1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duda awashukuru Watanzania kuwapokea wakimbizi wa Poland

Mohammed Khelef
9 Februari 2024

Rais Andrzej Duda wa Poland aliye ziarani Tanzania amewashukuru watu wa taifa hilo la Afrika Mashariki kwa kuwapokea wakimbizi wa nchi yake zaidi ya miaka 70 iliyopita.

https://p.dw.com/p/4cEaZ
Rais Andrzej Duda wa Poland.
Rais Andrzej Duda wa Poland.Picha: Czarek Sokolowski/dpa/picture alliance

Rais Duda, ambaye amefanya ziara yake ya kwanza nchini Tanzania tangu kuanza kwa ushirikiano wa miaka zaidi ya 60 kati ya nchi hizo mbili, amesema msingi wa uhusiano thabiti baina ya nchi yake na Tanzania umejengwa na namna watu wa taifa hilo walivyowapokea wakimbizi 5,000 kutoka Poland wakati wa Vita Vikuu ya Pili vya Dunia.

"Napenda nishukuru zaidi watu wa Tanzania na hasa kule Arusha na Tengeru na hii ni moja ya misingi mikubwa iliyojenga urafiki mpaka siku hii ya leo kati ya nchi ya Poland na Tanzania," alisema Rais Duda wakati akizungumza katika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, alikopokelewa na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu.

Soma zaidi: Chama cha CCM chatimiza miaka 47 tangu kuasisiwa Tanzania

“Namna raia hao wa Poland walivyopokelewa na wakaishi hapa, ndiyo msingi wa mahusiano yetu. Wakimbizi wengi walikuwa wanawake na watoto.” 

Kati ya mwaka 1942 na 1944 wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, takribani wakimbizi 18,000 raia wa Poland waliwasili Mombasa, Kenya na kisha baadhi yao wakapelekwa Tanzania.

Wakiwa Tanzania, wakimbizi hao walipelekwa kwenye kambi za Ifunda, Kigoma, Kondoa, Morogoro na wengine Tengeru, Arusha. 

Ushirikiano kupitia miradi ya maendeleo

Kwenye ziara hiyo ya kwanza nchini Tanzania, rais huyo wa Poland alisema analenga kuimarisha ushirikiano kupitia miradi ya maendeleo kwenye sekta za teknolojia ya habari na mawasiliano, kilimo, kodi, sekta ya uzalishaji, utalii, elimu, afya na usafirishaji. 

Marais hao wawili  kadhalika wamezungumzia maeneo mengine ya uwekezaji ikiwamo sekta ya utalii, ambapo wanahabari wameelezwa kuwa takriban watalii 6,000  kutoka Poland walifika nchini katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. 

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.Picha: Presidential Press Service Tanzania

Idadi hiyo ndiyo inayofanya Poland kuwa miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kuitembelea Tanzania na hivyo ili kuongeza ushirikiano huo, Rais Samia Suluhu alisema wamekubaliana kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Poland na Tanzania.

Soma zaidi: Rais Samia ataja mafanikio ya 2023, aainisha mipango ya 2024

"Sasa ili kuchochea zaidi utalii pamoja na biashara, tumewaelekeza wataalamu wetu kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza kwasafari za ndege moja kwa  moja kutoka Poland kuja Tanzania." Alisema rais huyo wa Tanzania akiongeza kwamba kwa kuwa masuala ya biashara kati yao bado ni madogo, basi wanapaswa kukuza biashara kati yao

Rais huyo wa Tanzania alibainisha pia kuwa amealikwa na Rais Duda kutembelea Poland, mwaliko ambao ameupokea.

Katika ziara yake hii ya siku mbili, Rais Duda alitarajiwa kutembelea mradi wa matibabu ya dharura katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao serikali ya Poland imetoa msaada wa dola za Kimarekani milioni 1.136  kwa ajili ya kusaidia sekta ya matibabu na elimu kwa wahudumu wa afya.

Vile vile, rais huyo wa Poland atakwenda kutembelea makaburi ya wakimbizi wa Poland.

Imetayarishwa na Florence Majani/DW Dar es Salaam