1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Victoire Ingabire azuwiliwa kugombea urais Rwanda

Saleh Mwanamilongo
22 Machi 2024

Nchini Rwanda, kiongozi wa upinzani Victoire Ingabire hatowania kiti cha urais kwenye uchaguzi wa hapo Julai 15 baada ya mahakama ya juu nchini humo kumzuia kugombea.

https://p.dw.com/p/4e0Pl
Ingabire alikaa gerezani kwa miaka minane kabla ya kupata msamaha wa rais mwaka 2018 uliofupisha kifungo chake cha miaka 15
Ingabire alikaa gerezani kwa miaka minane kabla ya kupata msamaha wa rais mwaka 2018 uliofupisha kifungo chake cha miaka 15Picha: Reuters/J. Bizimana

Majaji wa Mahakama ya Juu mjini Kigali walitupilia mbali ombi la Victoire Ingabire la kutaka  kurejeshewa haki yake ya kiraia na hivyo kumzuia kugombea katika uchaguzi wa urais baadae mwaka huu.

Kiongozi huyo wa upinzani ameiambia DW kwamba hata hivyo aliheshimu masharti yote yaliyowekwa baada yeye kuachiliwa huru kwa msamaha wa rais mwaka 2018. Victoire Ingabire amesema uamuzi huu wa mahakama si jambo la kushangaza kwa sababu serikali ya Kigali haitaki upinzani unaoaminika.

''Chama tawala, RPF, hakiko tayari kuwapa nafasi wapinzani, hakiko tayari kushindana na wengine ambao wana sera ambayo Wanyarwanda wanaweza kupata fursa ya kuchagua. Kwa hivyo chama cha RPF hakiko tayari kukubali ushindani. Lakini wakati huo huo, Wanyarwanda wana kiu ya demokrasia, wana kiu ya kuwa na nchi ambayo inaweza kujieleza kwa uhuru.'', alisema Ingabire.

Victoire Ingabire alikamatwa na kutuhumiwa kukana ukweli wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda, baada ya kuomba mnamo mwaka 2010 kwamba wahusika wa uhalifu dhidi ya Wahutu pia wahukumiwe.

Kagame mgombea pekee ?

Rais Kagame aliyeingia madarakani mwaka 2000 baada ya kuchaguliwa na bunge na alichabuliwa kwa asilimia zaidi ya tisini za kura mwaka wa 2003, 2010 na 2017
Rais Kagame aliyeingia madarakani mwaka 2000 baada ya kuchaguliwa na bunge na alichabuliwa kwa asilimia zaidi ya tisini za kura mwaka wa 2003, 2010 na 2017Picha: Halil Sagirkaya/Anadolu/picture alliance

Ingabire sio mpinzani pekee ambaye hatashiriki katika uchaguzi ujao wa urais. Bernard Ntaganda, mgombea urais wa mwaka 2010 kabla yeye pia kutupwa jela, anasema wataishitaki Rwanda kwenye mahakama ya Afrika Mashariki.

"Tangu chama cha RPF kuingia madarakani, hatujafanya uchaguzi wa wazi. Na kama kawaida, Rwanda haijawahi kuwa na uchaguzi wa kuaminika, jumuishi na wa uwazi. Jumuiya ya kimataifa lazima ibadili mwelekeo wake ili kulaani vitendo vya utawala wa Rwanda.'', alisisitiza Ntaganda.

Kwa sasa, Frank Habineza, wa chama cha kijani cha Rwanda (Democratic Green Party of Rwanda), ndiye mgombea pekee aliyetangazwa kushindana na Rais Paul Kagame katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Julai. Kwenye uchaguzi wa 2017 Habineza alipata chini ya asimilia moja.

''Linapokuja suala la demokrasia, Rwanda iko nyuma sana''

Mali Ali mchambuzi wa masuala ya kisiasa kwenye kanda ya Maziwa Makuu amesema ni vigumu kutumainia upinzani wa kuaminika dhidi ya Paul Kagame.

''Dhidi ya Kagame huwezi sema kuna upinzani na demokrasia nchini Rwanda. Ni nchi ambayo iko mikononi mwa mtu ambaye hataki ushindani. Kwa hiyo, linapokuja suala la demokrasia, Rwanda iko nyuma sana ukilinganisha na majirani zake.'', alisema  Mali.

Huku rufaa ya upinzani wa Rwanda ikisubiriwa, Rais Paul Kagame, aliye madarakani tangu 2000, tayari amidhinishwa na chama chake kuwa mgombea wa uchaguzi wa Julai 15 kuwania muhula wa nne.

Chanzo : AFP