1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani kuandamana Kongo licha ya marufuku ya serikali

Saleh Mwanamilongo
27 Desemba 2023

Wiki moja baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 20, zoezi la kuhesabu kura linaendelea polepole huku kukiwa na mito ya maandamano ya kupinga uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/4ac3r
Polisi wamewatawanya waandamanaji waliojaribu kukusanyika jijini Kinshasa kuduatia mwito wa upinzani kutaka uchaguzi mkuu urudiwe
Polisi wamewatawanya waandamanaji waliojaribu kukusanyika jijini Kinshasa kuduatia mwito wa upinzani kutaka uchaguzi mkuu urudiwePicha: Benjamin Kasembe/DW

"Uchaguzi wa Desemba 20, 2023 lazima ufutwe.'' ,alisema Mino Bompomi, mratibu wa kitaifa wa shirika la kiraia la Filimbi alianza mkutano wake na waandishi wa habari, mjini Kinshasa. Baada ya sherehe za Krismasi, baadhi ya viongozi wa upinzani waliitisha maandamano ya kupinga kile walichokiita "uchaguzi bandia".

Wapinzani hao ni pamoja na Martin Fayulu, Denis Mukwege na Théodore Ngoy ambao wanapinga pia kuongezwa muda wa ziada wa zoezi la upigaji kura nchini.

''Kuandamana na kupinga mapinduzi ya uchaguzi''

Viongozi wa upinzani Martin Fayulu (kulia), Theodore Ngoy na Denis Mukwege (kushoto) wameitisha maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi
Viongozi wa upinzani Martin Fayulu (kulia), Theodore Ngoy na Denis Mukwege (kushoto) wameitisha maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguziPicha: Paul Lorgerie/DW

Theodore Ngoy msemaji wa kundi la wagombea watano wa uchaguzi huo amesema hawayatambuwi matokeo yanayotangazwa na tume ya uchaguzi.

''Wananchi wa Kongo ni mashahidi na waathiriwa wa kasoro za wazi za uchaguzi bandia uliofanywa na tume ya uchaguzi Ceni. Wananchi watakuwa mitaani Jumatano hii, Desemba 27, 2023 kuandamana na kupinga mapinduzi ya uchaguzi yanayoandaliwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kadima na tume ya Ceni.'', alisema Ngoy. 

Wakati upinzani uligawanyika katika kambi mbalimbali wakati wa kampeni za uchaguzi, ambapo Martin Fayulu na Denis Mukwege walikataa kuungana, sasa wanashirikiana kwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo kupitia maandamano. Wanachama mbalimbali wa upinzani wamethibitisha kuwa majadiliano yanaendelea na kwamba maandamano ya pamoja yanaweza kupangwa katika siku zinazofuata. Hervé Diakiese, msemaji wa Ensemble pour la République, chama cha Moïse Katumbi ameapa kwamba chama chao hakitosita kuungana na vyama vingine ili kulazimisha uchaguzi urudiwe.

Marufuku ya serikali kwa maandamano

Rais anayewania muhula wa pili Felix Tshisekedi ameongoza kwenye matokeo ya awali akifuatiwa na Moise Katumbi na Martin Fayulu
Rais anayewania muhula wa pili Felix Tshisekedi ameongoza kwenye matokeo ya awali akifuatiwa na Moise Katumbi na Martin Fayulu

Waziri wa mambo ya ndani Peter Kazadi alisema maandamano hayo hayataruhusiwa kwa sababu yanalenga kuvuruga mchakato wa kuhesabu kura. Wakati huohuo, serikali imewapeleka maelfu ya polisi na wanajeshi kwenye mji wa Lubumbashi ambayo ni ngome ya mpinzani Moise Katumbi. Ikielezea hatua hiyo kama ishara ya kuzuia vurugu.

Enoch Kavindele, kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika SADC amesema wanasubiri kuona mchakato wa kuhesabu kura unakamilika kwa amani.

''Hatuna ushahidi kuhusu hilo, sisi kama watu wengine pia tunasubiri ,na tunaamini kama tume ya uchaguzi itafanya kazi nzuri. Kwa kini CENI ikubali matokeo ambayo haiendani na matakwa ya watu.'', alisema Kavindele.

Tshisekedi aongoza kwenye matokeo ya awali

Swali kubwa hivi sasa ni ikiwa upinzani utafaulu kuwashawishi raia kuandamana au hapana, huku rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili akionekana kuongoza kwa kiasi kikubwa katika matokeo ya awali. Tayari kura zaidi ya milioni sita zimekwisha hesabiwa na rais Tshisekedi ameongoza kwa asilimia 78, huku mpinzani wake wa karibu  Moise Katumbi akiwa na asilimia 14 na Martin fayulu akishikilia nafasi ya tatu na asilimia 4 za kura.