1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais nchini Misri waanza leo

10 Desemba 2023

Wamisri wameanza kupiga kura Jumapili10.12.2023 katika uchaguzi wa Rais uliogubikwa na mzozo wa Ukanda wa Gaza mdororo wa uchumi nchini humo.

https://p.dw.com/p/4ZzCu
Uchaguzi wa rais, Misri
Wananchi wa Misri waliojitokeza kupiga kuraPicha: Amr Nabil/AP/picture alliance

Uchaguzi huo unafanyika kwa siku tatu ambapo utakamilika Jumanne. Kwenye kinyang'anyiro hicho, Rais anayetetea kiti chake Abdel-Fattah Al Sissi anatarajiwa kushinda muhula wa tatu madarakani. Al Sissi,ambaye ameitawala Misri tangu mwaka 2014 alipiga kura katika kituo cha Heliopolis mashariki mwa mji mkuu Cairo.

Licha ya mfumuko mkubwa wa bei nchini humo, al-Sissi amepata uungwaji mkono mkubwa wakati Wamisri wengi wakikubaliana na tahadhari aliyoitoa akihofia kuwa wakaazi wa Gaza wanaweza kulazimika kuhamia Misri huku mashambulizi ya Israel yakiendelea.

Soma zaidi: Je, uchaguzi wa rais Misri utaleta mabadiliko yoyote?

Tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas Oktoba 7, al-Sissi pia ametahadharisha kuwa kuwahamishia Wapalestina Misri kutaigeuza rasi ya Sinai kuwa eneo la kuendeshea mashambulizi dhidi ya Israel.

Vituo kadhaa vya kupigia kura katika mji mkuu Cairo, vilipambwa kwa rangi za bendera ya taifa hilo huku nyimbo za kizalendo zikipigwa. Vyombo vya Habari vinavyoiunga mkono serikali viliwaonesha watu wakiwa nje ya vituo vya kupigia kura katika maeneo kadhaa nchini humo.

Kando ya al- sisi wagombea wengine watatu wanawania nafasi ya kuiongoza Misri. Wapinzani hao wa rais wa Misri kwenye uchaguzi huoni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto, Farid Zahran anayekiongoza chama cha Social Democratic Party; Abdel-Sanad ambaye ni kiongozi wa chama cha liberal Wafd party na mwanzilishi wa  chama cha kiliberali cha People's Republican Party.

Watu walifuatilia mikutano yake na waandishi wa Habari alipokuwa sambamba na viongozi kutoka mataifa ya kigeni wakati mashambulizi kati ya Israel na Hamas kwenye Ukanda wa Gaza karibu na mpaka wa Misri wa kaskazini mashariki, ulipochukua nafasi kubwa na hivyo kusahauliwa kwa matatizo ya ndani likiwemo tatizo la ukosefu wa uhuru wa kujieleza.

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi
Rais wa Misri anayetetea kiti chake Abdel Fattah el-SissiPicha: Vladimir Smirnov/dpa/TASS/picture alliance

Wafuasi waaminifu wa al-sisi wanamuona kuwa mtu sahihi anayeweza kuhakikisha utulivu katika nchi hiyo wakati kanda hiyo ikiwa kwenye mtikisiko.

Mabango makubwa yenye picha ya rais huyo anayetetea kiti chake yanaonekana katika mji wote wa Cairo hali inayowafifisha wagombea wengine.

Vituo vya kura kore nchini Misri vilifunguliwa mapema Jumapili kati ya saa tatu asubuhi. Vinatarajiwa kufanya kazi kwa saa 12. Kulingana na vyombo vya Habari vya ndani ya taifa hilo, Wamisri wasiopungua milioni 67, wanakidhi vigezo vya kushiriki katika kura hiyo.

Matokeo rasmi ya uchaguzi kutolewa Desemba 18

Matokeo rasmi ya mwisho ya uchaguzi huo war ais yanatazamiwa kutolewa tarehe 18, Desemba. Itakumbukwa kuwa Al-Sissi alichaguliwa kwa mara nyingine mwaka 2018 ambapo alipata ushindi wa kishindo.

Hata hivyo Mamlaka zinahofia kuwa kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura kunaweza kudhoofisha uhalali wake katika muhula ujao wa miaka sita. Mnamo mwaka 2018, wapiga kura walijitokeza kwa asilimia 40% wakati mwaka 2014 asilimia 47% ya watu nchini humo walipiga kura.

Uchaguzi wa Misri
Mgombea wa Urais wa Misri wa chama cha Wafd, Abdel-Sanad akipiga kuraPicha: Amr Nabil/AP/picture alliance

Katika wiki za hivi karibuni, serikali imekuwa ikijaribu kuwashawishi raia kupiga kura ikitumia njia ya televisheni, matangazo, vipindi vya mazungumzo na matangazo ya kizalendo.

Mwaka 2013 jeshi lililoongozwa na al-Sisi liliuangusha utawala wa rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia Mohammed Morsi. Morsi alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo baada ya ghasia za mwaka 2011.

Chini ya utawala wa Sissi, maelfu ya wanaharakati na Wafuasi wa dini ya Kiislamu wamefungwa jela au kulazimika kuishi uhamishoni na vyombo vvya Habari vimekuwa vikidhibitiwa kwa kiasi kikubwa na wafuasi waaminifu wa kiongozi huyo. Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya nchi hiyo imewakamata wapinzani kadhaa wa serikali.