1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yazidi kuishambulia Ukraine kwa makombora

19 Oktoba 2023

Urusi imeendeleza mashambulizi yake kwa Ukraine katika maeneo ya mashariki, kusini na kaskazini na kupelekea mauaji ya watu wawili na mmoja kujeruhiwa huku mamlaka za Ukraine zikisema majengo na miundombinu imeharibiwa.

https://p.dw.com/p/4XlQH
Ukraine Raketenangriff Ruine
Moja ya jengo liliharibiwa na kombora katika mji wa Mykolaiv uliopo kusini mwa UkrainePicha: Viktoria Lakezina/REUTERS

Vikosi vya Urusi vimeendelea kufanya mashambulizi ya anga katika maeneo ya mashariki, kusini na kaskazini mwa Ukraine, na kusababisha vifo vya watu wawili na mmoja kujeruhiwa baada ya kombora la Urusi kuangukia mgahawa mmoja uliopo eneo la Mykolaiv, kusini mwa Ukraine. 

Soma zaidi: Bunge la Ujerumani laidhinisha bajeti kubwa kwa jeshi

Mamlaka za Ukraine zimesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba jeshi la Urusi lilishambulia eneo la kusini mwa Ukraine la Mykolaiv, na kuharibu majengo, makazi ya watu na maeneo ya biashara.

Gavana wa Mykolaiv, Vitaliy Kim ameandika katika mtandao wa kijamii kwamba mashambulizi hayo ya makombora yalifanywa mara mbili katika kijiji cha Stepove, kilichoko karibu kilomita 45 kaskazini magharibi mwa jiji la Mykolaiv .

Taarifa za mashambulizi hayo zinatolewa baada ya mashambulizi mengine ya Urusi katika mikoa mingine ya Zaporizhzhia na Dnipropetrovsk kuwaua takriban watu sita usiku wa kuamkia jana Jumatano.

Kwa upande mwingine Jeshi la anga la Ukraine limesema limedungua ndege tatu za Urusi zisizo na rubani ambazo zilikuwa zimelenga kushambulia viwanda, miundombinu, raia na kambi za kijeshi.

Rais Putin ahitimisha ziara yake China

China I Russischer Präsident Putin zu Besucht in Peking
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na rais wa China Xi Jingping alipotembelea ChinaPicha: Sergei Guneyev/Pool/picture alliance

Huku hayo yakiendelea, mapema hii leo, rais Putin amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini China, na kusikika akiusifu ushirikiriano baina ya Moscow na Beijing huku akitaka ushirkiano huo kuimarishwa zaidi ili kufidia hasara iliyotokana na kulipoteza soko la Ulaya, kutokana na hatua ya kutengwa kwa taifa hilo na mataifa mengi ya magharibi.

Moscow inatarajia kuanza kujenga bomba la kusafirisha mafuta la "Power of Siberia 2" kutoka Urusi hadi China mwaka ujao, ambalo litakuwa ni mradi mkubwa wa Urusi wa kusafirisha gesi nyingi zaidi hadi China.

Scholz aihimiza Ulaya kuendelea kuisadia Ukraine

Mjini Berlin, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Umoja wa Ulaya unatakiwa kuendelea kuisaidia Ukraine katika siku zijazo, ingawa ameonya kwamba ufadhili zaidi hauwezi kuleta suluhu ya muda mrefu.

Scholz amesema akiwa bungeni mapema leo kwamba Ulaya inalazimika kufanya hivyo na hasa kutokana na matamshi ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky yanayoainisha madhila yanayowakumba raia wa Ukraine kutokana na vita hivyo.

Deutschland | Bundestag Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwa bungeni mjini BerlinPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Olaf Scholz amesema  " nimeguswa sana kwamba Rais wa Ukraine amezungumza waziwazi kuhusu vita hivi na wahanga wa ghasia. Na hilo ni muhimu sana, kwa sababu hilo ni jambo ambalo linahusu pia mshikamano wa wale wanaokabiliwa na vurugu kutoka nje. na ambao wana haki ya kujitetea."

Ameongeza kuwa msimamo wao ni uleule kwamba watatakiwa kuendelea kutoa ufadhili kwa pamoja ili kuiwezesha Ukraine kujisimamia kifedha.