1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa kuwandoa wanajeshi wake Niger

Sudi Mnette
25 Septemba 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kuondoka kwa jeshi lake huko Niger, hatua inayokwenda sambamba na kumrejesha nyumbani balozi wa Ufaransa baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa rais Mohammed Bazoum

https://p.dw.com/p/4Wlio
Paris TV Interview Macron
Picha: Geoffroy van der Hasselt/AFP

Tangazo hilo la Jana Jumapili, limepokelewa vyema na viongozi wa kijeshi wa Niger wakisema ni hatua njema kuelekea uhuru wa taifa lao. Tangazo hilo la Rais Macron linatolewa ikiwa ni takribani miezi miwili baada ya kushuhudiwa mapinduzi yaliomuondoa rais aliye madarakani.

Katika mahojiano maalumu kupitia televisheni ya Ufaransa, pasipo kutoa ufafanuzi wa kina, Macron alisikika akisema Ufaransa imeamua kumuondoa balozi wake katika kipindi cha masaa kadhaa yajayo lakini pia wanadiplomasia wake kadhaa watarejea nyumbani. Aliongeza kuwa ushirikiano wa kijeshi "umekwisha" na wanajeshi wa Ufaransa watajiondoa katika "miezi na wiki zijazo" na kujiondoa kikamilifu "mwishoni mwa mwaka".

Ufaransa ilikuwa Niger kwa ombi lao na la Burkina Faso na Mali

Frankreich | Paris Air Show in Le Bourget
Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika operesheni zao za kijeshiPicha: Lewis Joly/AP Photo/picture alliance

Zaidi Macrona anasema "Tulikuwa katika ardhi ya Niger kwa ombi lao, la Burkina Faso na Mali.  Na operesheni ya kijeshi la Barkhane, imekuwa ya mafanikio kwa sababu bila ya hiyo, nchi nyingi kati ya hizi zingekuwa tayari zimechukuliwa na makundi ya wenye itikadi kali." Alisema rais huyo wa Ufaransa.

Pasipo kuchelewa watawala wa kijeshi wa Niger walijibu hatua hiyo kupitia taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa. Watawala hao wanaoshikilia hatamu ya uongozi tangu Julai 26, kupitia taarifa yao ya kijeshi walisema "Wanasherehekea hatua mpya kuelekea uhuru wa Niger." Na kuongeza pia huu ni wakati wa kihistoria, ambao unaelezea hisia za watu wa Niger.

Kuzuiwa kuruka ndege kwa anga ya Niger

Lakini pia mapema Jumapili Shirika la Usalama wa Usafiri wa Anga barani Afrika na Madagascar (ASECNA) lilisema kwenye tovuti yake kwamba watawala wa kijeshi wamepiga marufuku "ndege za Ufaransa" kuruka katika anga ya nchi hiyo. Ingawa haikuwa wazi ikiwa hatua hiyo ingeathiri balozi huyo wa Ufaransa kuweza kusafri nje ya mipaka ya taifa hilo.

Katika taarifa yake, Macron alisema katika majuma na miezi ijayo, watashauriana na wahusika huko Niger kwa sababu wangependa hatua hiyo ifanyike kwa amani. Ufaransa ina takriban wanajeshi 1,500 nchini Niger kama sehemu ya kikosi cha kupambana na wenye itikadi kali  katika eneo zima la Sahel.

Soma zaidi:Mali, Niger, Burkina Faso wanakabiliwa na uasi wa jihadi kwa muda mrefu

Macron alisema mamlaka ya baada ya mapinduzi haitaki tena kushiriki vita dhidi ya ugaidi. Na kwamba viongozi wa kijeshi wa Niger walimtaka balozi wa Ufaransa nchini mwao kuondoka baada ya kumpindua Rais Bazoum.