1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa Wanyamapori Wanashangilia Uuzaji wa Meno ya Ndovu mwaka 2004

Shaaban M Shangama24 Novemba 2003
https://p.dw.com/p/CEI5
Karibuni katika makala nyingine ya Mtu na Mazingira kutoka Redio Deutsche Welle, Bonn, Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Ni Shaaban Mohamed nikiwatakia usikilizaji mzuri.
Mtaalamu wa hifadhi David Bradfield ana hadhithi ya kuvutia kutueleza, kuhusu ziara zake katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe. Akivalia kama mtalii, alikiuliza kikundi cha wauzaji wa vyombo vya sanaa mjini humo iwapo angeweza kununua pembe za tembo. " Nilipouliza iwapo wangeweza kuniuzia, mchuuzi moja alitoa magunia matatu ya meno ya ndovu yaliyochongwa kama vifaa vya sanaa na zawadi. Nilisema 'Siyo, sivutiwi'," anaeleza. Hii ni hali inayozikabili mamlaka za Malawi, mnamo mkesha wa kuuzwa tani 66 za meno ya ndovu katika nchi jirani za Botswana, Namibia na Afrika Kusini.
Katika mwezi wa Novemba mwaka jana, Mkataba wa Kimataifa wa Aina Zilizohatarika (CITES) kwa ufupi, ulipitisha uamuzi kwamba upigaji marufuku wa biashara ya meno ya ndovu, ungeweza kusitishwa mwakani kwa uuzaji wa mara moja wa shehena za nchi hizo tatu. Fedha zitakazopatikana zitatumiwa kustawisha hifadhi ya wanyamapori.
Hatahivyo, vikundi kadha vya wahifadhi vinaamini kwamba utaratibu wa kutosha wa kukagua uuzaji huo hauko - na matokeo yake yangeweza kusababisha furiko la ujangili ambalo limeshashuhudiwa nchini Malawi. Tanzania imeashiria pia kwamba inapendelea kuuza kadiri ya kilo 80,000 za shehena yake ya meno ya ndovu.
Mtaalamu mwingine wa hifadhi, Paul Taylor, anasema " Ni bora kabisa kupigwa marufuku. Ndiyo, fedha za kuendesha maeneo yanayolindwa ni muhimu. Lakini ni hatari mno. Mimi ninabisha moja kwa moja." Hata kama zinatangazwa sheria dhidi ya ujangili, matokeo yake ni machache mno. Katika kadhia ya karibu ya kustaajabisha, mwanamke mfanya biashara kutoka wilaya ya kusini Machinga, ambaye alikutiaka ana meno kumi ya tembo (yenye uzito wa kilo 127) alitozwa faini kadiri ya dolla 57 tu.
Kwa mujibu wa Jumuia ya Wanyamapori na Mazingira nchini Malawi (WESM) - yenye makao yake karibu na mji mkuu wa kibiashara Blantyre, inaigharimu serikali kadiri ya Dolla 4,700 kumshtaki mwanabiashara wa kike, Maria Akimu. Ni karibu mara mia faini aliyotakiwa alipe. Wakili katika Kituo cha Sera ya Mazingira na Utetezi nchini Malawi, Gracian Banda, ameajiriwa kuisaidia mamlaka ifungue upya kesi dhidi ya Akimu. "Kuna sababu njema za kudurusu kesi hii ... Sheria inasema ukikutikana na hatia ya kumiliki meno ya ndovu kinyume cha sheria, basi faini haitastahili kuwa chini ya thamani ya meno hayo. Huu ni msingi wa hoja yetu 'thamani ya kile kinachohusika"," anasema Gracian Banda.
Hatahivyo, anahofia athari za muda mrefu za uuzaji wa pembe za tembo mwakani. Utaratibu unahitajika kuhakikisha biashara huru," alisema Banda, akaongeza " Kuna haja pia ya ukaguzi, ili pembe za tembo haramu kutoka nchi nyingine hazigeuzwi halali. Kunahitajiwa ushrikiano zaidi baina ya polisi, maafisa wa kastamu na Interpol. (Interpol ni Shirika la Polisi wa Kimataifa dhidi ya makosa ya jinai, ambalo linasaidia vikosi vya polisi vya kitaifa kuwatia mbaroni wakosa. Makao yake yako nchini Ufaransa. Taylor anasikitishwa kwa kukosekana ushirikiano baina ya wakala mbali mbali za utekelezaji wa sheria nchini Malawi."Watumishi wa kastamu na wa wanyamapori hawafanyi kazi kama timu, na kusitishwa upigaji marufuku kungekuwa kiyama kwa nchi hiyo," anasema. Udhaifu huu wa ushirikiano - pamoja na mipaka isiyolindwa barabara na viwango vya juu vya umasikini, yote haya yameifanya Malawi kuwa kitovu cha biashara haramu ya meno ya ndovu.
