1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege

Admin.WagnerD25 Machi 2015

Watu wote nchini Ujerumani wanafuatilia kwa undani wote kila habari juu ya maafa yaliyosababishwa na ajali ya ndege. Wengi wanahisi wangeliweza kuwamo katika ndege hiyo.

https://p.dw.com/p/1ExGA

Kusafiri kwa ndege limekuwa jambo la kawaida kwa watu wengi barani Ulaya.Siyo ibura tena kupanda ndege kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Katika zama za leo siyo lazima mtu awe na kipato kikubwa ili aweze kukata tikiti ya ndege na kwenda kufanya shughuli zake iwe ndani au nje ya nchi.

Felix Steiner
Mwandishi wa DW Felix SteinerPicha: DW/M.Müller

Na hiyo ndiyo sababu kwamba habari juu ya kuanguka ndege ya abiria ya Ujerumani ya shirika la Germanwings hapo jana kusini mwa Ufaransa zimewashtua sana watu nchini Ujerumani.

Ni nadra ndege kuanguka barani Ulaya

Kuanguka ndege barani Ulaya ni nadra sana.Na inakuwa nadra zaidi ikiwa ndege inayoanguka ni ya Ujerumani. Watu 150 wamekufa katika ajali iliyotokea jana wakati ndege yao ya shirika la Ujerumani ilipokuwa angani kutoka Uhispania kuelekea Ujerumani.

Watoto wa shule 16 na walimu wao wawili walikuwa miongoni mwa waliokufa. Habari juu ya ajali ya ndege hiyo zimewagusa Wajerumani wote, na wote wanaombeleza. Kwa sababu yeyote angeliweza kuwamo katika ndege iliyoanguka.

Sasa jambo la kipaumbele ni kuwafariji ndugu na jamaa waliofikwa na msiba sambamba na kufanya juhudi ili kukibainisha kile kilichosababisha ajali iliyotokea. Watu wataendelea kupanda ndege licha ya ajali hiyo. Yumkini watu hapa nchini Ujerumani watajiuliza mara mbili kabla ya kupanda ndege ya Germanwings yaani shirika la ndege iliyoanguka.

Usafiri wa anga bado ni salama

Ni kweli watu watakuwa na mashaka mashaka kwa muda fulani lakini hatimaye mambo yatarejea katika hali ya kawaida. Imebainishwa kwamba njia nyingine za usafiri zinaweza kuwa za hatari kubwa zaidi kuliko kupanda ndege.

Ingawa ninachokisema kinaweza kuonekana kuwa kebehi kwa wale waliowapoteza ndugu zao kutokana na ajali, ukweli ni kwamba usafiri wa ndege bado ni wa salama kabisa. Wakati wote ajali ya ndege inasababisha mshtuko mkubwa.Lakini hakuna tofauti katika ajali ya ndege na ya barabarani.

Idadi ya watu wanaokufa kutokana na ajali za barabarani, kila mwezi nchini Ujerumani ni mara mbili ya ile ya watu waliokufa kutokana na ajali ya jana. Hata hivyo lengo sasa ni kuufanya usafiri wa anga uwe salama zaidi. Wadau wote,wahandisi, mafundi, na wanaotengeza ndege wanapaswa kulitilia hilo maanani.

Mwandishi: Felix Steiner

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Mohammed Khelef