1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Togo akubali jukumu la upatanishi Mali

5 Mei 2022

Rais wa Togo Faure Gnassingbe amekubali kuwa mpatanishi katika mzozo wa kisiasa wa Mali huku jeshi la serikali ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi likikabiliwa na shinikizo la kurejesha utawala wa kiraia

https://p.dw.com/p/4At41
Togos Präsident Faure Gnassingbe
Picha: picture alliance/Xinhua News Agency/Li Xueren

Kauli hiyo imetolewa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili. Mali imekuwa katika msukosuko tangu jeshi kunyakua mamlaka katika taifa hilo la Sahel mnamo Agosti mwaka 2020, huku mazungumzo yakiendelea juu ya muda unaohitajika ili kurejesha utulivu wa kikatiba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop na mwenzake wa Togo waliwaambia waandishi wa habariJumatano jioni katika mji mkuu wa Togo Lome kwamba Gnassingbe amekubali kuwa mwezeshaji katika mgogoro huo.

Soma zaidi:Mali yaishtumu Ufaransa kwa ukiukaji wa anga lake kupeleleza wanajeshi

Diop amesema, walimwomba Rais Faure Gnassingbe kutumia ofisi yake nzuri, hekima na uzoefu kuwezesha mazungumzo na watendaji wa kikanda pamoja na mazungumzo mapana zaidi na jumuiya nzima ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo Robert Dussey alithibitisha kuwa ombi hilo lilikubaliwa.

Awali, utawala wa kijeshi wa Maliuliahidi kurejesha utawala wa kiraia, lakini umewekewa vikwazo baada ya kushindwa kutimiza ahadi kwa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ya kufanya uchaguzi mwezi Februari mwaka huu.

Diop amesema kutokana na hali ya usalama nchini Mali na hitaji la mageuzi, nchi hiyo itahitaji miaka miwili kurejea katika utaratibu wa kikatiba.

Uhusiano wa Mali na Ufaransa wadorora

Uhusiano kati ya serikali ya kijeshi ya Mali na mkoloni wake wa zamani Ufaransa pia umedorora, na siku ya Jumatatu Mali ilitangaza kujitenga na makubaliano yake ya ulinzi na Ufaransa na kulaani "ukiukaji wa wazi" wa uhuru wake wa kitaifa unaofanywa na wanajeshi wa Ufaransa.

Mali Oberst Assimi Goita, Anführer der malischen Militärjunta
Assimi Goita, kiongozi wa utawala wa kijeshi MaliPicha: Francis Kokoroko/File Photo/Reuters

Serikali ya Mali ilisema Ufaransa haina tena "msingi wa kisheria" wa kuendesha operesheni za kijeshi nchini humo baada ya Bamako kuachana na mikataba muhimu ya ulinzi, katika duru ya hivi karibuni ya mzozo kati ya washirika hao wawili wa zamani.

Soma zaidi:Baerbock atoa wito kwa Mali kuacha kushirikiana na Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop alitangaza kwenye runinga ya taifa kwamba itachukua miezi sita kwa hatua hiyo kutekelezwa kwa makubaliano ya mwaka 2014, huku akisisitiza kuwa mikataba iliyotiwa saini mwaka 2013 na 2020 kuhusu shughuli za vikosi vya Barkhane na Takuba itaanza kutekelezwa mara moja. 

Kiongozi wa kijeshi wa Mali Assimi Goita alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2020 kufuatia maandamano dhidi ya jinsi serikali ilivyoshughulikia vita dhidi ya mashambulizi ya makundi ya kigaidi nchini humo.

Goita alifanya mapinduzi mengine mwaka 2021 ili kuwatimua viongozi wa kiraia na akaapishwa kama rais wa muda,na amekuwa akiutupilia mbali wito wa kimataifa wa kufanya uchaguzi.