1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaanza juhudi mpya ya mashambulizi Gaza

Sudi Mnette
5 Januari 2024

Israel imetangaza maeneo lengwa zaidi mapya katika kuwawinda wapiganaji wa Hamas na viongozi wao katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4at40
Gazastreifen Rauch über Rafah
Picha imepigwa eneo la Rafah ikionyesha moshi ukifuka juu ya mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza wakati wa mashambulizi ya Israel Januari 5, 2024.Picha: AFP via Getty Images

Hayo yanatokea katika kipindi hiki ambacho pia mashambulizi yake ya  anga yakizidishwa katika Ukanda wa Gaza, na kulazimisha baadhi ya familia zisizo na makazi katika eneo hilo kulikimbia kwa kutumia mikokoteni inayokokotwa na punda. Familia hizo zimeonekana zikiwa pia na idadi kadhaa ya watoto pamoja na mizigo yao muhimu.

Awali, Alhamis mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yameripotiwa kuwauwa Wapalestina zaidi ya 20, ikiwa ni pamoja na 16 katika mji wa Khan Younis uliopo kusini mwa eneo la pwani uliosheheni idadi kubwa ya watu ambao wamekimbia kutoka sehemu nyingine.

Vifo vya watoto tisa katika mashumbulizi

Mamlaka katika eneo hilo la Gaza ilisema miongoni mwa waliuwawa ni watoto tisa. Katika tukio tofauti maafisa wa afya wamsema Wapalestina watano wameuawa katika shambulizi la anga la Israel lililolenga gari katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nusseirat. Wakaazi wa Gaza walisema ndege na vifaru vya Israel pia vilishambuliwa kambi nyingine mbili za wakimbizi, jambo lililofanya watu wengi kuelekea upande wa kusini.

Gazastreifen Zerstörung in Rafah
Picha iliyopigwa Januari 5, 2024 inaonyesha majengo yaliyoharibiwa wakati wa mashambulizi ya Israel huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: AFP via Getty Images

Duru kutoka Ukanda wa Gaza zinasema kwa usiku wa Alhamis, ndege na vifaru vya kivita vya Israel vilizidisha mashambulizi yao kuelekea upande wa mashariki wa kambi za Al-Maghazi na Al-Nusseirat.

Israel yatangaza operesheni mpya ya kuwasaka Hamas

Hayo yanafanyika katika kipindi ambacho pia Waziri wa Ulinzi  wa Israel Yoav Gallant akiwa tayari, Alhamis amekwishatoa taarifa ya hatua mpya ya vita vya Israeli huko Gaza akionesha kuyalenga zaidi  maeneo ya kaskazini na kuwatafuta zaidi viongozi wa Hamas kama sehemu ya jitihada ya Israel ya kushinikiza kuwaachiwa huru mateka waliosalia wanaoshikiliwa na Kundi la Hamas.

Gallant amesema kwamba operesheni katika eneo la kaskazini itajumuisha uvamizi, ubomoaji wa mahandaki, mashambulizi ya angani na na operesheni za vikosi maalumu.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani Anthony Blinken ziarani Mashariki ya Kati

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani Anthony Blinken anarejea tena katika eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa ni safari yake ya nne tangu kuanza vita vya Hamas na Israel. Lakini safari hii anatarajiwa kufanya mazungumzo magumu, huku akishinikiza msaada mpya wa haraka kwa Gaza.

USA Aussenminister Blinken auf dem Weg in den Nahen Osten
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akipunga mkono wakati akipanda ndege kuondoka Washington kuelekea Mashariki ya Kati.Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Matthew Miller ambae ni Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani anafafanua zaidi kuhusu ziara hiyo. "Hatutarajii kila mazungumzo katika safari hii kuwa rahisi. Ni wazi kuna masuala magumu yanayokabili eneo hili na chaguo ngumu mbeleni. Lakini waziri huyo anaamini ni jukumu la Marekani kuongoza juhudi za kidiplomasia kukabiliana na changamoto hizo ana kwa ana. Na yuko tayari kufanya hivyo katika siku zijazo." Alisema afisa huyo.

OCHA inasema mashirika kiutu yashindwa kutekeleza majukumu yao Gaza.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya dharura OCHA limetoa taarifa ya kushindwa kwa siku kadhaa sasa, kutoa huduma na kusafirisha misaada ya kibinadamu kwa mashirika ya kimataifa kaskazini mwa Gaza. Imesema watu takribani 100,000 wanahitaji mahitaji hayo kaskazini mwa Gaza.

Uvamizi huu wa Israel katika Ukanda wa Gaza ulikuwa ni jibu kwa mashambulizi ya Hamas na makundi mengine nchini Israel ya Oktoba 7, ambapo watu 1,200, wakiwemo raia 800 waliuwawa, huku upande wa Hamas ukieleza idadi ya waliuwawa tangu wakati huo kufikia 22,438, wengi wao raia.

Vyanzo: RTR/AFP/DPA