1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Waasi wa Kihouthi wajizolea umaarufu

2 Mei 2024

Wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran wameanza kupanua mamlaka yake ndani ya Yemen na katika kanda nzima Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4fOuT
Yemen | Waasi wa Kihouthi waandamana mjini Sanaa dhidi ya Marekani na Israel
Mwanajeshi wa wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran akishiriki maandamano dhidi ya Marekani na Israel na mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya Marekani na Wahouthi kufuatia operesheni kadhaa za Wapalestina katika Bahari ya Shamu. Picha: Osamah Yahya/dpa/picture alliance

Hata hivyo, sera zake ziko mbali na utawala bora zikizidisha hali ya mbaya ya kibinadamu na mzozo wa kiuchumi nchini Yemen wakati ikiendeleza mashambulizi katika Bahari ya Shamu. 

Soma pia: Waasi wa Houthi wasema wanalenga meli za Magharibi katika bahari ya Shamu

Baada ya utulivu wa mashambulizi kwa takriban wiki mbili, wanamgambo wa Houthi nchini Yemen wameanza tena mashambulizi ya makombora yaliyolenga meli zenye uhusiano na Israel, Marekani au mataifa yanayounga mkono muungano wa kimataifa wa kupambana na Houthi kwenye Bahari ya Shamu.

Mashambulizi hayo, ambayo Wahouthi wamekuwa wakifanya tangu Novemba 2023, ni dhamira yao kubwa ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina huko Gaza.

Hata hivyo, kundi hilo linaloungwa mkono na Iran halijaweza kushawishi mwenendo wa vita kati ya Israel na Hamas, badala yake mashambulizi yanayoendelea yameongeza umaarufu wa kundi hilo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Mpasuko unazidisha mateso Yemen

Sanaa | Msemaji wa wanamgambo wa Kihouthi Yahya Sareya
Yahya Sareya msemaji wa wanamgambo wa Kihouthi akitoa taarifa mjini SanaaPicha: IMAGO/Xinhua

Yemen bado imegawanyika tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2014, wakati Wahouthi walipopindua serikali ya Yemen. Na tangu wakati huo Wahouthi wamechukua udhibiti kaskazini na magharibi, na mji mkuu wake Sanaa huku maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Baraza la Rais linalotambuliwa kimataifa la Yemen, mji mkuu wake uko Aden.

Soma pia: Houthi imeongeza mashambulizi kwenye Bahari ya Shamu tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas

Mwaka mmoja baadaye, mzozo huo uliongezeka zaidi wakati muungano wa kimataifa unaoongozwa na Saudi Arabia ulipokuja kusaidia serikali inayotambulika kimataifa.

Vita katika taifa hilo vimesababisha mauwaji ya maelfu ya watu na kusababisha moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Kufuatia makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa kati ya serikali hizo mbili zinazohasimiana mnamo Aprili 2022, umaarufu wa Wahouthi ulipungua, "kwa sababu ya usimamizi wao mbaya, ufisadi, ukandamizaji na ukweli kwamba uchumi ulikuwa mbaya," Hisham Al-Omeisy, mchambuzi wa migogoro na mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Rasilimali za Habari cha Yemen katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, aliiambia DW.

Lakini sasa, baada ya miezi mitano ya kushambulia meli za mizigo katika Bahari ya Shamu katika kuunga mkono Wapalestina, "Wahouthi kimsingi wanajikita katika umaarufu ambao wameupata ndani na kikanda, wakijishaua kama nguzo ya mataifa ya Kiislamu na Kiarabu," Al-Omeisy aliongeza.

Aidha Omeisy aliongeza kuwa  "Wanatumia umaarufu huo kupanua udhibiti wao, lakini pia kuimarisha utawala wao ndani ya maeneo ya Yemeni ambapo wameanzisha harakati kubwa ya kusajili wafuasi wapya chini ya kivuli cha kuunga mkono Gaza."

Hakuna utawala bora kwa Wayemen

Yemen Taiz
Vikosi vya usalama vya Yemen vikiwa katika ulinzi wakati wa mechi ya fainali ya Ligi ya mjini Taiz kati ya Al Ssumud na Al Easifa kwenye uwanja wa mpira wa Kidre katika eneo la Qadas la Taiz, Yemen.Picha: Abdulnasser Alseddik/AA/picture alliance

Kuongezeka kwa umaarufu wa wanamgambo wa Kihouthi hakujatafsiriwa kuwa utawala bora katika nchi iliyokumbwa na vita.

