1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uelewe ugonjwa wa Ebola

Philipp Sandner18 Agosti 2014

Ugonjwa wa Ebola umekuwa chanzo cha wasiwasi na uvumi. Vipi mtu huweza kuepuka kuambukizwa na ugonjwa huo? Na hatua gani aichukue akikutana na mgonjwa? DW imetafuta majibu ya maswali haya na mengine unayoweza kujiuliza.

https://p.dw.com/p/1Cwb9
Liberia Ebola Plakat in Monrovia
Picha: Reuters

Je, ni zipi dalili za kwanza ambazo mtu anaweza kugundua kwamba ameambukizwa ugonjwa wa ebola.

Maradhi hayo yanaenezwa na virusi. Ishara muhimu ni hali ya kutokwa na damu katika sehemu tofauti za mwili kama vile katika ufizi, pua, katika njia ya haja ya mbele na nyuma na kwingineko. Lakini kabla ya kufika daraja hilo, kwanza mtu huwa na homa kali, viwango vya joto vya mwili vinapanda sana, kisha anaweza kuwa anajisikia kutapika, na hata kutapika kwenyewe. Mara nyingine anaweza kuharisha, na pia kuwa mnyonge, viungo vyake vikiwa na maumivu. Wakati mwingine anaweza kuumwa tumbo au kichwa. Hata hivyo, njia ya pekee ya kuthibitisha mtu ana virusi ni kupitia maabara.

Huduma gani ya kwanza ambayo mtu anaweza kumpa yule aliyeambukizwa virusi vya ebola?

Kwanza kabisa ni muhimu kufika katika kituo cha afya haraka iwezekanavyo. Kuvigundua virusi vya ebola kunahitaji maabara ambayo ina uwezo wa kutosha. Kwenye vituo vya afya vya kawaida labda hawataweza kuvigundua kwa haraka.

Jambo la kwanza ni kuchunguza na kuhakikisha kwamba mtu ana virusi hivyo. Halafu jambo la pili ni kumtenga na watu wengine ili yeye mwenyewe asidhurike zaidi na asiwadhuru wengine. Mpaka sasa hakuna dawa maalumu ambayo inatumika kuwatunza wale walio na virusi. Dawa zilizoko bado ziko ngazi ya majaribio tu. Lakini mgonjwa anaweza kupewa dawa nyingine ambazo zaweza kumsaidia kupunguza joto na kupunguza maumivu, na kadhalika. Watu kwenda kupata huduma ni jambo muhimu sana.

Mtu anawezaje kuambukizwa virusi vya ebola?

Kwa bahati nzuri, virusi vya ebola havienei kwa njia ya hewa. Vinaenezwa kwa mtu kugusana na yale majimaji ya mwili, kama vile matapishi, mate, jasho, machozi, ama manii au shahawa kama mtu amegusana na mtu katika njia ya ngono.

Watu gani wanakabiliwa na hatari zaidi kuambukizwa Ebola?

Madaktari na wauguzi, wale wanaowatunza wagonjwa wa ebola, watu wenye uhusiano wa karibu na mtu aliyeambukizwa, watu wanaogusa maiti ya mtu mwenye virusi hivyo.

Mtu mwenye afya nzuri ambaye ameambukizwa na virusi hawezi kuvieneza kwa wengine ili mradi hajaonyesha dalili ya kuwa mgonjwa. Wakati wa kuwa mgonjwa, mara nyingi huwa mdhaifu kiasi cha kumzuia kusafiri bila ya kusaidiwa. Kwa hiyo, shirika la afya duniani WHO linatoa kauli ya kwamba hatari ya kuambukizwa kwenye safari ya ndege ni chini sana. Hata hivyo, watu hushauriwa kuwa waangalifu kuhusiana na hali yao na afya na ile ya wasafiri wengine.

Mtu anaweza kuchukua tahadhari gani ili asiweze kuambukizwa, awapo karibu na mgonjwa?

Deutsche Welle Kiswahili Redaktion Cartoon zu Ebola
Picha: DW/D. Gakuba

Ikiwa kuna ishara zinazoonyesha kuwa mtu huenda ana virusi hivyo, kwanza kabisa ni kumtenga yule mtu na kuhakikisha anapelekwa kwenye kituo cha afya.

Halafu ni kuhakikisha kuwa katika mazingira yetu, nyumba zetu, tunatumia dawa ambazo zinaweza kuua vijidudu, na kujihadhari sana kutomshika mgonjwa kwa mikono iliyo wazi. Badala yake, inabidi kutumia glavu na nguo nyingine maalumu ya kujikinga na viini.

Muhimu ni kujihadhari sana kuhusiana na majimaji yote yanayotoka kwenye mwili. Lazima tutumie zile dawa za kuuwa vijidudu katika choo, katika matapishi, katika mate na majimaji yoyote yanayotoka katika mwili wa yule na kiisha kuweza kupata kumtenga yule mgonjwa katika zahanati ama katika hospitali ili kuhakikisha kuwa wale wanaomhudumia wana ujuzi wa kutosha kutoeneza maradhi hayo.

Ni upi ukweli kuhusu uvumi juu ya matumizi ya aina ya chakula na maji katika kujikinga na ugonjwa wa Ebola?

Uvumi kwamba mtu anaweza kujikinga kwa kula chakula fulani ama kwa kunywa maji fulani hauna misingi yoyote. Badala yake, hatua bora ya kupunguza hatari ya maambukizi katika maisha ya kila siku ni kuongeza usafi wa mwili, hasa kunawa mikono.

Ushauri na maelezo yametolewa na Daktari Mohammed Karama kutoka taasisi ya utafiti wa magonjwa nchini Kenya(Kenya Medical Research Institute - KEMRI) na shirika la afya duniani WHO.

Mwandishi: Philipp Sandner

Mhariri: Daniel Gakuba