1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yawarai raia wake kutozuru Mashariki ya Kati

12 Aprili 2024

Ufaransa imewashauri raia wake kutofanya safari za kwenda Israel, Iran, Lebanon au eneo la Ukingo wa Magharibi kufuatia wasiwasi unaongezeka wa kutanuka kwa mzozo wa kijeshi kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4ehpS
Stéphane Séjourné
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Stéphane SéjournéPicha: JOSEPH EID/AFP

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Stéphane Séjourné ametoa ushauri na tahadhari hiyo wakati wa mkutano wa dharura wa usalama uliotishwa na serikali ya nchi hiyo.

Amesema maafisa wa Ufaransa hawatotumwa kwenda mataifa aliyoyataja na familia za wanadiplomasia wa nchi hiyo zinapaswa kuondoka mara moja kutoka mji mkuu wa Iran, Tehran. Tahadhari kama hiyo imetolewa pia na Urusi na India.

Israel yaapa kujibu iwapo Iran itashambulia

Inafuatia matamshi ya viongozi wa Iran wanaosema wako mbio kulipa kisasi kwa shambulizi la mnamo Aprili Mosi inaloaminika kufanywa na Israel dhidi ya jengo la ubalozi wa Iran nchini Syria . 

Watawala mjini Tehran wamesema Israel imefanya "kosa kubwa na ni lazima iadhibiwe." Israel nayo imeonya kwamba itajibu kikamilifu shambulizi lolote kutoka Iran.