1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UK: Mahakama yasema si sheria kuwapeleka wahamiaji Rwanda.

Zainab Aziz
29 Juni 2023

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema serikali yake itakata rufaa kwenye Mahakama ya Juu kabisa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa iliyobatilisha mpango wake wa kuwapeleka wahamijai nchini Rwanda.

https://p.dw.com/p/4TEkz
Großbritannien | Rishi Sunak
Picha: Kin Cheung/REUTERS

Waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema anaiheshimu mahakama lakini kimsingi hakubaliani na maamuzi ya mahakama hiyo. Rishi Sunak amesisitiza kwamba Rwanda ni nchi salama. Mahakama ya Uingereza leo Alhamisi iliamua kuwa mpango huo wa serikali wa kuwapeleka Rwanda watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza ni kinyume cha sheria. Uamnuzi huo wa mahakama ni pigo kwa serikali ya kihafidhina ambayo ilitoa ahadi hiyo kwa lengo la kuwazuia wahamiaji wanaofanya safari za hatari kuingia nchini Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Leon Neal/Getty Images

Katika uamuzi wa mgawanyiko wa majaji wawili kwa mmoja wa Mahakama ya Rufaa wamesema Rwanda haiwezi kuchukuliwa kama nchi ya tatu salama ambayo wahamiaji wanaweza kupelekwa.

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana, serikali ya Uingereza ilipanga kuwapeleka maelfu ya waomba hifadhi wanaofika katika ufuo wake ambao upo zaidi ya umbali wa kilomita 6,400 kutoka taifa la Afrika Mashariki la Rwanda.

Safari ya kwanza ya kuwasafirisha watu hao kwa ndege ilizuiwa mwakauliopita katika uamuzi wa dakika za mwisho wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR), ambayo iliweka amri ya kukataza kufanyika kwa zoezi lolote kama hilo hadi zitakapomilika hatua za kisheria nchini Uingereza.

Jaji Mkuu Lord Burnett.
Jaji Mkuu Lord Burnett.Picha: Cameras in Court/empics/picture alliance

Mnamo mwezi Desemba mwaka jana, Mahakama Kuu iliamua kuwa sera hiyo ilikuwa halali, lakini uamuzi huo ulipingwa na mashirika ya haki za binadamu pamoja na watu wanaoomba hifadhi kutoka nchi kadhaa.

Uamuzi wa leo unahusu malalamiko yaliyofikishwa mahakamani na wahamiaji 10 na shirika la hisani linalowasaidia wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza. Uamuzi huo wa mahakama ya rufaa ya Uingereza umepokelewa kwa furaha na mashirika ya kutetea haki za binadamu lakini umepokelewa kwa mtazamo tofauti nchini Rwanda. 

Kushoto: Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak. Kulia: Waziri wa Mambo ya Ndani Suella Braverman.
Kushoto: Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak. Kulia: Waziri wa Mambo ya Ndani Suella Braverman.Picha: Phil Noble/empics/picture alliance

Serikali ya Rwanda imesema inasimama na serikali ya Uingereza katika mpango wake licha ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya nchini humo na imesisitiza kuwa mpango huo umekidhi vigezo vya Umoja wa Mataifa kuhusu kuwahudumia wakimbizi.

Vyanzo:DPA/RTRE/AFP