Kwa mujibu wa Bw. Bradfield , ambaye yuko Malawi kwa mradi unaogharimiwa na Jumuiya ya Bustani za Wanyama mjini Frankfurt, jumla ya ndovu katika mbuga za Namizimu na Phirilongwe kusini mwa Malawi imepukngua kwa kadiri kubwa mnamo miaka michache iliyopita. "Angalia, miaka 15 iliyopita kulikuweko kadiri ya ndovu 200 katika hifadhi ya msitu ya Phirilongwe - lakini sasa wamebaki kadiri ya 30 tu. Wenyeji wanawaua ndovu hawa, na kuzurua na meno ya tembo mchana."
Naibu Mkurugenzi wa Mbuga za Wanyama na Wanyamapori, ambaye anahusika na utafiti na mipango, Roy Bhima, anasema mbuga za taifa za Kasungu, Vwaza na Nyika ni shabaha ya majangili kutoka nchi jirani.
"Hali ya mambo inatia wasiwasi zaidi katika mbuga ya taifa ya Kasungu...moja kati ya mbuga kubwa kabisa nchini, ambayo iliwahi kuwa pepo ya wanyamapori. Kuhesabiwa ndovu hivi karibuni katika mbuga ya Kasungu, mwaka huu, kumeonyesha kadiri ya ndovu 200...jumla ambayo ilipindukia 1,000 hapo zamani." Anasema Bhima.
Bustani ya Liwonde, kusini mwa nchi hiyo - na kutolewa katika mipaka ya nchi - inatoa baadhi ya matumaini. Kikundi cha ndovu kilioko huko, kinasemekana kwamba hali yake ni tulivu. Imekaridiwa kwamba Malawi hivi sasa ina ndovu wapatao 2,500. Bhima anasema kwamba maafisa wa Malawi na Zambia wanajdili mradi wa pamoja unaovuka mipaka ya nchi mbili, juu ya kulinda maeneo ya mpaka wao wa pamoja -- yaani mbuga za taifa za Kasungu, Zambia Nyika na Malawi Nyika. Mradi huo unagharimiwa na Wakfu wa Mbuga za Amani wenye makao yake nchini Afrika Kusini, ambao mlezi wake ni rais wa zamani Nelson Mandela. Kwa mujibu wa Banda, juhudi za kuimarisha sheria dhidi ya ujangili zinaendelea kujadiliwa. Sheria ya Mbuga za Taifa na Wanyamapori zilipitiwa katika mwaka 1999 na 2000. Lakini mabadiko hayakupitishwa. Utaratibu wa sera ni masuala ya mfululizo," alisema. Naibu Mkurugenzi wa Mbuga na Wanyamapori anayehusika na usimamizi wa wanyamapori, Humphrey Nzima, amesisitiza pia umuhimu wa kuizindua jamii nzima ya Malawi juu ya haja ya kuhami ndovu.
"Bila shaka uungaji mkono wa wanasiasa, watalamu wa sheria na jamii kwa jumla, ni muhimu kwa hifadhi nchini humu mnamo siku zijazo," alisema. Malawi hivi sasa inajaribu kujenga mfumo wa biashara ya utalii kwa msaada wa wanamapori kama kivutio chake kikubwa, kwa madhumuni ya kujipatia fedha za kigeni.
Biashara haramu ya meno ya ndovu inanawiri kwa sababu ya mahitaji makubwa maskariki mwa Eshia. "Waokoe Ndovu", kikundi cha hifadhi chenye makao yake nchini Uingereza na Kenya, kilizialika nchi kadha Mashariki ya Mbali mwaka jana, kuchunguza jinsi meno ya ndovu yanavyouzwa katika eneo hilo na kwengineko.
Watafiti Esmond Bradley Martin na Daniel Stiles wanakiri kwamba hali ya mambo inatia wasiwasi mkubwa nchini China, ambako alisema ilipokea tani 40 za peme za tembo mnamo miaka mitano iliyopita. Timu hiyo iligundua vifaa 270,000 vya meno ya ndovu kwaajili ya kuuzwa barani Afrika na Eshia.
Mkataba wa CITES ulipiga marufuku uuzaji wa meno ya ndovu katika mwaka 1990 ili kuwahami tembo ambao wamekuwa shabaha ya biashara hii ya faida kubwa ya fedha. Kwa mujibu wa Shirika la Uchunguzi wa Mazingira, kikundi cha wahifadi chenye makao yake nchini Uingereza na Marekani, jumla ya tembo barani Afrika imepungua kuanzi amilioni 1.3 hadi 624,000 mnamo mwongo uliotangulia kipindi kilichopiga marufuku biashara ya pembe za tembo.
Na hadi hapo tumefikia mwisho wa makala hii ya Mtu na Mazingira Kutoka Redio Duetsche Welle, Bonn, Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Ni Shaaban Mohamed nikisema asanteni kwa kutusikiliza.