1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Historische Chance

Klaus Jansen16 Septemba 2014

Alhamisi wiki hii wakaazi wa Scotland watapiga kura kuamua juu ya uhuru wao kutoka Uingereza. Utofauti wa kitamaduni na kisiasa wa Wascot unathibitisha vyema jaribio hilo, anasema Daniel Scheschkewitz. katika maoni yake.

https://p.dw.com/p/1DClB
Kiongozi wa kampeni ya "Ndiyo" Alex Salmond.
Kiongozi wa kampeni ya "Ndiyo" Alex Salmond.Picha: Getty Images/J.J Mitchell

Kwa miaka kadhaa watu wengi nchini Ujerumani na Ulaya ya Kati waliichukulia Scotland kama mkoa wa mbali kaskazini mwa Uingereza, ambako mvua hunyesha kwa wingi, na wanaume wake hupendelea kuvaa sketi, kunywa Whisky, na kwamba uchoyo wao wa kimethali ulikuwa ni zaidi ya utani. Lakini kwa karne nyingi hadi mwaka 1707, Scotland ilikuwa nchi huru iliojitegemea na kujivunia, ambayo nafasi ya historia yake ilifutwa baada ya kuungana na Uingereza.

Ikiwa Wascot wataamua kupiga kura ya Ndiyo, nchi hiyo itarudi kwenye ramani ya Ulaya baadaye, na matokeo yake ni kwamba Uingereza inaweza kujikuta katika wakati mgumu kutokana na madhara ya kisiasa na kiuchumi ambayo bado hayajulikana kiwango chake. Je, hii itakuwa hatua ya kurudi nyuma? Au ni kosa la wakati litakalopelekea kuanza kuundwa kwa majimbo madogo huru katika Ulaya ya sasa isiyo na mipaka? Nadhani siyo.

Scotland ilikuwa tofauti siku zote
Mara zote Scotland ilikuwa tofauti na jirani yake wa kusini England, na Waroma walilitambua hilo. Ni kwa sababu hii Mfalme Hadrian alijenga ukuta kutenganisha mpaka kati ya Scotland na England ili kuwadhibiti Wascot katika karne ya pili. Ilikuwa ni baada ya muungano wa familia za kifalme mwaka 1603, na jaribio lililoshindwa la Wascot kutaka kujenga himaya ya kibaishara, ndipo walikubaliana mwaka 1707 juu ya kuunganisha bunge lao na lile la England.

England na Scotland ziliungana na Wales iliyokuwa na utajiri wa makaa ya mawe, na kuunganisha rasilimali za mataifa hayo kuufanya muungano wa mataifa hayo - yaani Uingereza, kuwa taifa kubwa na lililostawi kisiasa na kiuchumi. Tofauti za kisiasa na kitamaduni zilitoweka baada ya muungano huo, lakini zilikuja kujitokeza tena katika nusu ya pili ya karne ya 20 kwa nguvu kubwa.

DW Deutsches Programm Daniel Scheschkewitz
Daniel Scheschkewitz.Picha: DW

Muungano na England umepitwa na wakati
Margret Thatcher aliiondolea Uingereza viwanda na kuikarabati bajeti goigoi ya nchi hiyo kwa kutumia mafuta yanayochimbwa katika bahari ya kaskazini ya Scotland. Wascot walilichukulia hilo kwanza kwa ufahari, lakini baada ya kugundua kuwa sehemu kubwa ya wakaazi wa mji mkuu wa mafuta wa Aberdeen, ambao kwao unapaswa kuwa kama Abu Dhabi ya Scotlanda, wanaishi katika hali ya umaskini, walianza kuwa na mashaka.

Mashaka hayo yaliimarishwa na hisia kwamba wahafidhina walikuwa dhidi ya Scotland, hata wakati Wascot walichagua mwakilishi mhafidhina katika bunge la Uingereza katika chaguzi zote tangu mwaka 1997. Zilikuwa hisia hizo zilizojenga mazingira ya kukua na kuimarika kwa chama cha wazalendo cha SNP katika miaka ya 1990, chama ambacho kinaongoza kampeni ya uhuru wa Scotland.

Kuzaliwa upya kwa Scotland
Kwa miongo kadhaa Scotland imekuwa ikushuhudia kuzaliwa upya kwa utamaduni. Tamasha la utamaduni la Edinburg ni moja kati ya matamasha yanayotembelewa zaidi na linalowakutanisha wasanii wabunifu zaidi duniani. Muziki wa Scotland ni maarufu na unapendwa sana duniani. Vyuo vikuu vya Scotland ni vya bure na vinapokea wanafunzi kutoka duniani kote. Wanasayansi wa Scotland wanatambulika hata nje ya mipaka ya uingereza.

Wakati nchini England elimu inazidi kuwa haki ya matajiri wachache na shule nyingi binafsi zinazidi kuchipukia, elimu ya juu imeendelea kuwa nafuu kwa watu wote nchini Scotland, na inavutia wahamiaji wengi wenye ujuzi wa juu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Huko chama cha UKIP kinachopinga uhamiaji hakina maana yoyote, wakati huko England sera zake za chuki dhidi ya wageni na kupinga uhamiaji zimekipatia mafanikio katika uchaguzi.

Manufaa kwa Umoja wa Ulaya
Scotland huru ingeomba mara moja kujiunga na Umoja wa Ulaya, ambao hauwezi kuikatalia. Tofauti na hii, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ametangaza kura ya maoni juu ya kuamua mustakabali wa Uingereza katika umoja huo ifikapa mwaka 2017. Hivyo anaweza kuwa amechelewa. Ishara zinaonyesha nafasi ya 50 kwa 50 kwa Scotland kutumia fursa hii ya kihistoria, na kupitia zoezi hilo la kidemokrasia kurejeshea taifa lao kwa njia za amani.

Hata kiuchumi Wascot hawapaswi kuwa na hofu. Licha ya hifadhi ndogo ya mafuta walionayo, serikali ya Scotland inaweza kutumia rasilimali zake luluki kuwa ya nishati jadidifu na kuwa miongoni mwa mataifa 20 yaliyostawi zaidi kiuchumi duniani. Umoja wa Ulaya unaweza kunufaika na taifa hilo jipya.

Mmwandishi: Daniel Scheschkewitz
Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Mohammed Khelef