1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Nigeria yaweka kikomo cha utoaji pesa zilizopo benki

6 Januari 2023

Kikomo cha utoaji pesa nchini Nigeria kimezua wasiwasi miongoni mwa raia na wafanyabiashara. Siku za usoni, raia hawataweza kutoa zaidi ya naira 20,000 ambayo ni sawa na dola 44 kwa siku na naira 500,000 kwa wiki.

https://p.dw.com/p/4LpC6
Öl Globaler Einfluss Geld Finanzen Nigeria Naira
Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Wakati serikali ya Nigeria ikijaribu kupunguza pesa katika mzunguko na kuongeza matumizi ya sarafu za kidijitali, tangazo la sera hiyo, ambalo litaanza kutekelezwa Januari 9 mwaka huu, linajiri wiki moja baada ya serikali kuzindua rasmi noti mpya za naira.

Ingawa wataalam wanasema katika nadharia sera hizo zina mantiki lakini wanaonya kuwa kuchukuliwa kwa wakati mbaya kunaweza kupunguza ufanisi wake. Uchumi wa Nigeria bado unakabiliwa na misukosuko lukuki ikiwa ni pamoja na kushuka kwa thamani ya naira na kuzorota kwa uchumi kutokana na janga la UVIKO-19.

Wafanyabiashara katika hali ngumu

Wamiliki wa biashara ndogondogo wanahofia kupata hasara kutokana na mapato yao kupungua wakati sheria hiyo mpya itakapoanza kutekelezwa, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wanategemea mno mauzo yanayofanyika kwa pesa taslimu pekee.

Mfanyabiashara wa Lagos Lukman Lasisi ameiambia DW kuwa mzunguuko mdogo wa pesa husababisha kuzorota kwa masoko. Kwa miaka 12 iliyopita, Lasisi amekuwa akiuza nguo za wanawake katika soko moja lenye shughuli nyingi zaidi mjini Lagos, na anahofia kwamba biashara yake itadorora au kufilisika kabisa, huku Wanigeria matajiri ambao tayari wanatumia benki za kidijitali watalindwa kutokana na tatizo hilo.

TV Standbild | Flourish Chukwurah berichtet aus Abuja
Flourish Chukwurah, Ripota wa DW nchini Nigeria aliyeripoti taarifa hiiPicha: DW

Wafanyabiashara wataruhusiwa kutoa hadi naira milioni 5 kwa wiki ikiwa ni naira milioni 4.5 zaidi ukilinganisha na watu binafsi. Hata hivyo, muda umebaki mchache wa uhalali wa noti za zamani za naira 200, 500 na 1,000, ambazo hazitakubaliwa tena kama zabuni halali kuanzia Januari 31, 2023.

Katika jaribio la kurahisisha hali hii ya mpito, noti mpya na za zamani zote kwa sasa bado zipo kwenye mzunguko. Lakini Wanaigeria wenyewe wanasema noti hizo mpya zimekuwa adimu kadiri muda wa mwisho wa matumizi ya noti za zamani unavyokaribia. DW haikuweza kupata noti mpya ya naira katika benki nyingi na hata mashine za ATM za mjini Lagos.

Soma zaidi: Nigeria na Ghana zashindana kuanzisha sarafu za kidijitali

Afrika Cholera Nigeria Wasser in den Gassen
Kibanda cha mfanyabiashara mjini Abuja nchinin NigeriaPicha: Gbemiga Olamikan/AP/picture alliance

Baadhi ya wamiliki wa biashara wamekataa pia kupokea noti hizo mpya kutoka kwa wateja wao, wakidai kuwa muundo wake unarahisisha vitendo vya kughushi. Mwanamke mmoja mjini Lagos ameimbia DW kuwa mara ya kwanza alipopewa noti ya naira hakuamini kama ilikuwa ya kweli:

" Binafsi siipendi kabisa kwa sababu inaonekana ni feki, kama ghushi. Unajua, mara ya kwanza nilipopewa noti ya naira 1,000 nilisema: Hapana, pesa hizi ni bandia, itakuwa ni bandia. Lakini hapana, kumbe ni noti mpya ya naira. Sikuwa na habari nayo."

