1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron ampiku Le Pen na kupata muhula wa pili

Bruce Amani
25 Aprili 2022

Rais Emmanuel Macron anaanza sasa juhudi za kuliunganisha taifa lililogawika pakubwa baada ya kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili katika duru ya pili ya uchaguzi Jumapili dhidi ya mpinzani wake Marine Le Pen.

https://p.dw.com/p/4AND0
Frankreich Präsidentschaftswahl Wahlsieger Macron
Picha: BENOIT TESSIER/REUTERS

Macron, wa siasa za mrengo wa wastani alishinda kwa asilimia 58.6 ya kura dhidi ya Le Pen aliyepata asilimia 41.45, kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Soma pia: Wafaransa wapiga kura katika duru ya pili ya urais

Macron ndiye rais wa kwanza wa Ufaransa katika miongo miwili kushinda muhula wa pili, lakini ushindi wake huu dhidi ya mpinzani wake wa siasa kali za mrengo wa kulia umekuwa mwembamba Zaidi kuliko kinyang'anyiro cha mwaka mwaka wa 2017 baina yao, wakati alishinda kwa asilimia 66.1 dhidi ya asilimia 33.9. Katika mwaka wa 2002, Jacque Chirac alichaguliwa kwa muhula wa pili.

Mafanikio hayo ya kihistoria kwa siasa za mrengo wa kulia yalitia doa sherehe za kiongozi huyo jana usiku. Akiwahutubia wafuasi wake mbele ya mnara wa Eiffel, aliapa kuziba mipasuko katika taifa lililogawiak pakubwa "Enzi hii mpya haitakuwa mwendelezo wa miaka mitano iliyopita, lakini uvumbuzi wa pamoja wa mbinu iliyorekebishwa kwa ajili ya miaka mitano bora, ya huduma kwa nchi yetu na kwa vijana wetu." Rais huyo mwenye umri wa miaka 44 ataanza muhula wake wa pili na changamoto ya uchaguzi wa bunge mwezi Juni, ambapo itakuwa muhimu kupata wingi wa viti ili afanikishe malengo yake.

Präsidentschaftswahl in Frankreich, Stichwahl, Marine Le Pen
Le Pen sasa amegeukia uchaguzi wa bungePicha: Francois Mori/AP Photo/picture alliance

Mamia kadhaa ya waandamanaji kutoka makundi ya misimamo mikali ya mrengo wa kushoto yaliandamana mitaani katika katika baadhi ya miji ya Ufaransa kulalamikia kuchaguliwa tena Macron na matokeo ya Le Pen. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuitawanya mikusanyiko Paris na mji wa magharibi wa Rennes.

Kwenye hotuba yake Le Pen mwenye umri wa miaka 53 alikiri kushindwa akisema matokeo hayo ni ushindi kwao, na sasa ni wakati wa kuangazia uchaguzi wa bunge Juni.

Ushindi wa Macron ulisababisha ahueni kubwa sana barani Ulaya baada ya hofu kuwa urais wa Le Pen ungeliacha bara hilo katika hali mbaya kufuatia Brexit na kuondoka kutoka ulingo wa siasa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi auita ushindi wa Macron kuwa ni "habari njema kwa wote barani Ulaya” wakati Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema wapiga kura wa Ufaransa "wamepiga kura muhimu ya kuwa na Imani barani Ulaya”.

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema umoja huo sasa unaweza "kuitegemea Ufaransa kwa miaka mitano zaidi” wakati rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen pia amempongeza Macron akisema "anafuraha kuendeleza ushirikiano wao bora Zaidi”.

Soma pia: Macron aimarisha uongozi wake katika mjadala wa televisheni

Marekani imesema Ufaransa ni mshirika wa jadi na muhimu katika kushughulikia changamoto za ulimwengu. Rais Joe Biden amesema watashirikiana kwa karibu ikiwemo kuisaidia Ukraine, kutetea demokrasia, na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

AFP/DPA/AP/Reuters