1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZambia

Yellen azuru Zambia kujadilia madeni ya China, afya ya umma

Bruce Amani
23 Januari 2023

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen yuko nchini Zambia katika kituo cha pili cha ziara yake barani Afrika inayonuwiwa kukuza uwekezaji wa Marekani na uhusiano.

https://p.dw.com/p/4MaqS
Washington | US-Finanzministerin Janet Yellen
Picha: JIM WATSON/AFP/Getty Images

Suala la deni linatazamiwa kuwa mada katika mazungumzo wakati Yellen atakapokutana na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema na Waziri wa Fedha wa Zambia, Situmbeko Musokotwane ili kuishinikiza China kuendelea kujadiliana kuhusu madeni iliyotoa kwa taifa hilo la Afrika. 

Yellen yuko katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka ambao unadhihirika wazi kuhodhiwa na uwekezaji wa China.

Waziri huyo wa fedha wa Marekani pia atazuru viwanda vya utengenezaji wa dawa vinavyonufaika na uwekezaji wa Marekani ili kuonyesha kile anachokiona kama ruwaza ya mafanikio.

Yellen aliliambia shirika la habari la Associated Press siku ya Jumamosi, kwamba mataifa mengi ya Afrika yanazongwa na mzigo mkubwa wa madeni, mengi yakihusiana na uwekezaji wa China barani humo. Hata hivyo, waziri huyo amesisitiza kuwa ziara yake haihusu ushindani na China.

Yellen yuko katika ziara ya siku 10 barani Afrika iliyoanzia Senegal, ambako alikitembelea kilichokuwa kituo cha biashara ya utumwa. Anatarajiwa pia kuizuru Afrika Kusini.