1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Europa: Leverkusen na Man U watoka na alama tatu

Sylvia Mwehozi
10 Machi 2023

Dura ya kwanza ya mechi za raundi ya 16 bora imechezwa ambapo jumla ya mechi 8 ziliunguruma katika viwanja mbalimbali barani Ulaya. Manchester United walikutana na Real Betis, huku Juventus wakichuana na Freiburg.

https://p.dw.com/p/4OTyH
UEFA Europa League | Bayer Leverkusen - Ferencváros Budapest
Picha: Frederic Scheidemann/Getty Images

Bayer Leverkusen ya Ujerumani ambayo imepata alamu tatu muhimu kuelekea hatua ya robo fainali baada ya kuwatandika mabingwa wa Hungary Ferencvaros mabao 2-0. Leverkusen inayoshikilia nafasi ya tisa katika ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga, ilipata bao la mapema katika dakika ya 10 ya mchezo kutoka kwa Kerem Demirbay na bao la pili limefungwa na Edmond Tapsoba na kuwanyanyua mashabiki wa Leverkusen ambayo ni mabingwa wa Kombe la UEFA mwaka 1988.Ndoto ya robo fainali ya Dortmund yazimwa na Chelsea

Union Berlin wanaoshikilia nafasi ya tatu katika Bundesliga, walitoka nyuma na kusawazisha mabao 3 dhidi ya Union Saint-Gilloise ya Ubelgiji ambayo iko nafasi ya pili katika ligi. Victor Boniface alipachika mabao mawili ya Unioni Saint-Gilloise katika dakika ya 28 na 72 huku bao la tatu likifungwa na Yorbe Vertessen katika dakika ya 58. Mabao ya Unioni Berlin yalitiwa kimiani na Josip Juranovic dakika ya 42, Robin Knoche dakika ya 69 na bao la tatu likifungwa na Sven Michel katika dakika ya 89 ya mchezo.

UEFA Europa League | Bayer Leverkusen - Ferencváros Budapest
Ligi ya Europa: Adam Hlozek wa Bayer Leverkusen akijaribu kuwatoka wachezaji wa Ferencvarosi Picha: Frederic Scheidemann/Getty Images

Vinara wa ligi kuu ya Premier Arsenal wametoka sare ya mabao 2-2 na Sporting Lisbon. Arsenal waliokuwa ugenini walitawala mchezo huo katika dakika za mwanzoni na hatimaye kujipatia bao la kwanza dakika ya 22 kupitia kwa William Saliba lakini Sporting walisawizisha dakika 12 baadae kupitia goli la Goncalo Inacio. Bao la Inacio liliwaamsha mashabiki wa Sporting na kufikia dakika ya 55, Sporting walikuwa mbele kwa bao 2-1. Arsenal walipambana na kusawazisha bao la pili kutoka kwake Morita katika dakika ya 62 na hivyo kumaliza mchezo huo kwa sare.Liverpool, Madrid kuumana Ligi ya Mabingwa

AS Roma ya Jose Mourinho imeitandika Real Sociedad ya Uhispania bao 2-0 shukrani kwa bao la mapema lililotoka kwa Stephan El Shaarawy na bao la kichwa la Marash Kumbulla. Mchezaji wa Sociedad Mikel Merino awali alikosa nafasi nzuri ya kusawazisha.

Wakiwa bado na jinamizi la kichapo cha bao 7-0 Manchester United wameibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Real Betis. Magoli ya Manchester United yamefungwa na Rashford dakika ya 6, Antony dakika ya 52, Bruno Fernandes dakika ya 58 na Wout Weghorst dakika ya 82. Betis walipata bao moja la kufutia machozi kutoka kwake Perez dakika ya 52.

Angel Di Maria wa Juventus amepachika bao lake la nne mfululizo katika ligi ya europa wakati Juventus walipovaana na  Freiburg ya Ujerumani na kushinda bao 1-0. Ushindi wa michuano ya ligi ya Europa kutaipa Juventus nafasi thabiti ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwani wako pointi 12 kutoka kwenye nafasi nne za juu kwenye ligi ya Serie A. Sevilla wameshinda magoli 2-0 dhidi ya Fenerbahce wakati Shaktar Donetsk ikitoka sare ya ya bao 1-1 dhidi ya Feyenoord.