1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Narges Mohammadi ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel

Sudi Mnette
6 Oktoba 2023

Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huu imekwenda kwa mwanaharakati wa Iran aliyefungwa gerezani, Narges Mohammadi kutokana na kupambana na ukandamizaji wa wanawake nchini humo.

https://p.dw.com/p/4XCGW
Mwanahakati wa haki za wanawake nchini Iran Narges Mohammadi aliyetunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2023 kutokana na juhudi zake za kuwapigania wanawake
Mwanahakati wa haki za wanawake nchini Iran Narges Mohammadi aliyetunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2023 kutokana na juhudi zake za kuwapigania wanawakePicha: Magali giardini/AP Photo/picture alliance

Akiwasilisha kwa umma tangazo hilo mjini Oslo, mwenyekiti wa kamati ya tuzo ya Nobel Berit Reiss-Andersen amemtaja Narges Mohammadi kuwa ni mtu anaepigania wanawake dhidi ya ubaguzi wa kimfumo na ukandamizaji.

"Kamati ya Nobel ya Norway imeamua kumpa Narges Mohammadi Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2023 kwa mapambano yake dhidi ya ukandamizaji wa wanawake nchini Iran na mapambano yake ya kuunga mkono haki za binadamu na uhuru kwa wote," alisema Bi. Reiss-Andersen.

Soma pia: UN yaitaka Iran kufuta sheria mpya kali ya hijab

Mwezi Novemba mamlaka nchini Iran ilimtia mbaroni Mohammadi, baada ya kuhudhuria kumbukumbu ya wathiriwa wa maandamano yalogubikwa na ghasia ya mwaka 2019. Kimsingi Mohammadi ana rekodi ndefu za kifungo, hukumu kali na kuwepo kwa miito ya kimataifa kuhusu kushughulikiwa kwa kesi zinazomuhusu.

Mwenyekiti wa kamati ya Tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel Berit Reiss-Andersen akitangaza tuzo hiyo kwa mwaka 2023
Mwenyekiti wa kamati ya Tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel Berit Reiss-Andersen akitangaza tuzo hiyo kwa mwaka 2023 Picha: Heiko Junge/NTB/AFP

Kazi ya Narges Mohammadi kabla ya kifungo

Kabla ya kukamatwa na kufungwa, Mohammadi alikuwa makamo wa rais wa shirika lililopigwa marufuku nchini Iran la utetezi wa haki za binaadamu. Kadhalika amekuwa mtu wa karibu sana  na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2003 nae pia Muiran,  Shirin Ebadi, ambaye alianzisha shirika hilo alilokuwa akihudumu.

Soma pia: Iran: Waandamanaji waadhimisha mwaka mmoja wa ukandamizaji wa vikosi vya usalama Zahedan

Ebadi alikimbia nchini Iran baada ya duru ya pili ya uchaguzi uliomrejesha tena Rais Mahmoud Ahmadinejad wa mwaka 2009, ambao ulisababisha maandamano makubwa na ukandamizaji uliofanywa na mamlaka.

Mwaka 2018, Mohammadi, ambae kitaaluma ni mhandisi alipata tuzo ya haki za binadamu ya  Andrei Sakharov kwa mwaka huo. Mohammadi alisimamishwa kizimbani kwa dakika tano tu na kuhukumiwa miaka minane gerezani na viboko sabini juu.

Tuzo za Nobel hubeba zawadi ya pesa taslimu ya karibu dola milioni 1

Tuzo za Nobel huhusisha zawadi ya pesa taslimu ya karibu dola milioni 1. Washindi pia hupokea medali ya dhahabu ya karati 18 na heshima nyingine katika hafla ambayo kwa kawaida hufanyika mwezi Desemba.

Wawakilishi wa washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2022 iliyokwenda kwa wanaharakati wa nchini Ukraine na Belarus
Wawakilishi wa washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2022 iliyokwenda kwa wanaharakati wa nchini Ukraine na Belarus Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Kwa mwaka uliopita tuzo zilikwenda kwa wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Ukraine, Belarus na Urusi, katika kile kilichoonekana kushiriki kwao katika karipio kali kwa Rais Vladimir Putin na  mshirika wake wa Belarus. Kimsingi tuzo hii inatolewa kwa mtu mmoja mmoja au shirika.

soma pia: Tuzo ya Amani ya Nobel 2022 yawaendea wanaharakati wa haki za binadamu

Kwa rekodi washindi wengine waliopita ni pamoja na Nelson Mandela, Barack Obama, Mikhail Gorbachev, Aung San Suu Kyi na Umoja wa Mataifa. Tofauti za ilivyozoeleka washindi wa tuzo ya amani ya Nobel wanachaguliwa na kutangazwa mjini Stockholm, mwasisi wake Alfred Nobel safari hii amefanya uamuzi wa kutangazwa na kutolewa mjini Oslo na wajumbe watano wa Kamati ya Nobel ya Norway.

Jopo hilo huru limeteuliwa na bunge la Norway. Na kwa mwaka huu kamati hiyo mapendekezo   351 yale yanye kuhusu mtu mmoja mmoja mmoja 259 na makundi au mashirikia  92. Watu wanaoweza kufanya uteuzi ni pamoja na washindi wa zamani wa Tuzo ya Amani ya Nobel, wajumbe wa kamati, wakuu wa nchi, wabunge na maprofesa wa  sayansi ya siiasa, historia na sheria za kimataifa.

Awali Jumatano, kamati ya Nobel ilimtunukia tuzo ya fasihi mwandishi wa Kinorway Jon Fosse. Tuzo ya kemia ilienda kwa wanasayansi wa Marekani, Moungi Bawendi, Louis Brus na Alexei Ekimov. Lakini pia Jumanne kwa upande wa ujuzi katika sayansi ya fizikia tuzo ilikwenda kwa mwanafizikia mwenye asili ya Kifaransa na Uswisi, Anne L'Huillier, mawasayansi wa Ufaransa Pierre Agostini mwingine mzaliwa wa Hungary, Ferenc Krausz.