1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Navalny hatimaye asafirishwa Ujerumani

22 Agosti 2020

Ndege iliyombeba kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny ambaye amepoteza fahamu baada ya kudaiwa kutiliwa sumu kwenye chai, imeondoka Urusi na kuelekea hospitali moja Ujerumani.

https://p.dw.com/p/3hKdU
Russland | Alexei Navalny am Flughafen Richtung nach Deutschland
Picha: Reuters/A. Malgavko

Haya yanakuja baada ya mvutano wa muda mrefu kuhusiana na hali yake na matibabu anayopokea. 

Ndege hiyo imeonekana ikipaa kutoka uwanja wa ndege wa Siberia katika mji wa Omsk muda mfupi baada ya saa mbili asubuhi kwa saa za Urusi. Navalny ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Vladimir Putin na ambaye pia huchunguza visa vya ufisadi alilazwa chumba cha wagonjwa mahututi mjini Omsk hapo juzi. Wafuasi wake wanaamini kwamba chai aliyokunwa katika uwanja wa ndege kabla ya safari yake ilikuwa imetiwa sumu na kwamba serikali ya Urusi ndiyo iliyohusika na pia imehusika katika ajizi ya kumkubalia asafirishwe Ujerumani.

Russland | Alexei Navalny am Flughafen Richtung nach Deutschland
Ambyulensi iliyombeba Navalny kumpeleka uwanja wa ndegePicha: AFP/D. Dilkoff

Kremlin imekanusha kuchelewa kusafirishwa kwa Navalny ilikuwa ni sababu za kisiasa

Inaarifiwa kwamba madaktari wa Ujerumani walipowasili kwa ndege iliyokuwa na vifaa vya hali ya juu vya matibabu kutokana na ombi la familia yake, madaktari waliokuwa wanamshughulikia huko Urusi walisema kwamba alikuwa mgonjwa mno na hakuweza kusafiri. Wafuasi wake wanasema hiyo ilikuwa mbinu ya serikali kuhakikisha kwamba anawekwa nchini humo kwa kipindi kirefu hadi pale sumu aliyokuwa amekunywa ipotee mwilini.

Madaktari hao walikubali kuondolewa hospitalini humo kwa mwanasiasa huyo pale shirika linalofadhili usafiri wa Navalny kusema kuwa madaktari wa Ujerumani wamemchunguza na kuona kwamba yuko katika hali anayoweza kusafirishwa. Baada ya hapo daktari mkuu wa hospitali hiyo ya Omsk Anatoly Kalinichenko akawaambia waandishi wa habari kwamba hali yake imeimarika na kwamba familia yake imeamua asafirishwe licha ya hatari zilizoko.

IKulu ya Kremlin imekanusha kwamba ajizi hiyo ya kusafirishwa kwa Navalny ilikuwa ni mbinu ya kisiasa huku msemaji Dmitry Peskov akisema ulikuwa ni uamuzi wa kimatibabu.

Navalny alikuwa mgonjwa ghafla kwenye ndege na akapoteza fahamu

Siku ya Ijumaa viongozi wa Ujerumani na Ufaransa walisema kuwa nchi hizo mbili ziko tayari kuisaidia familia ya Navalny kwa njia yoyote ile na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusiana na tukio hilo.

Russland Omsk Yulia  Navalny vor Krankenhaus
Mke wa Navalny Yulia Navalny akizungumza na waandishi wa habariPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Sofiychuk

Navalny alifanya kampeni katika uchaguzi wa mwaka 2018 ili kushindana na Putin ila hakupewa nafasi ya kushiriki uchaguzi huo. Kutokea wakati huo amekuwa akiwanadi wagombea wa upinzani katika chaguzi za kieneo nchini humo.

Mwanasiasa huyo alikuwa mgonjwa ghafla alipokuwa kwenye ndege kurudi mjini Moscow kutoka Siberia na alikiimbizwa hospitali baada ya ndege kutua ghafla. Timu yake ilifanya mpango wa kumuondoa na kumpeleka katika hospitali ya Charite mjini Berlin. Hospitali hiyo ina historia ya kuwatibu wapinzani na viongozi maarufu kutoka nchi za nje.