Thomas Juneau, mchambuzi wa Mashariki ya Kati na profesa katika Chuo Kikuu cha Ottawa cha Kanada, aliiambia DW, "Jinsi wanavyowatendea Wayemeni chini ya utawala wao inakinzana na ule unaoonekana kuwa wa kibinadamu au wa kimaadili ambao wanadai kuwa unashughulikia suala la Palestina."

Kauli inayokubalika katika mji wa tatu kwa ukubwa nchini Yemen, Taiz, wenye wakazi  940,600.

Taiz imezingirwa kwa takriban miaka minane na wanamgambo wa Kihouthi wanaendelea kuziba barabara kuu zinazoingia katika mji huo unaodhibitiwa na serikali. Maji na bidhaa muhimu zinaendekea kuwa adimu.

"Hatujapata makubaliano yoyote au kuona hatua zozote za kupunguza mateso ya watu huko Taiz tangu Wahouthi waanzishe msaada wao kwa Wapalestina," Fatima, mama wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 20 anayeishi Taiz aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina la pili kwa hofu ya kuadhibiwa, aliiambia DW.

Fedha mpya huzidisha kiwango cha ubadilishaji

Yemen | Sarafu
Sarafu za Yemeni Picha: JANUSZ PIENKOWSKI/Zoonar/picture alliance

Katika siku za usoni, mgawanyiko wa kiuchumi, na kwa upande mwingine, hali ya kibinadamu, inaweza kuzorota zaidi, sio tu katika mji Taiz lakini katika maeneo yote yanayoshikiliwa na serikali.

Mnamo Aprili, Benki Kuu inayoendeshwa na Wahouthi huko Sanaa ilitoa aina mpya ya sarafu ya ndani.

Soma pia: Marekani yawaorodhesha wanamgambo wa Houthi kama kundi la kigaidi tena

Katika taarifa, Benki Kuu inayoongozwa na Houthi ilisema sarafu hizo mpya zitachukua nafasi ya noti za karatasi zilizoharibika za kiima sawa.

Hata hivyo, Benki Kuu inayoshirikiana na serikali huko Aden mara moja ilikashifu sarafu hizo mpya na kuitaka kama "bandia." Wakati hali ya tete ya kiuchumi ikizidi kuongezeka.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Yemen, mjini Aden wiki hii, dola moja ya Marekani iligharimu riyal 1,683 za Yemeni, huku kiwango cha ubadilishaji cha dola 1 kikisalia kuwa riyal 530 za Yemeni katika mji mkuu wa Sanaa unaoshikiliwa na Wahouthi.

Malengo ya Wahouthi hayajabadilika

Ghuba ya Aden | Meli ya mizigo ya Rubymar yazama
Meli ya mizigo ya Rubymar yazama baada ya kushambuliwa katika Bahari ya Shamu.Picha: Khaled Ziad/AFP/Getty Images

Lengo kuu la ndani la Wahouthi ni kuibuka kama mamlaka inayotawala na halali nchini Yemen, kutokana na kile wanachofanya katika Bahari ya Shamu, wanahisi kuwa wako katika nafasi ya kupata makubaliano zaidi kutoka kwa wapinzani wao wa ndani, haswa serikali inayotambuliwa kimataifa, lakini pia kutoka kwa wapinzani wao wa kikanda, haswa Saudi Arabia.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohamed bin Salman amekuwa wazi kuhusu nia yake ya kujiondoa katika vita vya gharama kubwa nchini Yemen lakini mazungumzo yamekwama kutokana na vita vya Gaza.

Soma pia:Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi yaliyouwa watu 70 Yemen 

Hata hivyo, wataalamu wanaamini kwamba mapema au baadaye, kujiondoa katika vita huko Yemen kutakuja kwa gharama ya kukubali wanamgambo wa Kihouthi kama mamlaka kuu ya Yemen, licha ya miaka mingi ya kuiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa.

Hisham Al-Omeisy ana mashaka kuwa serikali ya Yemen inaweza kuzuia mafanikio ya Wahouthi.

"Kwa bahati mbaya, serikali ya Yemen na vuguvugu dhidi ya Houthi hazijaungana ipasavyo katika ujumbe wa kitaifa au mpango wa utekelezaji zaidi ya kuwapinga Wahouthi," alisema. "Kwa kusema ukweli watahitaji kufanya kitendo chao pamoja ili kuwa na msimamo thabiti ambao unaweza kuzuia shauku ya Houthi na matarajio ya upanuzi."