1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Wolfgang Schäuble afariki dunia akiwa na miaka 81

Iddi Ssessanga
27 Desemba 2023

Mwanasiasa mashuhuri wa chama cha CDU nchini Ujerumani Wolfgang Schäuble amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81. Schäuble alikuwa waziri wa fedha wa Angela Merkel wakati wa mzozo wa madeni wa kanda ya sarafu ya Euro.

https://p.dw.com/p/4acAO
Ujerumani | Mwanasiasa mashuhuri Wolgfanga Schäuble amefariki dunia
Schäuble amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81.

Spika wa zamani wa bunge la Bundestag na waziri wa fedha Wolfgang Schäuble amefariki akiwa amezungukwa na familia yake, ambayo kwa mara ya kwanza ililiarifu shirika la habari la Ujerumani DPA kuhusu kifo chake mapema Jumatano. Schäuble alikufa kwa amani majira ya saa mbili Jumanne usiku, familia yake ilisema.

Akiwa mwanachama mkongwe na mashuhuri wa chama cha Christian Democrats, CDU, Schäuble alizaliwa huko Freiburg mnamo 1942. Aliingia bungeni mwaka wa 1972 na kuchaguliwa tena moja kwa moja kuliwakilisha eneo lake la Offenburg katika kila uchaguzi uliofuata, na kumfanya kuwa mbunge wa muda mrefu zaidi katika historia ya baada ya vita vya Ujerumani.

Yumkini alikuwa mtu mashuhuri zaidi kimataifa wakati wa msukosuko wa kifedha wa 2008 na matatizo ya madeni ya kanda ya euro, wakati alipokuwa waziri wa fedha wa Ujerumani, akitoa wito kwa nchi za kusini mwa Ulaya kupunguza ukopaji wao. Alikua mtu mashuhuri, na mara nyingi alitukanwa, katika nchi kama Ugiriki katika kipindi hiki.

Ujerumani| Angela Merkel na Wolfganga Schäuble
Schäuble alikuwa mtu wa akribu sana wa Kansela Angela Merkel, kushoto.Picha: Andreas Rentz/Getty Images

Lakini wakati mmoja, Schäuble pia alionekana kuwa anayefuata katika mstari baada ya Kansela Helmut Kohl katika wadhifa wa juu wa kisiasa wa Ujerumani. Alikuwa amehudumu katika nyadhifa kadhaa serikalini ikiwa ni pamoja na waziri wa mambo ya ndani. Huo ndiowadhifa alioshikilia mwaka 1990, wakati jaribio la mauaji na majeraha ya risasi yalipomfungia kwenye kiti cha magurudumu maisha yake yote. Ameacha mke Ingeborg na watoto wanne.

Rambirambi na sifa

Kiongozi wa sasa wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, Friedrich Merz alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kuzungumzia kifo chake Jumatano mtandaoni. Alisema kifo cha Schäuble "kinanijaza huzuni kubwa."

Soma pia: Wolfgang Schaueble spika mpya Bundestag

"Kwa Wolfgang Schäuble, ninampoteza rafiki yangu wa karibu na msiri ambaye nimewahi kuwa naye katika siasa," Merz alisema kwenye mtandao wa kijamii, akitia saini na herufi zake za kwanza kuashiria kuwa aliandika chapisho hilo. "Mawazo yangu yako kwa familia yake, hasa mkewe Ingeborg."

Kansela wa sasa Olaf Scholz, Msosho Demokrat ambaye alimrithi Schäuble kama waziri wa fedha mnamo 2018, alisema "ameunda nchi yetu kwa zaidi ya nusu karne," kama mbunge, waziri na kama spika wa bunge.

"Kwake Ujerumani imepoteza mwanafikra mahiri, mwanasiasa mwenye shauku na mdemokrati thabiti," Scholz alisema.

"Akili yake, upendo wake wa mijadala ya kidemokrasia, mtazamo wake wa kihafidhina wa ulimwengu na matamshi yake makali yalimfanya aonekane bora kwa muda mrefu," alisema Scholz katika taarifa.

Wolfgang Schäuble baada ya kunusurika kuuawa.
Mnamo Oktoba 12, 1990, Schäuble, kulia, aliekuwa waziri wa mambo ya ndani, alijeruhiwa katika jaribio la mauaji.Picha: Norbert Försterling/dpa/picture-alliance

Mwanasiasa mkongwe wa chama cha Kijani Katrin Göring-Eckhardt alichapisha wasifu mrefu, akisema nchi imempoteza "mtetezi mwenye shauku ya demokrasia ya bunge letu," ambaye alisema alikua akimheshimu sana licha ya "kutofautiana itikadi za kisiasa."

Soma pia: Ujerumani yataka Ugiriki ibakie katika kanda ya Euro

"Nilithamini uwezo wake katika mjadala, ustahimilivu wake, hakuwa anang'ag'ana kila mara lakini alikuwa muwazi kila wakati, akibakia katika majadiliano, katika ngazi ya juu na yenye changamoto," Göring-Eckhardt alisema, akisifu miongo yake ya utumishi wa kisiasa.

Baraza Kuu la Wayahudi nchini Ujerumani pia lilituma ujumbe wa heshima, likimuita mzee huyo wa miaka 81 "rafiki wa karibu wa jumuiya ya Wayahudi nchini Ujerumani."

Chanzo: dpa, dw