1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia akutana na wanawake kwenye siku ya Demokrasia

Georges Njogopa15 Septemba 2021

Dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya demokrasia na huko nchini Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na wanawake kama sehemu ya maadhimisho hayo.

https://p.dw.com/p/40Lrr
Tansania Dodoma | Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Habari Maalezo

Rais Samia anatumia jukwaa la wanawake kufikisha ujumbe unaomulika masuala ya demokrasia hasa wakati huu kukiwa na msukumo mkubwa unaotaka fursa sawa za uongozi kwa wanawake na wanaume.

Ingawa kumekuwa na juhudi kubwa ya kuziba pengo la fursa za uongozi kwenye ngazi zote za maamuzi, bado wanawake wanaendelea kuandamwa na vikwazo vingi pindi wanapotaka kujitokeza kwenye ngazi za kisiasa na ndiyo maana kwenye kongamano la leo sehemu kubwa ya ujumbe ni ule unaotaka wanawake kuendelea kuaminika na kupewa nafasi.

''Mpaka leo tunazungumzia wanawake wajasiriamali,wanawake wafanyabiashara wakubwa,lakini wanawake makontrakta wako wengi nchini,ingawa bado kunachangamoto ndogondogo ambazo tunatakiwa kuzifanyia kazi  iliwaweze kufanya kazi zao .'',alisema Samia.

Ama, siku hii ya leo inaadhimishwa huku kukiwa na maoni tofauti kuhusiana na hali jumla ya ukuzaji wa demokrasia huku wengi wakiona kwamba vitendo kama vile kuendelea kubanwa kwa vyama vya siasa kufanya baadhi ya majukumu yao ikiwamo mikutano ya wazi ni doa linalopaswa kushughulikiwa.

Tanzania bado inasafari ndefu

Women gathered in Dar es Salaam, Tanzania
Picha: DW/E. Boniphace

Mara kwa mara viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa wakijikuta wakiangukia mikononi mwa dola kutokana na harakati zao za kisiasa, na wakati wote jeshi la polisi limekuwa likitupia lawama kutokana na kilekinachoelezwa kuingilia baadhi ya shughuli za vyama hivyo.

Chama cha NCCR Mageuzi ambacho hivi karibuni kilishindwa kufanya mkutano wake wa kamati kuu baada ya kuzingirwa na jeshi la polisi kinasema, ingawa siku ya demokrasia ina umuhimu wake mkubwa, lakini Tanzania bado inasafari ndefu, kama anavyosema mkuu  wa idara ya uenezi na mawasiliano ya umma, Edward Simbeye.

Kuwaleta pamoja wanawake

Hata hivyo kuwepo kwa kongamano hilo lililowaleta pamoja wanawake wa kada mbalimbali, huenda ikawa ni ishara nyingine ambayo serikali inavyotambua umuhimu wa ukuzaji wa demokrasia na kuwepo uhuru wa maoni.

Lakini baadhi ya wadadisi wa mambo wanahoji kufanyika kwa kongamano hilo katika kilele cha siku hii kwa kuwaleta pamoja wanawake pekee,ili hali siku hii ni ya demokrasia duniani. 

Siku ya demokrasia duniani iliasisiwa na Umoja wa Mataifa katika azimio lake lilipitishwa New Yorok, Marekani kama hatua ya kuhimiza dunia kutumbua na kuzingatia masuala ya ukuzaji wa demokrasia na kuepuka ukandamizaji wa haki.