1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa ADF wadaiwa kuwaua raia

Admin.WagnerD16 Januari 2023

Mji mdogo wa Kasindi ulioko kwenye mpaka wa Congo na Uganda ulishambuliwa na kundi la kigaidi kutoka Uganda ADF jana Jumapili. Watu wasiopungua kumi wanadaiwa kuuawa na wengine zaidi ya thelathini kujeruhiwa vibaya.

https://p.dw.com/p/4MFfn
Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Shambulizi hilo la Kasindi linatokea wakati operesheni za pamoja kati ya jeshi la Congo na Uganda zikiendelea katika maeneo ya Beni na Irumu. Wakati huo huo, gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini Jenerali Ndima Constant anatarajiwa kuuzuru mji wa Goma kwa ajili ya kuwapa pole watu walioondokewa na wapendwa wao katika shambulizi hilo. 

Soma Zaidi: Waasi wa ADF wafanya mauaji huko Ituri DRC

Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa jana mjini Kasindi, pale majeruhi wakipelekwa kwenye vituo vya afya, baada ya bomu kuripuka kwenye kanisa la kipentekoste CEPAC Lubiriha Kasindi wakati wa ibada. 

"Walikuwa kwenye ibada hadharani, na ndio ghafla wakasikia mripuko wa bomu. Pembezoni kwa kanisa hilo kuna vioske, mahala pakuuzia bidhaa mbalimbali na kadhalika. Inaonekana kuwa bomu hilo lilitegwa karibu na duka la kuuzia muda wa kuzungumzia kwenye simu. Watu wengi walikuwa wameketi hapo na wengine katika mahema. Kwa kweli watu wengi wamefariki dunia" alisema mmoja ya mashuhuda wa mkasa huo.

DRK Symbolbild FARDC
Wanajeshi wa serikali ya Kongo wakipiga doria katika maeneo ya karibu na mji wa Beni kwa ajili ya kuhakikisha usalama.Picha: Alexis Huguet/Getty Images/AFP

Alipozungumza na wanahabari katika mji wa Beni, msemaji wa jeshi katika sekta ya operesheni Sokola1 Grand Nord, kapteni Anthony Mualushayi alisema, kuwa shambulizi kwenye kanisa CEPAC ni la kigaidi na lilifanywa na waasi wa ADF. Alisema hayo baada ya vyombo vya kijasusi kumkamata mshukiwa mmoja akihusishwa na mkasa huo. 

Soma Zaidi:Zaidi ya watu 50 wauawa na ADF Congo Mashariki

Akasema "Tumejitahidi kabisa na tumefanya kazi kubwa kwani tumeweza kumshika mshukiwa mmoja ambae alichangia katika shambulizi hilo. Na hilo ndio la muhimu kwetu kwani kwa kumsikiliza mshukiwa huyo, tunaelewa kwamba ni tendo la kigaidi lililotekelezwa na magaidi wa ADF-MTM."

Shambulizi hili la kigaidi katika mji mdogo wa Kasindi linatokea wakati operesheni za kijeshi za pamoja kati ya jeshi la Congo na Uganda zikiwa zinaendelea katika wilaya za Beni na Irumu.

Mji huo mdogo wa Kasindi ambao pamoja na mengine una miundombinu finyu na isiyojitosheleza kwa ajili ya kuwahudumia waliojeruhiwa hali inayosababisha changamoto kubwa. 

Msemaji wa jeshi la Congo katika eneo kubwa la mkoa wa Kivu ya Kaskazini Anthony Mualushayi ameiambia idhaa ya Kiswahili ya DW kwamba shambulizi hili la Kasindi kwenye kanisa la CEPAC limetokea wakati majeshi ya muungano yaani UPDF na FARDC yakizidisha mashambulizi kwenye ngome mbalimbali za ADF na kubwa kuliko yote likiwa ni lile la Mughalika Ameongeza kuwa ADF wamewapoteza wapiganaji wao wengi. 

Taaarifa nyingine toka eneo la Kasindi zasema, kuwa gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini Jenerali Ndima Constant atauzuru mji huo, kuomboleza na familia zilizoondokewa na wapendwa wao.