iliyoanguka alifuata maelekezo: Ripoti 

Ajali ya mwezi Machi mwaka 2019 iliyohusisha ndege ya Ethiopia chapa 737 MAX ilisababisha mataifa duniani kusitisha matumizi ya aina hiyo ya ndege baada ya taharuki kwamba huenda mifumo yake ya kiufundi  ilikuwa na hitilafu.

Äthiopien Flugzeugabsturz Ethiopian Airlines Flight ET 302
Mabaki ya ndege iliyoanguka nchini Ethiopia. Ajali hii inatajwa kuwa ilikuwa ni janga kubwa nchini humo Picha: Reuters/T. Negeri

Kwenye taarifa kwa shirika la habari la AFP wiki hii, shirika hilo la ndege lilisema uamuzi wa kurejesha safari za ndege hizo za 737 MAX baada ya uthibitisho wa kina kutoka kwa wasimamizi nchini Marekani, Umoja wa Ulaya, China na Ethiopia kwenyewe. Aidha lilitoa pia orodha ya mashirika mwengine 35 ambayo pia yameanza kuzitumia tena ndege hizo.

Safari ya Jumanne hii, awali ilipangwa kuelekea Kilimanjaro nchini Tanzania, lakini hali mbaya ya hewa ilisababisha kubadilisha safari hiyo. Ndege hiyo ilipita karibu na Mlima Zuqualla, kuelekea Milima ya Bale kabla ya kurejea Addis Ababa.

Lakini kwa wale waliopoteza wapendwa wao miaka mitatu iliyopita kwenye ajali hiyo hata hivyo wamesema siku hii si ya furaha kwao. Familia za wahanga wa ndege 302 iliyoanguka, katika ajali mbaya kabisa kutokea nchini Ethiopia walitokea katika mataifa zaidi ya 30, lakini wengi wao walikuwa ni raia wa Kenya.

Rais wa familia hizo zawahanga hao Virginie Fricaudet alisema kurejeshwa kwa safari hizo kutarejesha maumivu makubwa kwake. Fricaudet, alipoteza kaka yake kwenye ajali hiyo.

Mashirika: AFPE