1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi 4 zataka mageuzi ya Baraza la Usalama la UN

Grace Kabogo
21 Septemba 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock anakutana na mawaziri wenzake wa kundi la nchi nne zinazojulikana kama G4 kujadiliana namna ya kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/4WeoC
USA New York | 78. UN-Generalversammlung | Sicherheitsrat | Wolodymyr Selenskyj, Präsident Ukraine
Ukraine yatoa wito Ujerumani kuwa na kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Picha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Baerbock anakutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Brazil, Japan na India, mataifa ambayo yote yanaunga mkono juhudi za kila mmoja kuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Marekani, China, Urusi, Uingereza na Ufaransa zote zina viti vya kudumu, na utanuzi wa baraza hilo ni mada ambayo imekuwa ikijadiliwa mara kwa mara kwa miongo kadhaa.

Zelensky na wito wa Ujerumani kuwa mwanachama wa kudumu

Siku ya Jumatano, kufuatia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Baerbock alisema kwamba Ujerumani inaweza kufikiria kuwa mwanachama wa kudumu.

Akilihutubia jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alisema Ujerumani inapaswa kupewa kiti cha kudumu kwenye baraza hilo, kwani nchi hiyo imekuwa moja ya wadhamini wakuu wa amani na usalama.

USA | Annalena Baerbock in Washingtion
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Poland imesema Alhamisi kuwa inapinga Ujerumani kupewa kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku Waziri wake wa Ulinzi Mariusz Blaszczak, akilitaja pendekezo hilo la Ukraine kama lenye kukatisha tamaa, na kudai kuwa Ujerumani ilisitasita kuiunga mkono Ukraine katika siku za mwanzo za uvamizi wa Urusi.

Libya yatoa wito kwa nchi hiyo kupatiwa msaada wa kimataifa

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Vijana na Michezo wa serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli, ambaye pia anakaimu nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje, Fathallah al-Zani ameuhutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu maafa yaliyoikumba nchi hiyo na ametoa wito kwa nchi yake kupatiwa msaada wa kimataifa.

''Ninautolea wito ulimwengu kutekeleza wajibu wake kwa Libya, ili kusaidia kukabiliana na maafa haya. Hasa, kuchukua hatua muhimu za kiafya ili kuwalinda walionusurika katika jiji la Derna na miji jirani ili kuepusha maafa ya kiafya ambayo wataalam wanaonya kuwa yanaweza kutokea,'' alisisitiza al-Zani.

Sudan | General Abdel Fattah Al-Burhan
Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Sudanese Army/AFP

Mwanasiasa huyo wa ngazi ya juu wa Libya pia amewatolea wito wananchi wa Libya kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa na kuonyesha mshikamano na umoja, katika kukabiliana na majanga yaliyosababishwa na kimbunga Daniel.

Naye kiongozi wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan pia siku ya Alhamisi anatarajiwa kuhutubia katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wiki moja baada ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes kujiuzulu.

Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pia linatarajia kufanya kikao cha dharura kuijadili hali inayoendelea Nagorno-Karabakh, baada ya shambulizi la Azerbaijan ambalo watu wanaotaka kujitenga, wamesema limewaua watu 200.

(DPA, AP, DW)