1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yachukuwa hatua dhidi ya uchomaji Quran barani Ulaya

Mohammed Khelef
29 Januari 2023

Uturuki imetoa onyo la hadhari ya usalama kwa raia wake wanaoishi au wanaopanga kuyatembelea mataifa ya Ulaya, ikitaja ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu na maandamano ya kupinga utawala wa Ankara.

https://p.dw.com/p/4MqFD
Türkei | Der türkische Präsident Recep Tayyip Erdogan
Picha: Murat Kula/AA/picture alliance

Onyo hilo lililotolewa siku ya Jumapili (Januari 29) linafuatia maandamano ya mwishoni mwa wiki nchini Sweden, baada ya mfuasi mmoja wa siasa kali za mrengo wa kulia kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Qur'an mjini Stockholm na pia maandamano ya kuwaunga mkono Wakurdi dhidi ya serikali ya Uturuki. 

Wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki iliwaomba raia wake kuchukuwa tahadhari na kukaa mbali na maeneo yanakofanyika maandamano hayo. 

Vile vile taarifa ya wizara hiyo iliwataka raia hao kuripoti kwenye vyombo vya usalama kwenye maeneo waliyopo, ikiwa watakabiliwa na mashambulizi yanayotokana na ubaguzi ama chuki dhidi ya wageni.

Uchomaji moto Qur'an wasambaa

Uturuki ilimlaani vikali raia wa Sweden anayefuata siasa kali za mrengo wa kulia, Rasmus Paludan, ambaye aliichoma Qur'an mjini Stockholm na kisha kurejea kitendo kama hicho siku ya Ijumaa mjini Copenhagen nchini Denmark.

Karikatur | Der türkische Präsident Recep Tayyip Erdogan hat erneut Schweden kritisiert und will seine NATO-Mitgliedschaft nicht unterstützen
Picha: DW

Ankara pia ilimuita balozi wa Uholanzi mjini Istanbul baada ya mfuasi mwengine wa siasa kali kuchana kurasa za kitabu hicho kitakatifu kwa Waislamu mjini The Hague.

Soma zaidi: Erdogan aionya Sweden kuhusu NATO baada ya kuchomwa Qur'an

Serikali ya Uturuki ilisema kumekuwa na ongezeko la maandamano ya kuupinga utawala wake yanayofanywa na makundi "yenye mafungamano na magaidi" - kauli ambayo huitumia kumaanisha Chama cha Wafanyakazi cha Wakurdi, PKK, ambacho kimeanzisha uasi wa miongo kadhaa dhidi ya utawala wa Uturuki.

Makundi yanaounga mkono Wakurdi yamekuwa yakiandamana nchini Sweden, yakipeperusha bendera za PKK na vyama washirika. 

Maandamano hayo yamekuwa yakitumika kama hatua ya kuonesha ghadhabu kwa serikali za Sweden na Finland zilizoahidi kupiga marufuku harakati na PKK kwenye nchi zao ili kupata ridhaa ya Uturuki kwenye maombi yao ya kuwa wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO.

Uturuki yawekea mguu maombi ya Sweden, Finland

Kufuatia maandamano hayo, Rais Recep Tayyip Erdofan wa Uturuki aliionya Sweden kwamba isitarajie uungaji mkono wake kwenye maombi ya kujiunga na NATO.

Istanbul | Protest for dem schwedischen Konsulat
Maandamano mjini Istanbul kulalamikia uchomaji Qur'an nchini Sweden na Denmark.Picha: Hakan Akgun/Demiroren Visual Media/ABACA/picture alliance

Vile vile, Uturuki iliahirisha kwa muda usiojulikana mkutano muhimu uliokuwa ufanyike mjini Brussels, Ubelgiji, kujadili maombi ya Sweden na Finland kujiunga na NATO.

Soma zaidi: NATO: Uturuki iridhie uanachama wa Finland na Sweden

Mapema siku ya Jumamosi (Januari 28), kabla ya Uturuki kutoa onyo hilo la hadhari ya usafiri, mataifa ya Nordic yalitowa miongozo mipya ya usafiri kwa raia wao walioko na wanaotaka kwenda nchini Uturuki.
 
 Denmark, Finland, Norway na Sweden ziliwatolea wito raia wao wanaoitembelea Uturuki kuepuka mikusanyiko mikubwa na kuchukuwa kila hatua ya tahadhari.

Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Sweden ilisema kupitia ujumbe uliotumwa mtandaoni kwamba ubalozi wake mjini Ankara ungeliendelea kufungwa na kuwaomba wageni waliotaka kuutembelea ubalozi wake mdogo mjini Istanbul "kufanya hivyo kwa tahadhari."

"Tunawataka raia wa Sweden walioko Uturuki kufahamu kwamba matukio mabaya zaidi yanaweza kutokea," ilisema wizara hiyo, ikikusudia maandamano yaliyofanyika nchini Uturuki kupinga yale yaliyofanyika mjini Stockholm.