1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi aupigia debe mradi wa ujenzi wa miundombinu

Josephat Charo
26 Aprili 2019

Rais wa China Xi Jinping leo amejaribu kuondoa wasiwasi kuhusu mradi wake wa ujenzi wa barabara na miundombinu, akisema mradi wake huo wa kimataifa hautaruhusu kabisa rushwa, huku akiahidi kuepusha athari za madeni.

https://p.dw.com/p/3HUIz
Peking Belt and Road Forum for International Cooperation; Xi Jinping; Wladimir Putin
Picha: picture-alliance/dpa/V. Sharifulin

Rais wa China Xi Jinping ametoa kauli ya kufurahisha kwa Marekani kuhusu ruzuku, sarafu ya yuan na biashara wakati nchi hizo mbili zikijiandaa kufanya mazungumzo mapya muhimu wiki ijayo. Sera ya kigeni ya Xi inalenga kuuimarisha mradi wa ujenzi wa barabara na miundombinu kuliunganisha bara la Asia na Ulaya na Afrika kupitia uwekezaji mkubwa katika miradi ya usafiri wa baharini, barabara na reli wa mabilioni ya dola kutoka kwa mabenki ya China.

Mradi huo unatoa fursa ya kuleta miundombinu ya kisasa kwa mataifa yanayoendelea, lakini wakosoaji wanasema unagubikwa na mikataba yenye vipengee vya siri inayozipendelea kampuni za China, wakati huo huo ikizikaba koo nchi na madeni makubwa na uchafuzi wa magzingira. Xi amesema kila kitu lazima kifanyike kwa uwazi na ameahidi China itatekeleza sheria mpya ya uwekezaji wa kigeni inayolenga kulinda haki miliki ya mali za makampuni ya kigeni.

"China itafanya kila jitihada kujenga mazingira mazuri ya biashara yanayoheshimu thamani ya ujuzi, kuboresha mfumo wa sheria za kulinda mali, kuimarisha sheria zinazosimamia utekelezaji na pia kuimarisha haki ya wamiliki wa mali na kukomesha uhamishaji wa teknolojia kwa kutumia nguvu."

Guterres aipongeza China

Akizungumza katika mkutano huo wa Beijing uliowaleta pamoja wakuu 37 wa serikali, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema mradi wa China unatoa fursa kusaidia kubadili mkondo wa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

"Na nataka kuitambua China kwa jukumu lake kubwa kama nguzo ya ushirikiano wa kimataifa. Mkutano huu unadhihirisha ari hiyo ya kujitolea kwa dhati wakati ulimwengu ukipitia kipindi kigumu. Lakini wakati tunapokabiliwa na changamoto nyingi, tunaona pia ishara za matumaini. Uongozi wa China katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi unasaidia kuonyesha njia."

Hata hivyo Guterres ameonya kwamba uwekezaji katika miradi ya China lazima uwe endelevu.

China Imran Khan beim Second Belt and Road Forum
Waziri Mkuu wa India, Imran KhanPicha: Pakistan Prime Minister Press Office

Akizungumzia pia katika mkutano huo wa Beijing leo rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema ni muhimu kuunda mkakati madhubuti utakaoshughulikia kitisho cha kuvurugika siasa za kimataifa, uchumi na teknolojia. Ameonya dhidi ya mataifa kujihami na kujilinda kibiashara na kutumia mbinu za kutoheshimu mamlaka ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katika kupitisha maamuzi na hata mbaya zaidi kujiingiza katika vita vya kibiashara. 

Waziri Mkuu wa India, Imran Khan, ambaye nchi yake inauunga mkono mradi wa China wa ujenzi wa miundombinu, ametoa wito kuundwe afisi maalumu ya ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa.

Kwa mujibu wa maafisa wa China tangu rais Xi aipouzindua mradi wa ujenzi wa barabara na miundombinu mwaka 2013, China imewekeza dola bilioni 90 katika miradi mbalimbali huku mabenki yakitoa mikopo ya thamani ya dola bilioni 300.

afpe, ap