1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali: Rais wa zamani apelekwa Abu Dhabi kwa matibabu

Zainab Aziz Mhariri: John Juma
6 Septemba 2020

Afya ya kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 75 imekuwa sio nzuri na kusababisha kulazwa hospitalini mara alipoachiwa baada ya kuzuiliwa na watawala wa kijeshi kwa siku 10.

https://p.dw.com/p/3i3bK
Mali Ibrahim Boubacar Keita
Picha: AFP/L. Marin

Duru za kidiplomasia nchini Mali zimesema Rais wa Mali aliyeondolewa madarakani kwenye mapinduzi ya kijeshi mnamo mwezi Agosti, Ibrahim Boubacar Keita,alisafirishwa mwishoni mwa wiki na kupelekwa Falme za Kiarabu kwenda kupata matibabu.

Kiongozi huyo wa Mali aliyeondolewa madarakani ameandamana na mkewe, Aminata Maiga Keita, msaidizi, madaktari wawili na maafisa wanne wa usalama, hayo ni kwa mujibu wa Mamadou Camara mkuu wa zamani wa wafanyikazi wa Bobackar Keita aliyeliambia shirika la habari la Reuters kuwa Keita aliondoka kutoka mjini Bamako Jumamosi jioni ndani ya ndege iliyokodishwa na Falme za Kiarabu kufuatia ombi kutoka kwa mamlaka ya Mali na Keita mwenyewe, ili aweze kwenda kutibiwa katika hospitali ya kijeshi katika mji wa Abu Dhabi. Camara amesema hiyo ni ziara ya matibabu itakayochukua muda wa kati ya siku 10 hadi 15.

Kiongozi huyo wa zamani ameondoka nchini Mali wakati ambapo mazungumzo juu ya kurudishwa kwa utawala wa kiraia kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita yameanza kwa mivutano.

Wanajeshi wa Ufaransa wanaotumikia operesheni ya Barkhane
Wanajeshi wa Ufaransa wanaotumikia operesheni ya Barkhane Picha: picture-alliance/dpa/P. De Poulpiquet

Wakati huo huo wanajeshi wawili wa Ufaransa wameuawa katika mkoa wa Tessalit kaskazini mwa Mali. Maafisa hao walihudumu kwenye kikosi kinachoendesha operesheni inayoitwa Barkhane ya kupambana ugaidi katika eneo linalokumbwa na machafuko la Sahel. Kulingana na taarifa ya jeshi la Ufaransa maafisa hao walikufa baada ya gari lao kugonga kifaa cha kulipuka.

Kulingana na wizara ya ulinzi ya Ufaransa nhi hiyo ina zaidi ya wanajeshi 6,500 wanaotumika kwenye operesheni za nje ya nchi na zaidi ya askari 5,000 ni sehemu ya wanajeshi wanaotumika katika operesheni hiyo ya Barkhane.

Ufaransa inashiriki katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel. Baadhi ya makundi hayo yanashirikiana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS pamoja na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.

Chanzo:/AP/RTRE