1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pasaka yagubikwa na siasa nchini Ukraine

20 Aprili 2014

Sherehe za Pasaka nchini Ukraine zimegubikwa na malumbano ya kisiasa baina ya viongozi wa kanisa la Othodoksi nchini Urusi na Ukraine, huku serikali Mjini Kiev ikiahirisha operesheni za kijeshi dhidi ya wanaharakati.

https://p.dw.com/p/1BlEK
Mwanaharakati mashariki mwa Ukraine akishika doria.
Mwanaharakati mashariki mwa Ukraine akishika doria.Picha: Reuters

Katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev, Askofu Mkuu Filaret amewahutubia waumini katika kanisa lililo karibu na uwanja wa Maidan ambao ni maarufu kwa maandamano ya wanaharakati wa mageuzi, akiita Urusi adui ambaye mashambulizi yake dhidi ya Ukraine yatashindwa. Askofu Mkuu huyo alisema mashambulizi ya Urusi ya kishetani na yanakwenda kinyume na matakwa ya Mungu.

Kwa Upande mwingine, Askofu Mkuu wa Kanisa la Othodoksi la Urusi, Kirill amesoma sala kwa ajili ya Ukraine ambamo amemuomba Mungu kuwawekea kikomo wale aliosema 'wamepania kuiharibu Urusi takatifu'. Askofu Mkuu Kirill amesema ingawa Ukraine imetengwa na Urusi kisiasa, watu wa nchi hiyo na wa Urusi ni ndugu kiroho na kihistoria. Katika sala yake Kirill aliendelea kuiombea Ukraine kupata uongozi 'halali uliochaguliwa na wananchi'.

Waumini walioshiriki katika ibada ya mjini Kiev, wameelezea matumaini kwamba ingawa kwa sasa upo mgawanyiko kati ya magharibi na mashariki, Pasaka ingeiunganisha nchi.

Waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga wanazidi kujichimbia .
Waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga wanazidi kujichimbia.Picha: Reuters

'Wanaharamu' kushughulikiwa kisheria

Kwingineko katika mzozo wa Ukraine, waziri Mkuu wa mpito wa nchi hiyo Arseniy Yatsenyuk amefanya mahojiano na kituo cha televisheni cha NBC cha huko Marekani, na kuwaita 'wanaharamu' watu ambao wanadaiwa kueneza vikabrasha vinavyowataka wayahudi mashariki mwa Ukraine kujiorodhesha ili wafukuzwe. Yatsenyuk amesema watu hao watafikishwa mbele ya sheria. Katika mahojiano hayo Yatsenyuk pia alimshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kuwa na ndoto ya kurejesha Muungano wa Kisovieti.

Na wakati huo huo, Marekani imeazimia kutumia jeshi lake kuiwekea Urusi shinikizo ili itumie ushawishi wake kumaliza mvutano nchini Ukraine kwa kuwanyang'anya silaha wanaharakati wa mashariki mwa nchi hiyo. Gazeti la The Washington Post limeripoti kuwa Marekani ilikuwa ikikaribia kuwatuma wanajeshi wake nchini Poland na pengine katika mataifa ya kanda ya Baltiki, kuimarisha mkono wa umoja wa kujihami wa NATO mashariki mwa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Mpito wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk
Waziri Mkuu wa Mpito wa Ukraine Arseniy YatsenyukPicha: picture-alliance/AP Photo

Marekani kutuma vikosi Polland

Waziri wa ulinzi wa Poland Tomasz Siemoniak amenukuliwa akisema nchi yake iko tayari kuiongoza operesheni hiyo ambayo inaandaliwa huku ikiaminika kwamba Urusi imerundika vikosi vyake karibu na mpaka kati yake na Ukraine. Marekani imeonya kwamba Ukraine ilikuwa ikipita katika kipindi kigumu kutokana na hatua ya wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa nchi hiyo kukataa kuyatambua maazimio ya mkutano wa Geneva ambao Alhamisi iliyopita ulizileta pamoja Ukraine, Urusi, Marekani na Umoja wa Ulaya.

Serikali ya mjini Kiev ambayo inaegemea upande wa nchi za magharibi imesema itasitisha operesheni za kijeshi dhidi ya wanaharakati wanaotaka kujitenga kwa sehemu ya mashariki ya nchi hiyo, hadi kesho Jumatatu ambayo ni mwisho wa sherehe za Pasaka nchini Ukraine.

Serikali ya Kiev, Marekani na Umoja wa Ulaya wanashuku kuwa Urusi inao mkono katika uasi mashariki mwa Ukraine, na kwamba imetuma vikosi vyake maalumu nchini humo. Mara zote Urusi imezikanusha shutuma hizo, lakini imetangaza kuwepo kwa vikosi vyake jirani na Ukraine, pengine kama onyo kwamba hali inaweza kudhoofika zaidi, ikiwa Marekani itaamua kuiwekea vikwazo zaidi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri:Caro Robi