1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhamisho wa wachezaji umegharimu mabilioni

1 Septemba 2014

Soko la usajili limekamilika na uhamisho unaozungumziwa na wengi ni uliofanywa na Manchester United kumleta Radamel Falcao Old Trafford.

https://p.dw.com/p/1D4yw
Radamel Falcao
Picha: picture-alliance/dpa

Takwimu zinaonyesha kuwa biashara ya wachezaji wapya iliyofanywa katika kipindi hiki cha uhamisho imeweka rekodi mpya barani Ulaya. Mcolombia Falcao anajiunga na Man Utd kwa mkataba wa msimu mmoja kwa mkopo akitokea Monaco ya UFARANSA na kufikisha pauni milioni 150 kiasi cha fedha zilizotumika katika usajili wa wachezaji wapya tangu Juni 6.

Timu kutoka ligi kuu za England, Uhispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa zimetumia zaidi ya dola bilioni 2.1 wakati wa kipindi cha uhamisho na kiasi hicho kitaongezeka ifikapo muda wa mwisho kufanya biashara.

Bundesliga Borussia Dortmund VfB Stuttgart
Shinji Kagawa anarejea BVB baada ya miaka miwili ya masaibu katika klabu ya Manchester UnitedPicha: Reuters

Man Utd ndio waliotumia kiasi kikubwa cha fedha, mbele ya Real Madrid wa Uhispania. Man Utd wamemsajili Daley Blind kutoka Ajax AMSTERDAM na pia wamempata Angel Di Maria kutoka Real Madrid kwa kiasi cha pauni milioni 59, Ander Herrera wa Uhispania na beki wa Uingereza Luke Shaw pamoja na Muargentina mwingine Marcos Rojo.

Kuongeza na biashara waliofanya United, pia wametumia kiasi cha dola milioni 190 (hasa kwa ununuzi wa Mario Balotelli, Adam Lallana na Dejan Lovren). Chelsea imetumia zaidi ya dola milioni 125 (ikiwa ni pamoja na ununuzi wa Cesc Fabregas na Diego Costa) nayo Arsenal zaidi ya milioni 103.

Vilabu vya Uingereza vimetumia karibu dola milioni 300 kwa kuwasajili wachezaji wa Uhispania. Real Madrid na Barcelona pia vimewauza baadhi ya wachezaji wao na kuwanunua wengine. Barcelona iliilipa Liverpool zaidi ya dola milioni 125 kuipata saini ya Luis Suarez, wakati Real Madrid ikitumia dola milioni 108 kumpata James Rodriguez kutoka Monacho na zaidi ya dola milioni 35 kumnyakua mshindi wa Kombe la Dunia kiungo Mjerumani Toni Kroos.

Soko la ununuzi wa wachezaji limepungua kwa kiasi kikubwa nchini Italia na Ufaransa, ambako uchumi unaoyumba na masharti ya UEFA kuhusu matumizi ya fedha vimeathiri biashara ya kandanda. Vilabu vikuu nchini Ufaransa Paris St Germain na Monaco vimetumia chini ya asilimia 75% mwaka huu katika kuwanunua wachezaji wapya kuliko ilivyokuwa katika kipindi kama hicho mwaka wa 2013.

Toni Kroos
Toni Kroos alihamia Real Madrid kutoka Bayern MunichPicha: picture-alliance/dpa

Matumizi ya vilabu vya Italia yalikaribia dola milioni 200. AC Milan wamemsajili Fernando Torres na Marco Van Ginkel wote kutoka Chelsea kwa mkataba wa mkopo. Na kuhusiana na suala hilo la biashara ya uhamisho wa wachezaji, bila shaka mojawapo ya vilabu ambavyo mashabiki wake wanatabasamu kwa sasa hapa Ujerumani ni Borussia Dortmund. Hii ni baada ya kumsajili tena kiungo nyota Mjapan Shinji Kagawa kutoka Manchester United. Kagawa amesaini mkataba wa miaka minne.

Kagawa mwenye umri wa miaka 25 alipendwa saan na mashabiki wa Dortmund ambayo aliichezea kuanzia mwaka wa 2010 hadi 2012 na kushinda Bundelsiga mwaka wa 2011 na kombe la SHirikisho la Soka Ujerumani – DFB mara mbili. Alifunga magoli 21 katika mechi 49 za Bundesliga.

Kwingineko aliyekuwa mshambuliaji wa Chelsea Salomon Kalou amejiunga na Hertha Berlin kwa mkataba wa miaka mitatu. Kalou raia wa Cote d'Ivoire mwenye umri wa miaka 29 amewasili Berlin akitokea katika klabu ya Ufaransa Lille na anachukua nafasi ya Mcolombia Adrian Ramos aliyejiunga na Borussia Dortmund. Kalou ni mchezaji wa nane kusajiliwa na Hertha msimu huu.

Mwisho wa michezo kwa sasa, umekuwa nami Bruce Amani. Kwaheri kwa sasa.

Mwandishi; Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Saumu