1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafungua uchunguzi mpya wa jinai dhidi ya Navalny

Saleh Mwanamilongo
30 Desemba 2020

Wachunguzi wa umma nchini Urusi wamesema wamefungua mashtaka mapya ya jinai dhidi ya Alexei Navalny ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali nchini humo.

https://p.dw.com/p/3nMa3
Urusi yafungua uchunguzi mpya wa jinai dhidi ya Alexei Navalny
Urusi yafungua uchunguzi mpya wa jinai dhidi ya Alexei NavalnyPicha: Vasily Maximov/APF/Getty Images

Wachunguzi wa umma nchini Urusi wamesema wamefungua mashtaka mapya ya jinai dhidi ya Alexei Navalny ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali nchini humo. Navalny ameilezea hatua hiyo kuwa ni kichekesho. 

Wapelelezi hao wanamtuhumu Navalny na washirika wake ambao hawakutajwa, kwa kutumia takriban dola milioni 5 kwa mahitaji binafsi ilhali ni misaada ya umma kwa mashirika anayosimamia.

Kamati ya uchunguzi imeeleza kwamba Navalny alizitumia fedha hizo kwa kununua vifaa vyake binafsi na kuhudumia likizo zake binafsi nje ya Urusi. Akikutwa na hatia, Navalny huenda akahukumiwa hadi kifungo cha miaka kumi jela kulingana na sheria ya Urusi.

''Navanly anaweza kurejea nyumbani''

Wakili wa Navalny amesema kuwa viongozi wa Urusi walimtaka Navanly kurejea nchini kabla ya Jumanne ya Desemba 29. Mamlaka ya Magereza imemshutumu Navalny kwa kukiuka masharti ya hukumu ya kifungo ambacho bado anatumikia tangu mwaka 2014. Urusi ilidai kwamba Navalny anaweza kurejea nyumbani kama raia wengine.

Dmitri Peskov msemaji wa rais wa Urusi Vladimir Putin
Dmitri Peskov msemaji wa rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: picture-alliance/M.Metzel

Dmitri Peskov msemaji wa rais wa Urusi, amesema Navalny anaweza kurejea nyumbani kama raia wengine.

''Kila raia wa Urusi yuko huru kurejea nchini. Na hakuna vizuizi kwa yeyote yule. Kuhusiana na hali ilivyo nadhani ni bora kwa mamlaka ya magereza ambayo ilitoa ilani hiyo kutoa taarifa.''

Hatua hiyo huenda ikatizamwa kama ishara ya hivi karibuni ya Urusi kumkamata Navalny ambaye anaendelea kupona nchini Ujerumani baada ya jaribio la kuuawa kwa kuwekewa sumu mwezi Agosti.

Kwenye mtandao wake wa Twitter, Navalny aliandika kwamba hatua hiyo inaonesha kwamba Rais Vladmir Putin anakumbwa na jazba dhidi yake. Huku akiwatolea mwito wafuasi wake kupuuza uchunguzi huo ambao aliuita kuwa hatua ya kichekesho na kuwaomba waendelee kuchangia misaada kwa ajili ya mashirika yake.

Urusi yawwawekea vikwazo maafisa wa Uingereza

Mpinzani huyo wa Rais Putin amesema uchunguzi dhidi yake, unatokana na kashfa ya sumu aliopewa mwezi Agosti. Navalny ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Rais Putin. Hata hivyo Urusi ambayo imepinga madai ya kumtilia Navalny sumu, imesema yuko huru kurejea nyumbani.

Navalny amesema wanataka kumtupa jela kwa sababu walishindwa kumuuwa na kwa sababu amekuwa akichunguza kuhusu watu waliopanga njama ya kumuuwa.

Hii leo, Urusi imetangaza kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa Uingereza, kuhusiana na tuhuma za kupewa sumu Navalny. Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya iliishutumu Urusu kuumpa sumu mpinzani huyo wa Putin.