1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mandela, mtu wa kufikirika

6 Desemba 2013

Vyombo vya habari na wanasiasa dunia kote wanaendelea kushindana katika kuonyesha heshima zao kwa Nelson Mandela, ambaye yeye mwenyewe hakupenda kuchukuliwa ni kama mungu

https://p.dw.com/p/1AU57
Picha: Reuters/Suzanne Plunkett

Hilo ni mojawapo ya mambo ambayo yalimfanya kuwa mtu wa kipekee, jinsi anavyosema Mkuu wa Idhaa za Kiafrika katika DW Claus Stäcker.

Nelson Mandela hakuwa mtakatifu, hata ingawa hivyo ndivyo vyomvo vya habari vinavyomwelezea. Kila kichwa cha habari kinamfanya aonekane ni kama mtu aliyefanya maajabu na hasa kuonekana kama kuiabudu sabamu. Baadhi ya watu waliokutana naye wanasema walijihisi kuwa wa kipekee, na “Muujiza wa Madiba” ulijitokeza kila mara Afrika Kusini ilipohitaji muujiza. Mandela mwenyewe hakupenda kuabudiwa. Alikuwa alikubali tu shingo upande barabara, shule na taasisi kuitwa jina lake, kuruhusu sanamu za shaba na majumba ya makumbusho ya Mandela kujengwa, mtindo ambao bila shaka utaendelea kukua.

Mkuu wa idhaa ya za Afrika wa Deutsche Welle Claus Stäcker
Mkuu wa idhaa za Afrika za Deutsche Welle Claus StäckerPicha: DW

Kila mara alitaja mifano ya mafanikio ya pamoja ya harakati za upinzani, zilizofaynwa na vigogo waliomtangulia katika vita dhidi ya udhalimu na kwa wanaharakati wenzake kama vile Mahatma Gandhi, Albert Luthuli au rafiki yake na mwenzake katika vita Oliver Tambo ambaye leo bila kustahili anasimama katika kivuli cha Mandela. Wakati mfungwa huyo nambari 46664 alipoachiliwa huru baada ya miaka 27 gerezani, alikuwa amejitengenezea jina, kielelezo cha ulimwengu, chanzo cha matumaini na matamanio ambayo hakuna binadamu yeyote angeweza kuyatimiza peke yake.

Hakukukosa dosari

Nani angejaribu kukwaruza sifa ya mwanamme kama yeye? Orodha ya vituko vyake vya ujana, wanawe aliozaa nje ya ndoa? Nani angeweza kutaja udhaifu wake kwa wanawake, wanamitindo, nyita wa miziki na waandishi habari wa kike ambao walitaniana kwa njia isiyokubalika kisiasa wakati tayari alikuwa kiongozi wa taifa aliyeheshimika?

Nani angezungumzia mashambulizi aliyopanga wakati alikuwa kiongozi wa tawi la kijeshi la ANC Umkhonto we Sizwe (Mkuki wa Taifa?) na nani angekosoa namna alivyokasirika kila mara au kupuzilia mbali maoni ya wenzake isipokuwa yake tu? Leo, wafungwa wenzake na wafanyakazi wanaweza sasa kutabasamu kuhusu mambo ya aina hiyo.

Rekodi yake kama kiongozi wa serikali kuanzia mwaka wa 1994 hadi 1999 pia siyo safi kabisa. Miaka hiyo ilikuwa ya vitendo na ukimya wa kisiasa. Maamuzi yaliyochelewa hayakuchukuliwa, masuala ya kila siku yaliachiwa wengine. Wakati akiwachagua wmarafiki zake wa kisiasa uamuzi wake haukuwa kila mara mzuri. Mjukuu mmoja wa Mandela alipewa jina la aliyekuwa dikteta wa Libya Muammar Gaddafi.

