1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa kiwango gani Ujerumani inautambua uovu wa ukoloni wake?

Mohammed Khelef
27 Aprili 2021

Mauaji, uporaji wa sanaa, wizi wa mafuvu: yote ni sehemu ya sauti zinazopazwa kuitaka Ujerumani kutambuwa historia yake ya kikoloni miaka minne baada ya serikali kuahidi kuliangalia upya suala hili. Je, imefikia wapi?

https://p.dw.com/p/3se1g
Deutsch-Südwestafrika Zeichnung Hereroaufstand 1904/5

"Alama za ukoloni wa Kijerumani zipo wazi kabisa kwa mwenye kutaka kuziona", anasema Naita Hishoono kutoka Nambia.

Ukitembea kwenye mitaa ya mji mkuu, Windhoek, unakutana na majina ya mitaa ya Kijerumani, maduka ya Kijerumani, na hata kanisa lililojengwa wakati wa ukoloni wa Mjerumani.

Juu ya yote, unakutana na picha ya kuogofya ya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa jamii za Herero an Nama yaliyofanywa na vikosi vya Kijerumani.

Kwa kila hali, ni ukurasa mbaya sana kwenye kitabu cha historia ambacho kila Mnamibia anakijuwa, lakini ni mada ambayo haipewi uzito wowote nchini Ujerumani. 

Kwa Hishoono anayeongoza taasisi isiyo ya kiserikali, National Institute for Democracy, tafauti juu ya namna Wajerumani na Wanamibia wanavyouchukulia uhalifu wa Ujerumani wakati wa ukoloni ni kubwa sana. 

"Wanamibia tunaufahamu sana ukoloni kwa sababu tunauona kwenye majengo, tunauona kwenye athari za kiuchumi, tunauona na tunaishi nao kila siku. Lakini nchini Ujerumani, hata mumeshasahau kabisa kwamba nchi hii iliwahi kuwa na makoloni," alisema kwenye kongamano lililoitishwa na Taasisi ya GIGA ya Masomo ya Kiafrika iliyopo mjini Hamburg.

Ujerumani yaanza kukiri

Deutsch-Südwestafrika Holzstich Hereroaufstand 1904/5
Mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wajerumani dhidi ya Waherero nchini Namibia mwaka 1904.Picha: akg-images/picture alliance

Mtazamo huo unaungwa mkono na Waziri wa Sera ya Utamaduni wa Kitaifa wa Ujerumani, Michelle Müntefering, ambaye alipozungumza bungeni hivi karibuni alisema umewadia wakati wa kuukiri ukweli.

"Sisi, hapa Ujerumani, tumejiachia na dhana kwamba tumetoka kwenye zama za ukoloni tukiwa na vyuma vichache vichakavu ama kwamba ukoloni wa Kijerumani ulikuwa wa muda mfupi mno kuweza kuleta madhara ya muda mrefu." Alisema waziri huyo.

Ni kweli kuwa Ujerumani ilikuwa taifa la kikoloni kwa muda mchache, ikizikalia nchi za Kiafrika mwishoni mwa miaka ya 1800 na kisha ikapoteza makoloni yake wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Lakini hata ndani ya Ujerumani kwenyewe, bado nyayo za ukoloni huo zingalipo, japokuwa hazijioneshi waziwazi. 

Kuna mitaa na masanamu na majengo kadhaa yenye majina ya kuwatukuta Wajerumani wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa zama za ukoloni. Makoloni ya zamani yanaorodhesha madai ya kazi za sanaa zilizomo sasa kwenye makumbusho za Ujerumani ambazo ziliporwa kutoka mataifa ya Kiafrika wakati wa ukoloni.

Imechelewa na inayoyafanya hayajatosha

Namibia Windhuk | Denkmal zur Erinnerung an den Völkermord an den Herero und Nama
Sanamu ya mauaji ya Wajerumani dhidi ya Waherero nchini Namibia mwaka 1904.Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz

Iliichukuwa serikali ya Ujerumani zaidi ya miaka 100 kukiri rasmi matendo maovu ya ukoloni wa nchi hii barani Afrika. Mwaka 2018, muungano wa vyama vinavyotawala vya CDU/CSU na SPD ulikubaliana kuchukuwa mtazamom mpya kuelekea historia ya ukoloni ya Ujerumani.

Kwa mujibu wa Müntefering, serikali imechukuwa hatua ya kutunga baadhi ya sheria. Kwa hakika, imeanza hata kuchukuwa hatua mpya, kwa makumbusho za Ujerumani kutakiwa zieleze vipi zinataka kuendelea kushughulikia mali zilizoporwa wakati wa ukoloni.

Kimsingi kabisa, kumeanzishwa kitengo maalum ambacho kinayawezesha makoloni ya zamani kudai kurejeshewa mali zao hizo.

Kwa upande mwengine, wanasiasa nao wanazidi kujihusisha na suala hili. Kwa mfano, Waziri wa Utamaduni Monika Grütters amewaalika wadau kwenye mkutano wa kujadiliana hatima ya kazi za sanaa kutoka Benin, ambazo zinachukuliwa kama ngawira ya ukoloni, lakini Nigeria inataka zirejeshwe kwao.

Majumba ya makumbusho yamerejesha mabaki ya mifupa ya binaadamu yaliyoletwa nchini Ujerumani wakati wa ukoloni kwa kile kiitwacho uchunguzi wa kisanyansi.

Miji imeanza kuibadilisha mitaa majina iliyopewa kuwatukuza wakoloni na Ijumaa iliyopita (23 Aprilki) ilikuwa ni zamu ya Mtaa wa Wissmann mjini Berlin, ambao ulikuwa umepewa jina la Herman von Wissman, aliyetumia ukatili wa kutisha dhidi ya uasi wa Waafrika kwa kile kilichoitwa Dola la Ujerumani la Afrika Mashariki, mwanzoni mwa miaka ya 1900.