1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka Sudan kusitisha uhasama wakati wa Ramadhan

Sylvia Mwehozi
9 Machi 2024

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka pande zinazozozana nchini Sudan kukomesha mara moja uhasama wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuruhusu misaada kuwafikia watu milioni 25.

https://p.dw.com/p/4dKaJ
Wakimbizi wa Sudan
Wakimbizi wa Sudan waliokimbia vita Picha: LUIS TATO/AFP

Azimio hilo linaelezea wasiwasi mkubwa juu ya kuenea kwa vurugu na kuzorota kwa hali ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na viwango vya ukosefu mkubwa wa chakula, hasa mkoa wa Darfur.

Naibu balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa James Kariuki amezihimiza pande hasimu nchini Sudan kutafuta njia endelevu kusuluhisha mzozo huo kupitia mazungumzo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu milioni 8.3 wameyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa RSF.

Sudan
Wakimbizi wa SudanPicha: LUIS TATO/AFP

Sudan ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili, wakati mvutano wa muda mrefu kati ya jeshi la nchi hiyo likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, nawaasi wa kikosi cha RSF kinachoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo walipozua mapigano katika mji mkuu wa Khartoum.

Mapigano yameenea katika maeneo mengine ya nchi, hasa mijini lakini katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan mapigano hayo yalichukua sura tofauti, kutokana na mashambulizi ya kikatili ya vikosi vya RSF ambavyo vinavyotawaliwa na Waarabu dhidi ya makabila mengine.

WFP: Sudan kuwa "janga kubwa zaidi la njaa duniani"Maelfu ya watu wameuawa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizitaka pande zote mbili siku ya Alhamisi kuunga mkono usitishaji vita wa Ramadhani, na kuonya kuwa mgogoro huo wa karibu mwaka mzima unatishia umoja wa nchi na "unaweza kusababisha ukosefu mkubwa wa utulivu wa kikanda." Umoja wa Afrika pia umeunga mkono kusitisha mapigano wakati wa Ramadhani.

Burhan amekaribisha wito wa Guterres, lakini wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilitoa taarifa siku ya Ijumaa ikiorodhesha idadi ya masharti kwa ajili ya kusitisha mapigano kuwa na ufanisi.

Sudan
Wakimbizi wa SudanPicha: Mohammad Ghannam/MSF/REUTERS

Naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Anna Evstigneeva amelishutumu Baraza la Usalama kwa "unafiki" baada ya kushindwa kupitisha azimio la kutaka kusitishwa kwa vita vya Israel na Hamas huko Gaza, akimaanisha kura ya turufu ya Marekani.

Alidai vipengele vingi katika azimio hilo tayari vinafanyika, akisisitiza kuwa kukomeshwa ghasia lisiwe tu lengo la Baraza la Usalama "lakini muhimu zaidi kwa watu wa Sudan wenyewe".Pande hasimu zatenda uhalifu wa kivita Sudan - UN

Akihutubia Baraza la Usalama siku ya Alhamisi, katibu mkuu Guterres aliashiria mashambulizi mapya, kuongezeka kwa hofu ya uhasama mashariki mwa Sudan, wito wa raia kupatiwa silaha katika majimbo mbalimbali, na makundi yenye silaha kuingia kwenye mapigano huko Darfur na Kordofan Kusini.