1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Uingereza yashinikizwa kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel

Tatu Karema
4 Aprili 2024

Majaji watatu wa zamani wa mahakama ya juu nchini Uingereza wameungana na zaidi ya wafanyakazi 600 wa kisheria nchini humo kutoa wito kwa serikali kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel

https://p.dw.com/p/4eQ5B
Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akielezea kuhusu mpango wa kuzuia uhamiaji haramu wakati wa mkutano wa habari mnamo Desemba 7 2023
Waziri mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: James Manning/AP/picture alliance

Majaji hao watatu walijiunga na mawakili, majaji wa zamani na wasomi wa sheria katika kumtaka waziri mkuu wa nchi hiyo Rishi Sunak kubadili sera ya uuzaji silaha na kutilia mkazo wito wa idadi kubwa ya wanasiasa wa upinzani wanaotaka kusitishwa kwa uuzaji huo wa silaha kwa Israel.

Huenda Uingereza ikahusishwa na mauaji ya halaiki katika ukanda wa Gaza

Katika barua ya kurasa 17, majaji na mawakili hao walisema kuwa msaada wa silaha wa Uingereza kwa Israel huenda ukaifanya nchi hiyo kuwa mshirika katika mauaji ya kimbari pamoja na ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Soma pia:Israel yasema shambulizi lililowauwa wafanyakazi wa misaada lilikuwa "kosa kubwa"

Barua hiyo imeendelea kusema kuwa sheria hiyo inatambua wazo la kusaidia kitendo kibaya cha kimataifa.

Netanyahu aghadhabishwa na madai ya mauaji ya kimbari

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameyataja madai hayo ya mauaji ya kimbari kuwa ya kuchukiza na kusema kuwa Israel imejitolea kikamilifu kuzingatia sheria ya kimataifa.

Soma pia:Austin aghadhibishwa na kuuwawa wafanyakazi wa misaada Gaza

Mmoja wa majaji hao wa zamani Jonathan Sumption, ameliambia shirika la habari la Uingereza BBC kwamba ana wasiwasi kuwa serikali ya Uingereza imepoteza muelekeo wa jukumu lake la kuzuia mauaji ya kimbari.

Sunakamepinga miito hiyo ya kusitisha uuzaji wa silaha na kusema nchi hiyo ina utaratibu makini wa utoaji leseni ambao itazidi kuzingatia.

Rais Joe Biden alaani mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa msaada Gaza

Rais wa Marekani Joe Biden, ameongoza shtuma za kimataifa kuhusu shambulizi dhidi ya wafanyakazi wa shirika linalosambaza chakula huko Gaza la World Central Kitchen waliokuwa wakisambaza chakula katika eneo hilo.

Rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano na wanahabari mjini Washington mnamo Januari 12, 2023
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Andrew Harnik/AP/picture alliance

Biden amesema kuwa ameghadhabishwa na kuvunjwa moyo na shambulizi hilo baya lililosababisha vifo vya mfanyakazi mwenye uraia pacha wa Marekani na Canada, watatu wa Uingereza , mmoja wa Poland, mwengine wa Australia na wa mwisho kutoka Palestina.

Kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu vita vya Israel Gaza

Matamshi hayo makali ya Biden na kusisitiza kwake kwamba Israel ichukue hatua zaidi za kuwalinda wafanyakazi wa msaada pamoja na raia, yanaashiria ongezeko la mafadhaiko kuhusu jinsi Israel inavyaoendesha vita vyake dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas.

Israel yasema shambulizi la Gaza ni kosa

Israel imekiri kuhusika katika shambulizi hilo ililoliita kosa huku waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Yoav Gallant akiviagiza vikosi vya kijeshi nchini humo, kudumisha njia wazi ya mawasiliano na mashirika ya msaada ya kimataifa.

Waziri mkuu wa Poland ataitaka Israel kufidia familia za waathiriwa

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, pia ameelezea kughadhabishwa kwake na shambulizi hilo wakati alipofanya mazungumzo na Gallantwakati Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, akisema lazima Israel iombe msamaha na kuzifidia familia za waathiriwa.

Haya yanajiri wakati ambapo rais Biden anatarajiwa leo kufanya mazungumzo na Netanyahu.