Je, kupunguza mzunguuko wa pesa kutaleta uthabiti wa kiuchumi?

Frankreich Paris | Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria, Muhammadu BuhariPicha: JULIEN DE ROSA/AFP/Getty Images

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, amesema muundo mpya wa naira una lengo la kupambana na mtiririko haramu wa fedha na ufisadi, na kuongeza thamani ya sarafu hiyo.

Wakati huo huo, gavana wa Benki Kuu ya Nigeria, Godwin Emefiele, anasema vikwazo vya utoaji fedha pia vitaruhusu benki kuu ya CBN kushirikiana kwa ukaribu zaidi na Tume ya Taifa ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha ili kukabiliana na miamala haramu.

Hatimaye, hatua zote mbili ni sehemu ya jitihada za Benki kuu ya Nigeria CBN za kuleta utulivu wa kiuchumi na kuufanya kuwa wa kidijitali.

Mwanauchumi Martha Sembe ameiambia DW kuwa hali hii imekuwa ikishuhudiwa kote duniani na ni jambo la kawaida. Nigeria imeendelea kupambana na viwango vya juu vya mfumuko wa bei kwa mwaka mzima, kuanzia asilimia 15.6 mwezi Januari hadi asilimia 21.5 mwezi Novemba.

Lakini Bi Sembe anasema ingawa hatua za CBN zilipokelewa vyema kwa ujumla na wanauchumi, kuna uwezekano zimetekelezwa katika wakati mbaya na kwa haraka mno, na hivyo kuwaacha wafanyabiashara wadogowadogo na familia zao wakilazimika kuubeba mzigo huo.

Soma zaidi:Madaktari Nigeria warejea kazini baada ya mgomo wa miezi 2 

Bi Sembe ameendelea kuwa baada ya kuhimili mfumuko wa bei kwa mwaka mzima, pamoja na gharama kubwa za chakula na nishati, jambo ambalo Wanigeria wanatakiwa kuwa na wasiwasi nalo ni kukusanyika katika ofisi za benki ili kubadilisha noti za naira.

Rekodi ya kiuchumi ya Buhari yazingatiwa kabla ya uchaguzi

Nigeria Änderung der Wähung Naira
Naira: Sarafu ya NigeriaPicha: Ubale Musa/DW

Katika kipindi chote cha miaka minane na mihula miwili madarakani, Buhari aliahidi mara kwa mara kufufua uchumi wa Nigeria. Hata hivyo, kinyume chake kimetokea: kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, uchumi wa nchi hiyo ulikua kwa kusuasua kiasi kwamba Mnigeria wa kawaida alizidi kuwa maskini kwa kuzingatia mfumuko wa bei.

Kuanzia 2015 hadi 2022, deni la umma la Nigeria liliongezeka kutoka takriban naira trilioni 12.6 hadi naira trilioni 44. Kwa sasa serikali inadaiwa na benki kuu jumla ya naira trilioni 22.

Soma zaidi: Athari kiuchumi kwa Afrika kufuatia mzozo wa Ukraine

Mwanauchumi Kola Ayeye amesema serikali inapaswa kushughulishwa zaidi na kulipa deni lake kuliko kuwabebesha watu wa kawaida mzigo wa hatua kali za kiuchumi. Ayeye ameongeza kuwa, deni hilo la serikali sio tu kubwa bali pia ni kinyume cha sheria na limechangia kushuka kwa thamani ya sarafu. Amesema tatizo hilo linahitaji kushughulikiwa.

Raia wa Nigeria watapiga kura Februari 25 katika uchaguzi mkuu unaosubiriwa kwa hamu ambao pia utashuhudia rais mpya akiingia madarakani. Hali ya uchumi wa Nigeria inatarajiwa kusalia kuwa suala kuu kwa wapiga kura.