1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mzozo wa Mashariki ya kati wagubika mkutano wa G7 Tokyo

Amina Mjahid
7 Novemba 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ametoa wito kwa kundi la nchi tajiri zaidi duniani la G7, kuzungumza kwa sauti moja kuhusu mzozo wa Israel na Hamas.

https://p.dw.com/p/4YWdM
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa ziarani Israel
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Katika ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa kundi la G7 unaofanyika mjini Tokyo Japan, Blinken amesema huu ni wakati muhimu wa kundi hilo kuungana na kuzungumza kwa kauli moja.

Ameyasema hayo wakati jeshi la Israel  likiendelea na mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, wakati wanamgambo wa Hamas waliposhambulia kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,400, huku Gaza ikiripoti vifo vya zaidi ya watu 10,000 wakiwemo watoto zaidi ya 4000 na watu milioni moja wakipoteza makaazi yao.

Baada ya kuwasili mjini Tokyo akitokea Mashariki ya kati, Blinken atawafahamisha mawaziri wenzake kuhusu ziara yake na alikofikia kuhusu mchakato wa kufikisha misaada zaidi Gaza na juhudi za kudhibiti mgogoro huo.

Katika ziara yake Uturuki Blinken, alisema Marekani inafanya kazi usiku na mchana kuongeza msaada kwa raia wa Gaza wanaothirika pakubwa na vita hivyo, bila ya kutoa maelezo zaidi.

Marekani bado haijaridhia wito wa kusitisha mapigano ya Hamas na Israel

Marekani ambaye ni mshirika muhimu wa Israel imekataa kutoa wito wakusitishwa kwa mapigano, ikisisitiza kwamba Israel ina haki ya kujilinda lakini imetaka tu vita visimamishwe kwa muda, ili kutoa nafasi ya misaada hiyo kuwafikia walengwa.

Shambulizi la Israel lilivyouharibu Ukanda wa Gaza
Sehemu ya Ukanda wa Gaza ilivyoharibiwa na makombora ya IsraelPicha: Bashar Taleb/APA/ZUMa/picture alliance

Hata hivyo Ufaransa inayowakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje Catherine Colonna, imesema inagelipenda mkutano huo wa G7 ujadili umuhimu wa kujibu mahitaji ya watu wa Gaza na kuheshimiwa kwa sheria ya kimataifa. Mwenzake wa Japan Yoko Kamikawa, amesema anahitaji uwepo wa majadiliano ya wazi na ya kina kuhusiana na suala hilo.

Suala lengine muhimu kabisa linalozungumziwa katika mkutano huo wa siku mbili ni mgogoro pia au vita kati ya Urusi na Ukraine. Waziri wa nchi za nje wa taifa hilo Dmytro Kuleba anatarajiwa kuzungumza kupitia njia ya vidio katika mkutano huo wa kundi la G7 ikiwa ni pamoja na Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya. 

Waziri mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema G7 itajadili njia za Ukraine kujilinda hasa wakati huu wa kipindi cha baridi.

Masuala ya Asia ya Kati pia yapo katika ajaenda ya G7

Kingine kitakacokuwa ndani ya ajenda ya mkutano huo ni ushirikiano zaidi wa mahusiano na Asia ya Kati huku Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo pia wakitarajiwa kuzungumza kwa njia ya vidio.

Japan | Baerbock katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G7 Tokyo
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalean Baerbock akiwa na mwenzake wa Japan Yoko KamikawaPicha: Thomas Koehler/photothek/picture alliance

Kando na hilo Waziri wa mambo ya nchi za nje na wa ulinziwa Japan na Uingereza wamekutana pembezoni mwa mkutano huo na kukubaliana kuongeza ushirikiano wao wa kijeshi, chini ya makubaliano mapya ya kiusalama yanayoridhia wanajeshi kuingia katika sehemu hizo mbili kushiriki mafunzo ya pamoja.

Nchi hizo mbili zimeongeza ushirikiano wao katika miaka ya hivi karibuni kufuatia ushawishi wa China.

Vyanzo: afp/ap/reuters