Lakini Mandela anaweza kusamehewa kutokana na maüungufu haya kwa sababu, licha ya kila kitu, alipata mafanikio kuwaliko binaadamu wengine wengi. Kipindi chake kirefu gerezani kilitekeleza jukumu muhimu hapa. Hakikumvunja, bali kilimjenga. Kisiwa cha Robben kilikuwa kama “chuo kikuu cha maisha” kwake, Mandela aliwahi kusema wakati mmoja.alijifunza nidhamu huko, katik mazungumzo na walinzi wake alijifunza unyenyekevu, uvumilivu na subira. Hasira yake ya ujana iliyeyuka, akapata hekima ya ukomavu. Alipoachiliwa huru hakuwa na hasira, na hakuwa na fikira za kimapinduzi. Hicho ndicho ambacho baadhi ya wapiganaji wake wa uhuru walitofautiana naye, ijapokuwa siyo hadharani. Walitaka vuguvugu kamili la mapinduzi.

Nelson Mandela na mkewe wa tatu Graca Machel
Madiba alijulikana kama mtu mcheshi na mnyenyekevuPicha: Reuters

Heshima kwa wote

Mandela alitaka maridhiano, kwa vyovyote vile. Mabadiliko yake mwenyewe yalikuwa nguvu zake, uwezo wa kuondokana na mchakato wa mawazo ya kiitikadi na kuona picha kubwa, na kutambua kwamba wale wanaofikiria vingine siyo maadui, uwezo wa kusikiza, kusambaza ujumbe wa maridhiano karibu kufikia kiwango cha kukisaliti kile alichokiamini.

Ni kwa njia hii pekee ambapo angeweza kutumiwa kama kielelezo kwa Waafrika kusini weusi na weupe, wakomunisti, wajasiria mali, wakristo na waislamu. Alikuwa mmishionari, mhubiri wa upendo na umoja. Ni lazima atajwe kwa sifa sawa kama Mahatma Gandhi, Dalai Lama au Martin Luther King. Mandela aliandika sura ya historia ya maisha yake, hata Barack Obama alisema hangeweza kuwa rais wa Marekani bila Mandela kama kielelezo chake.

Kuhudumia jamii

Wakati Mandela alipoachiliwa huru kutoka gerezani mwaka wa 1990, ulimwengu wa zama wa enzi ya Vita Baridi ulikuwa unaporomoka. Mandela alisimama katika njia panda na akauchukua mkondo unaofaa. Angeweza kucheza na moto kwa urahisi, kutafuta kulipiza kisasi, au kushindwa. Angejificha kutoka maisha ya umma, kama tu wenzake, waliopata mamilioni. Ndoa mbili zilivunjika kwa sababu ya mazingira ya kisiasa. Wanawe wa kiume wakafa mapema kabla yake. Ilikuwa tu wakati alipokuwa na umri wa miaka 80 alipokutana na mkewe wa tatu Graca Machel, ndipo akapata tena upendo, ushirikiano na maisha ya kibinafsi.

Nelson Mandela ARCHIVBILD
Nelson Mandela na mkewe wa tatu Graca MachelPicha: picture-alliance/dpa

Changamoto haikumwacha akiwa na machungu, lwa sababu alichukulia maisha yake kuwa yasiyo na umuhimu kuliko jambo alilolenga kulitimiza. Aliihudumia jamii kwa unyenyekevu, na uwajibikaji, na nia ya kujitoa mhanga, sifa ambazo sasa ni nadra kupatikana. Ulimwengu katika miaka ya 1990, na sifa yake kubwa vilimpa fursa ya kihistoria. Kinyume na wengine, akaichukua fursa hiyo. Alijitwika mzigo huo na kuielimisha nchi, kuwaongoza watu wake na kuubadilisha ulimwengu.

Sasa warithi wake wanaonekana wadogo sana na wenye kusikitisha. Mapambano yao ya madaraka sasa huenda yakaendeshwa hata vibaya zaidi kuliko siku za nyuma. Ni aibu kubwa namna jamaa zake walivyozozania sifa yake akiwa hospitalini. Mandela hakuwa mtakatifu, lakini mtu mwenye uwezo wake na mapungufu, yaliyotokana na mazingira yake. Itakuwa vigumu kupata mtu mwenye umuhimu kama wake. Angeongezwa uhai kidogo tu, Mandela kila siku angepata mafanikio ya makubwa. Siyo tu barani Afrika, lakini pia Berlin, Jerusalem au Moscow.

Mwandishi: Claus Stäcker/Bruce Amani

Mhariri: Sekione Kitojo